Na Mwandishi wetu, Karatu
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imeendelea kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa taasisi hiyo kupitia mafunzo ya kijeshi yanayotolewa katika kituo cha mafunzo ya kijeshi (Paramilitary) kilichopo Mbulumbulu, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishina wa Uhifadhi NCAA, Katika hafla ya kuhitimisha mafunzo kwa watumishi iliyofanyika kituoni hapo Leo Agusti 6, 2025, Kamishina Msaidizi Mwandamizi Victoria Shayo alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na NCAA kuhakikisha kwamba maafisa na askari wanapatiwa mafunzo ili kuongeza tija katika utendaji.
“Leo tunahitimisha mafunzo kwa Maafisa na Askari, tunaamini mafunzo mliyopata yamewawezesha kujua mbinu na maarifa yatakayoimarisha utendaji wenu katika kuwajengea ujasiri, ukakamavu, uweledi na utendaji kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria”alisema Victoria.
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo, mkuu wa mafunzo katika kituo hicho Kanali Fikiri Machibya amesema kwamba mafunzo hayo yalihusisha mafunzo ya mabadiliko ya kimuundo yanayohusisha kwata, ulengaji shabaha, masomo ya darasani pamoja na upigaji wa buruji (Bugle) kwa maafisa na askari.
“leo tumehitimisha kozi tukiwa na jumla ya wahitimu 17 Kati ya hao wahitimu 10 walikuwa ni wa mafunzo ya mabadiliko ya muundo kozi namba tatu (3) na 7 mafunzo ya upigaji wa buruji kozi namba moja (1)” Alisema Kanali Machibya.
Kanali Machibya, alisisitiza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha na kuwafanya maafisa na askari kuwa wazalendo na wachapa kazi kwa ajili ya ulinzi na Uhifadhi wa rasilimali za nchi pamoja na kuwaandaa askari kukamilisha itifaki mbalimbali za kijeshi katika utendaji kazi wao.