Mtego wa ACT Wazalendo kuvuna wanaotemwa CCM

Dar es Salaam. Nyuma ya hatua ya kusogezwa mbele mara kwa mara kwa mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu katika Chama cha ACT Wazalendo yamejificha mengi, wachambuzi wa siasa wanaeleza.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, ni mbinu ya kawaida kwa vyama vya upinzani, kuweka mitego ya kuwanasa wanasiasa mashuhuri watakaotengwa na vyama vyao katika michakato ya ndani ya kuusaka urais, ubunge na udiwani.

Wanasema jambo hilo linapata baraka zaidi hasa ukizingatia, halivunji matakwa ya Katiba wala kanuni za chama husika, badala yake kinatengeneza njia za kujiimarisha kisiasa kwa kuvuna wanasiasa wenye ushawishi.

Mitazamo hiyo ya wachambuzi wa siasa, inajibu kile kilichoshuhudiwa ndani ya ACT Wazalendo, kusogeza mbele kwa takriban mara nne, mchakato wake wa ndani wa uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge na udiwani.

Kwa mara ya kwanza, chama hicho kilitangaza kufungua pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo Aprili 28, kikitangaza mchakato huo ungekoma Mei 15, mwaka huu.

Baadaye, kilitangaza kuongeza muda, badala ya Mei 15 sasa ni 25 kwa urais wa Zanzibar na Mei 31 kwa ubunge, uwakilishi na viti maalumu.

Hakikuishia hapo, ilipofika Juni 8, 2025 kilitangaza kusogeza mbele tena mchakato huo, kuanzia Juni 8 hadi 30, mwaka huu, badala ya kuja na tangazo lingine la kimya kimya kuanzia Julai 15, 2025.

Kwa mara ya mwisho, chama hicho, kimesogeza muda tena ya uchukuaji na urejeshaji hadi Agosti 4, mwaka huu, jambo ambalo wadau wa siasa wanalihusisha na mbinu za kuwanasa wanasiasa mashuhuri.

Hata hivyo, ACT Wazalendo inayafanya hayo, katikati ya michakato ya vyama vingine kikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kwa sasa kipo katika hatua za mwisho kukamilisha uteuzi.

Katika uteuzi huo, waliokuwa wabunge wa Bunge la 12 zaidi ya 40 wameachwa na wengine wanatarajiwa kuachwa baada ya kura za maoni.

Kati ya wanasiasa hao waliotemwa kwenye mbio za ubunge ndani ya CCM, aliyekuwa Mbunge wa Kisesa kwa miaka 20, Luhaga Mpina ndiye anayetajwa tayari kuwa karibu kujiunga na chama hicho cha upinzani.

Ukiacha Luhaga Mpina, nyavu za ACT Wazalendo katika kusogeza mbele michakato yake, zilitega kuwanasa pia waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu wa Chadema na tayari kilishamnasa mmoja, Naghenjwa Kaboyoka.

Tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hadi huu wa sasa unaosubiriwa kwa hamu mwaka 2025, historia inaonyesha kuwa walioachwa na CCM si watu wa kubezwa, bali mara nyingi ni majina makubwa yenye ushawishi, mtandao na ari ya kisiasa. Kwa vyama vya upinzani, hawa huwa dhahabu.

Mwaka 1995 ulifungua ukurasa mpya katika siasa za Tanzania kwa kuruhusu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Huu ndio ulikuwa mwanzo wa mchakato wa kutengwa kwa baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM, waliotafuta hifadhi upinzani.

Augustino Mrema, aliyekuwa Waziri mashuhuri wa Mambo ya Ndani, alihama CCM baada ya mvutano wa ndani na kujiunga na NCCR-Mageuzi, kilichokuwa chama kipya wakati huo. Aligombea urais na kupata asilimia 27.77 ya kura, akishika nafasi ya pili nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM.

Mrema alionyesha kuwa waliokataliwa ndani ya CCM wanaweza kuwa nguvu ya kweli upinzani.

Mwaka huohuo, Mabere Marando, mwanasheria na mwanasiasa machachari, naye aliachana na CCM na kuwa mmoja wa waanzilishi wa NCCR-Mageuzi. Baadaye akahamia Chadema akiwa Katibu Mkuu. Kwao, kupigwa breki CCM ilikuwa tu tiketi ya kuanza sura mpya ya kisiasa.

Miaka ya 2000 na 2005 haikushuhudia uhamaji mkubwa, lakini migongano ya ndani ya CCM iliendelea kuibua minong’ono ya kutoridhika. Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, alianza kuonekana kutofautiana na uongozi wa juu wa chama chake baada ya mchakato wa kumpitisha mgombea urais mwaka 2005. Hata hivyo, hakuhama rasmi hadi baadaye.

Dk Wilbrod Slaa, aliyekuwa Padri na baadaye mwanasiasa, alihama CCM na kujiunga na Chadema. Mwaka 2010 aligombea urais kwa tiketi ya Chadema, na kupata asilimia 27 ya kura. Slaa aliweka msingi wa upinzani makini uliotokana na watu waliokulia CCM.

Hakuna mwaka ulioleta uhamaji mkubwa wa kisiasa kama 2015. Wanasiasa wakubwa walitemwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia CCM na wakaamua kusaka hifadhi upinzani.

Hayati Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu na mwanachama maarufu wa CCM, alikatwa dakika za mwisho katika mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho.

Alijibu kwa kishindo kwa kujiunga na Chadema, na kupitia muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, na NLD, akapewa tiketi ya kugombea urais.

Lowassa alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97, akishindwa na Dk John Magufuli wa CCM aliyepata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46. Hili lilikuwa pigo kubwa kwa CCM, kwa sababu sehemu kubwa ya wanachama wake walihamia upinzani wakifuatana na Lowassa.

