Dar es Salaam. Kada mpya wa Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina ameibua shangwe kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa chama hicho, wakati akiingia ndani ya ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Sio yeye pekee bali hata mtiania urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman aliibua shangwe baada ya jina lake kutangazwa na kutakiwa kwenda jukwaani kuwasalimia wajumbe wa kamati kuu.
Shangwe zimetokea leo Jumatano Agosti 6, 2025 katika mkutano mkuu maalumu wa chama hicho unaoendelea ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo pia utawapitisha watiania urais wa Tanzania na Zanzibar.

Mpina ambaye ni mbunge wa zamani wa Kisesa ameingia ukumbini hapo kimyakimya ambapo ni wajumbe wachache walimuona kupitia televisheni iliyopo mbele wakati Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ( THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa akizungumza.
Wakati akiendelea kutoa salamu, utulivu ukaanza kukosekana kwa wajumbe baada ya wanahabari kwenda moja kwa moja kwenye eneo aliloketi Mpina kwa ajili ya picha.
Ili kuweka utulivu kwa wajumbe wa mkutano huo, ilimlazimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kuiwahisha ratiba ya utambulisho wa watiania wa urais tofauti na ilivyopangwa hapo awali kuwa watatambulishwa jioni.

“Kwa vile msajili msaidizi wa vyama vya siasa (Sisty Nyahoza) amekugusia suala la wagombea ngoja niwatambulishe ingawa ratiba yao ilikuwa baadaye. Nawaomba niwaite kabla ya Kiongozi wa chama hajafika kutoa hotuba yake,” amesema Ado.
Baada ya hapo, Ado alianza kumuita Othman ambaye ni Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, kwenda mbele ya jukwaa kuu kuwapungia mkono wajumbe wa mkutano mkuu maalumu.
Alipoitwa ukumbi ulilipuka kwa shangwe na vigeregere kwa mtiania huyo, kisha akafuata mtiania Aaron Kalikawe anayewania naye akashangiliwa. Lakini funga kazi ilikuwa kwa Mpina aliyeitwa ambapo karibu wajumbe wote walisimama na kumshangilia.

“Sasa hapa naweza kumwita Kiongozi wa chama (Semu) aje kuhutubia maana utulivu kupatikana,” amesema Ado baada ya kuwatambulisha watiania urais hao.
Watiania urais watatu hao watapigiwa kura za maoni hapo baadaye ili kuwapata watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Endelea kufuatilia Mwananchi