SERIKALI YAENDELEA KUHAMASISHA KILIMO CHA KISASA KUPITIA MAONESHO YA NANENANE

Na Alex Sonna-DODMA

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, amesema maonesho ya wakulima- Nanenane yamekuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya kilimo nchini, akibainisha kuwa taasisi za umma na binafsi zimeonyesha jitihada kubwa katika kuboresha sekta hiyo kupitia teknolojia na ubunifu wa kisasa.

Akizungumza baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya maonesho hayo, Dkt. Serera amesema kuwa amejionea jinsi taasisi zinazoshiriki zimekuwa zikitumia vifaa na mbinu za maandalizi zinazolenga kuongeza tija, kupata mazao bora na bidhaa zinazokubalika kwenye soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi hizo ili kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha kuwa wakulima wanapata huduma bora, teknolojia mpya na mbolea zenye viwango vinavyowawezesha kuzalisha kwa ufanisi.

“Kila mmoja niliyemkuta hapa ana hamasa kubwa ya kuendeleza kilimo chetu. Wakulima wanazungumza kwa matumaini makubwa wakitamani kuona juhudi hizi zinaendelea zaidi. Hii ni dalili kuwa tupo kwenye mwelekeo sahihi wa kuleta mapinduzi ya kilimo,” amesema Dkt. Serera

Aidha, Dkt. Serera amesisitiza kuwa Serikali inatambua jukumu lake la kuhakikisha mazingira ya kilimo yanakuwa rafiki kwa wakulima kwa kushirikiana na wadau wote wanaojitahidi kuinua sekta hiyo.

Alibainisha kuwa hatua kubwa zimepigwa katika uzalishaji wa bidhaa za kilimo ambapo baadhi ya bidhaa ambazo hapo awali zilipatikana kutoka nje ya nchi sasa zinazalishwa ndani, jambo linaloashiria maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo.

“Leo hii tunazalisha bidhaa ambazo zamani tuliziona tu zikitoka nchi za wenzetu. Hii ni hatua kubwa inayoonesha kuwa Tanzania inazidi kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula barani Afrika kutokana na upatikanaji wa mbolea bora na teknolojia zinazoongeza tija,” ameongeza

Dkt. Serera ametoa wito kwa Watanzania wote kutumia fursa ya maonesho ya Nanenane kujifunza mbinu za kisasa za kilimo na kuzitumia kuongeza uzalishaji, akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha taifa linakuwa kinara wa kilimo na chakula barani Afrika na duniani.