Wengine waliomfuata ni pamoja na Frederick Sumaye, aliyekiri kuwa CCM imekosa dira na kupotoka kwenye misingi ya Azimio la Arusha. Wote walikuwa waliokatwa na chama tawala, lakini wakawa vichwa vya upinzani.

Uchaguzi wa 2020 ulifanyika katika mazingira magumu kwa upinzani, huku viongozi wengi wakilalamikia kunyimwa nafasi za kufanya siasa. Hakukuwa na uhamaji mkubwa kama wa 2015, lakini hali ya kutoridhika ndani ya CCM iliendelea kukua kimya kimya.

Mwaka huu 2025, tayari CCM imeshuhudia maelfu ya wanachama wakijitokeza kuwania nafasi mbalimbali. Zaidi ya wagombea 30,000 wameomba udiwani na mamia wamejitokeza kuwania ubunge. Hili lina maana moja, idadi ya watakaokatwa ni kubwa kuliko nafasi zilizopo.

January Makamba, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, ametemwa katika jimbo lake na huenda akasaka njia mbadala.

Mrisho Gambo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa na Mbunge wa Arusha Mjini, naye ametupwa nje ya mchakato na vyama vya upinzani tayari vimeanza kumwinda.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa, wamesema hatua ya ACT Wazalendo kuongeza muda mara kwa mara si jambo baya na hawakiuki katiba ya chama chao, kwa sababu wana lenga kupata watiania watakaowasimamisha katika uchaguzi Oktoba.

Pia, walibainisha kuwa hatua ya ACT Wazalendo kusogeza mbele mara kwa mara chama hicho, kinalenga kuwapata makada wapya watakaotemwa kwenye mchujo wa kura za maoni za CCM uliofanyika Agosti 4, 2025.

Sio CCM pekee bali chama hicho kimewategea ndoano ya kuwanasa makada wengi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho hakitashiriki uchaguzi mkuu, baada ya kushindwa kusaini Kanuni za Maadili ya mchakato huo.

Ingawa miongoni mwa wachambuzi hao, alionyesha hofu kuhusu hatua hiyo, akisema huenda ikawavunja moyo makada waandamizi wa ACT Wazalendo waliochukua na kurejesha fomu na kufikia hatua ya kuhoji kwanini chama hicho kimefikia hatua kusogeza mbele kila kukicha.

“Pamoja na sababu walizozitoa, nadhani wamelenga zaidi kuvuna makada wapya kutoka CCM watakaotemwa kwenye mchujo wa kura za maoni, lakini si hao bali hadi kutoka Chadema ambao bado wapo njiapanda hawajui waende wapi,” amesema.

“Sioni kosa ACT Wazalendo kusogeza muda mbele wa uchukuajia na urejeshaji wa fomu za udiwani na ubunge, kwa sababu hawavunji katiba yao, lakini ni sehemu ya mkakati wa kujiimarisha ili kupata watiania wa kutosha kwenye uchaguzi wa baadaye,” amesema Dk Aviti Mushi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Kiama Mwaimu alianza kukubaliana na mawazo ya Dk Mushi, akisema kinacholengwa zaidi ni kuwapata makada watakaotemwa na CCM katika mchakato wa kura za maoni.

“Hapa ACT Wazalendo, inawategea CCM kwa kuhakikisha watiania watakaokatwa kwenye kura za maoni wahamie katika chama chao. Jambo hili si baya ndio mambo ya siasa, lakini hofu yangu itawakatisha tamaa makada waandamizi wa chama watahisi nafasi zao zitapokonywa.”

“Kikubwa ACT Wazalendo, wacheze ndani ya kalenda ya INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi) kwa kuhakikisha wanamaliza michakato yao kabla ya pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani na ubunge halifunguliwa kuanzia Agosti 14, 2025 hadi Agosti 27,” amesema Mwaimu.

Taarifa zilizopo zinaeleza huenda baada ya Agosti 4, kutamatika, mchakato huo ukasogezwe tena mbele kulingana na mapendekezo mahususi ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, ambayo imekuwa ikifanya utafiti wa majimbo yatakayaokuwa na muhimu na kutoa fomu hizo.

Kwa upande wa Mchambuzi wa Siasa, Dk Lazaro Swai anasema kinachofanywa na chama hicho, kinafanywa na kila chama cha upinzani makini chenye malengo ya kukua.

Kwa mazingira ya siasa za Tanzania, anasema ni vigumu kwa chama cha upinzani kushinda nafasi ya urais, lakini angalau kupata kura nyingi kunakiwezesha kupata ruzuku kubwa na wabunge lukuki wa viti maalumu.

“Kura nyingi za urais ni mtaji mzuri kwa chama cha siasa hasa cha upinzani. ACT Wazalendo wanachokifanya ni kuvuna watu mashuhuri ili wapate kura nyingi na hatimaye ruzuku kubwa na wabunge wengi wa viti maalumu,” amesema.

Amesema ili kupata kura nyingi inahitaji mwanasiasa anayekubalika na mwenye ushawishi na hapo ndipo vyama vya upinzani vinapotega mitego yake kuwapata kutoka katika vyama vingine.

“Kiuhalisia ukiangalia ACT Wazalendo ni chama kinachotaka kukua na kimekuwa kikifanya mikakati mbalimbali kukuwa, kumpata mwanasiasa nguli atakayesukuma ukuaji wake ni jambo la msingi.

“Lazima kitege mitego ya namna hiyo kuwapata wanasiasa wenye ushawishi na hatimaye wawezeshe chama husika kupata kura nyingi. Wanachama ndio mtaji wa vyama, kila chama kinafanya mbinu yake kuhakikisha kinapata wanachama,” ameeleza.