Dar es Salaam. Bei ya mafuta ya petroli imeshuka kwa mwezi wa nne mfululizo sababu zikitajwa ni kupungua kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia, kushuka gharama za ubadilishaji wa fedha za kigeni na za uagizaji wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 2.3 kwa mafuta ya petrol na zimeongezeka kwa asilimia 5.5 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa.
Pia, kwa Agosti 2025, gharama za kuagiza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 12.43 kwa petroli, asilimia 3.11 kwa dizeli na kuongezeka kwa asilimia 13.08 kwa mafuta ya taa.
Sasa watumiaji wa mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam kwa bei za rejareja watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,843 badala ya Sh2,947 iliyokuwapo Aprili mwaka huu, dizeli Sh2,777 badala ya Sh2,868 na mafuta ya taa Sh2,768 badala ya Sh3,053, mtawalia.
Katika Bandari ya Tanga hakuna mabadiliko na bei zimeongezeka kwa asilimia 6.12 kwa mafuta ya petroli na asilimia 60.82 kwa mafuta ya dizeli katika Bandari ya Mtwara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura Dk James Mwainyekule jana Jumanne, Agosti 5, 2025, pia wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 2.
Kwa wanunuaji wa rejareja kwa mafuta yanayopita Bandari ya Tanga watanunua petroli lita moja kwa Sh2, 904 kutoka Sh2,994 iliyokuwepo Aprili, dizeli Sh2,839 kutoka 2,914 na mafuta ya taa Sh2,829, mtawalia.
Kwa Bandari ya Mtwara, petroli sasa itanunuliwa Sh2,935 lita moja kwa badala ya Sh3,020 iliyokuwapo Aprili mwaka huu, dizeli imefikia Sh2,870 kutoka Sh2,940 na mafuta ya taa Sh2,861 kutoka Sh3,125, mtawalia.
Kufuatia hilo, Ewura imewataka wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja kuuza kwa bei kikomo zilizowekwa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakayekiuka agizo hilo.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa.
“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi, ili kushamirisha ushindani,” amesema.