ONGEZEKO LA WAKULIMA WA MKONGE DODOMA LAMKUNA DC NYANGASSA

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Fatma Nyangassa amefurahishwa na hamasa inayofanywa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), ambayo imechangia upatikanaji wa wakulima zaidi ya 15 wenye takribani ekari 240 za zao la Mkonge ndani ya muda mfupi.

Akizungumza wakati alipotembelea Banda la TSB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Uvuvi na mifugo yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma leo Jumatano Agosti 6, Mhe. Fatma pia alitaka kujua hali ya uzalishaji mkoani Dodoma, kitaifa na mkoa unaoongoza huku akitamani Dodoma hususani Wilaya ya Kondoa kuongoza kwa uzalishaji.  

Akitoa maelezo kwa Mhe. Fatma Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge wa TSB, Simon Kibasa amesema Mkoa Dodoma bado uzalishaji haujaanza kufanyika kwa sababu wakulima wengi Mkonge wao bado mdogo.

Amesema uzalishaji kwa sasa umefikia tani 61,215 kutoka tani 39,484 mwaka 2021 na mkoa unaoongoza kwa uzalishaji ni Tanga ambapo inazalisha takribani tani 34,000.

“Tunategemea uzalishaji kuongezeka kutokana na wakulima kuongezeka katika kipindi cha hivi karibuni ikiwamo Mkoa wa Dodoma ambao kwa sasa wakulima wengi bado hawajaanza kuvuna Mkonge wao kwani wameanza kulima hivi karibuni baada ya serikali na Bodi kufanya uhamasishaji ambapo watu wengi wameitikia. 

“Kwa Dodoma hadi sasa kuna ekari zaidi ya 240 na za wakulima waliotembelewa tu kuna wengine bado hawajatembelewa. Kupitia maonesho haya kuna wakulima watatu walikuja jana wakaomba kutembelewa ili wasajiliwe na bodi na sisi tutawatembelea hivi karibuni baada ya kumaliza maonesho haya,” amesema Kibasa