Tofauti kubwa ya watoto wa sasa ni uelewa wao wa haraka sana. Tunaweza kusema ni kizazi, kwamba cha kale hakikuwa na mambo mengi kama ilivyo kwa kizazi kipya. Ingemchukua muda mrefu kwa mtoto wa zamani kujifunza jambo, lakini hivi sasa watoto hutumia muda mfupi sana. Naweza kutumia maneno mengi kulielezea hili, labda tu niseme dunia inakwenda mbio sana zama hizi.
Watanzania wa leo si wale wa jana na juzi. Wanajifunza mengi kadiri teknolojia inavyokua kwa kasi nchini. Inawachukua watu muda mfupi sana kujua mambo wasiowahi kukutana nayo.
Na kwa vile dunia sasa ni ndogo sana kuliko mtaa, hatoki hata kwa hatua moja kuyatazama ya wenzake wa huko ng’ambo.
Akiwa kitandani kwake anaweza kulinganisha maisha yake na ya walimwengu chini ya sheria zinazofanana.
Si jambo rahisi kumficha Mtanzania wa leo jambo linalomhusu. Inapotokea hivyo, yeye huperuzi na kushiriki na wenzake wa nje na ndani. Kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa mashirika mengi ya kimataifa (hasa yanayosimamia haki), anagundua kuwa tofauti ipo kwenye kanuni ndogondogo tu, na si kwenye mambo ya msingi. Anapata majibu kuwa nchini kwake kuna shida. Inaonesha uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu. Ugumu wake unatokana na watendaji kutokubaliana na ukweli kuwa watanzania wa leo si wa jana.
Wanachukulia picha za miaka iliyopita kama rejea katika mchakato wa uchaguzi huu. Hawatazami mambo ya nyakati kutoka uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa.
Mtu yeyote aliye kwenye mchakato huu angepaswa kuongeza umakini. Wakati ule tuliona wanachama wa chama tawala wakiwazogoma viongozi wao mara tu walipoyaleta majina ya watia nia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ugomvi ulikuwa maradufu wakati na baada ya mchakato wa mchujo, wanachama wengi wakidai kuwa majina yaliyorudi si waliyoyapendeza. Wakatishia kutoshiriki kwenye zoezi la uchaguzi, au kushiriki katika njia hasi (kwa maana ya kuwasapoti wapinzani au kupiga kura ya chuki).
Hiki ndicho kilichotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mapema mwaka huu. Wafuasi wa chama tawala waliandamana kupinga matokeo ya uchaguzi mitaani mwao mara baada ya kutangaziwa ushindi wa chama chao.
Ni ishara tosha kuwa maendeleo ya mtaa yatakuwa finyu kwa kuzingatia uhusiano wa wananchi na viongozi wao. Hili halijapita, ila ni bomu linalosubiri muda wa kulipuka. Sasa tumeletewa mapya.
Kule wlayani Simanjiro katika Mkoa wa Arusha wanachama waaminifu wa Chama cha Mapinduzi wameomba warudishiwe majina yote 9 ili mchakato na uchujaji uanze upya.
Wamesema hivyo baada ya jopo la wachujaji wa majina ya wagombea ubunge kuwaletea majina wasiyoyafahamu. Hii inaonesha ni kwa jinsi gani wananchi wanachoshwa na figisu za vyama.
Lakini huko Songwe nako limetokea linaloshangaza zaidi. Wachakataji wa majina wameshangazwa na kile kinachoonekana kwenye orodha iliyopokelewa na wananchi. Matukio yote mawili yanaonesha ni kupokwa kwa mamlaka za wachakata majina, na kwamba kuna tume ingine yenye nguvu juu yao inayoamua kama “Politburo” ya Urusi.
Politburo ni kamati ya wakomunisti wachache, lakini yenye nguvu zaidi ya Kamati Kuu ya Chama. Malalamiko yote yafanyiwe kazi kabla kipyenga hakijapulizwa. Ieleweke kuwa makosa mengi ni vivuli vya mambo yanayovitangulia. Hivyo kama figisu zitaendelea kupanga foleni, kutakuwa na mnyororo mrefu wa matatizo.
Haya yatazalisha harakati na kaulimbiu nyingi zitakazotazamwa kwa jicho la uhaini; watu watakamatwa, na vyama vitasusia uchaguzi. Hili litavisukuma vyama kuamini usemi wa “Mdharau mwiba mguu huota tende.”
Ili ichaguzi uwe huru na wa haki, hatua zote kuanzia mwanzo hazina budi kuheshimiwa. Wapigakura wa leo wanatambua haki zao za kidemokrasia.
Hawabweteki na ahadi zisizotekelezeka na maneno matupu kutoka kwa wagombea wasiojitambua. Hata kama mgombea hana sura nzuri na maneno ya kumtoa nyoka pangoni, kitu cha msingi anachoweza kuwavutia nacho ni sera. Kwamba atatumia njia zipi kuwavusha kutoka kwenye korongo waliloshindwa wenzake. Na yamtoke mtimani, sio mdomoni. Yeyote atakayeahidi bila kutekeleza achukuliwe kuwa amewadanganya wananchi, na itafutwe namna ya kumdai. Haiwezekani kiongozi anatoa ahadi katika miongo miwili mizima, kila anaporudi anadai muda haukutosha.
Hivyo ni wajibu wa vyama vya siasa kusikiliza mahitaji ya wanachama wao. Viongozi juu katika vyama wasijilinganishe na miungu kwa kudhani wanayajua matatizo ya wadogo.
Wanaweza wakadhani kuwa wanayajua vema matatizo ya jimbo kuliko wakazi wa jimbo hilo, lakini ukweli unabaki kuwa “Siri ya mtungi aijuaye kata.”
Wanachama wana sababu zao za kumtaka fulani aongoze jimbo lao. Baadhi ya wananchi huvichukulia vyama kuwa sawa na mitandao ya simu.
Hivyo hesabu ya wanachama wao inaweza kuwadanganya kwa mauzo ya kadi, wakae wakijua wenye kadi za CCM ndio haohao wana kadi za ACT Wazalendo.
Wasije kushangaa siku nusu ya wanachama wao wakipiga kura kwa mgombea wa chama kingine. Huo ndio mfano wa kadi za simu.