Shule 60 zajengwa kwa miaka mitano Zanzibar

Unguja. Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakirejesha nyuma elimu visiwani hapa ni uchakavu na uchache wa vyumba vya madarasa na mfumo wa elimu ngazi ya msingi na sekondari, uliofanya wanafunzi kuingia darasani kwa mikondo mitatu – asubuhi, mchana na jioni.

Hata hivyo, hali hiyo ya kusoma kwa wastani wa saa tatu kwa siku, imepungua baada ya Serikali kujenga shule mpya zaidi ya 60, zikiwemo za ghorofa 23.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2020, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alitangaza sekta ya elimu kuwa kipaumbele cha kwanza, ili kupindua meza ya matokeo na kuongeza ufaulu wa wanafunzi, vitu ambavyo vimeanza kuonekana.

Kipindi cha nyuma Zanzibar ilikuwa inavuta mkia kwa matokeo ya elimu ya msingi na sekondari, hatua iliyotajwa kutokana na mazingira duni ya ujifunzaji na ufundishaji yaliyokuwepo, hali ambayo imeanza kubadilika.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Abdalla Khamis Juma amesema kwa sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu kwa kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni pamoja na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mageuzi ya sekta ya elimu, Agosti 5, 2025 Khamis amesema Zanzibar ilikuwa na changamoto kubwa vya vyumba vya madarasa, wanafunzi wanaingia mikondo miwili na baadhi ya shule wanaingia mikondo mitatu kwa siku, mmoja asubuhi, mwingine mchana na wa jioni, lakini kwa sasa zaidi ya asilimia 70 wanaingia mkondo mmoja.

“Ukitaka kupima ubora wa elimu ni ufaulu, ndani ya kipindi hiki kiwango cha ufaulu Zanzibar hakijawahi kutokea, matokeo kidato cha sita ufaulu umefikia asilimia 96.8, tunaweza kusema wote wana uwezo wa kuingia vyuo vikuu na vya kati na hiyo asilimia iliyobaki ni kwa sababu ya kuumwa au changamoto zozote za kibinadamu,” amesema.

Amesema, michepuo ya darasa la saba imeongezeka kutoka asilimia 5.5 hadi kufikia asilimia 15 na ndio maana zimejengwa dahalia (mabweni) nyingi zaidi ya 14 katika shule mbalimbali ili kuwasaidia wanafunzi kufaulu.

“Ufaulu unaonekana kwa sababu Dk Mwinyi amefanya miundombinu mizuri, kaajiri walimu na ameweka mazingira rafiki ya kujinzia pamoja na kuchapa vitabu vya kutosha zaidi ya milioni 3.4. Ameimarisha maabara za sayansi na kujenga vituo vya ubunifu, haya ni miongoni mwa mambo yanayochagiza kuongeza ubora na ufaulu Zanzibar,” amesema.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, uandikishaji wa shule za maandalizi umeongezeka kutoka asilimia 81.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 84.4 mwaka 2024, yaani kwa kila watoto 10 ni mmoja ambaye hayupo shuleni.

Pia, katika shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, uandikishaji umeongezeka kutoka asilimia 83.9 hadi asilimia 103.

“Hii haijatokea kwa bahati mbaya, ni kwa sababu kuna mazingira mazuri, uhamasishaji, maandalizi na madarasa ya kuwapokea watoto na walimu wa kuwafundisha,” amesema.

Kwa kipindi cha miaka minne, wizara imejenga madarasa 4,810, ikijumuisha shule za ghorofa 36 ambazo zimejengwa katika wilaya zote – mjini na vijijini – hatua ambayo inatajwa kuondoa usumbufu wa kuwachangisha wazazi fedha kwa ajili ya kujenga shule.

Amesema kwenye shule zote zilizojengwa, zimewekewa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ambapo zaidi ya kompyuta 3,000 mpya zimewekwa katika shule hizo.

Pamoja na hayo, kwa sasa zipo baadhi ya shule ambazo zinatumia elimu kwa masafa kutokana na uwekaji huo, unaowawezesha wanafunzi katika shule tofauti kufundishwa kwa wakati mmoja kupitia njia ya masafa.

“Katika nchi za Afrika, ukiondoa Afrika Kusini, Zanzibar itakuwa inaongoza katika vifaa vya Tehama kwa shule za sekondari. Kuna tablet sensor kwenye shule, walimu wanatumia kwa ajili ya kufundishia, haijawahi kutokea,” amesema.

Kwa mujibu wa wizara, walimu 5,265 wameajiriwa katika kipindi cha miaka mitano, ambapo kabla ya mwaka 2020 Pemba ilikuwa na walimu wa kujitolea 1,500. Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wameajiriwa 650 kwa Pemba pekee.

Mishahara ya walimu asilimia 70 hadi 90 imeboreshwa na walimu hulipwa posho ya kila mwezi ya Sh50,000 kwa ajili ya nauli.

Katika kuendelea kuwawekea walimu mazingira mazuri na kuepuka kutembea masafa marefu, Serikali imeanza kujenga nyumba za walimu vijijini ili walimu wakae maeneo ya shule na kupata muda wa kutosha kufundisha, huku ikitoa posho ya Sh50,000 kila mwezi kwa ajili ya nauli.

Wakati Rais Mwinyi anaingia madarakani mwaka 2020, bajeti ya elimu ilikuwa Sh265 bilioni. Hadi kufikia bajeti ya mwaka 2025/26, imefikia Sh860 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 212.

Licha ya mafanikio hayo, bado kuna uhitaji wa miundombinu kwa sababu Zanzibar inakua kwa kasi – ukuaji wa watu uko asilimia 3.7 kwa mwaka,  kiwango ambacho kinatajwa kuwa kikubwa.

Hivyo, pasipokuwa na maandalizi ya kuongeza miundombinu, kunaweza kusababisha changamoto kubwa zaidi siku za usoni.

Katibu Mkuu amesema wanaendelea na mipango ya kujenga shule nyingine za ghorofa 23 za msingi na sekondari, ambazo zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.

Katika Tehama, Serikali inaendelea na maandalizi ya kujenga shule 100 na kuziunganisha na mkongo wa Taifa. Wapo katika hatua za mwisho kumalizia hilo, na tayari wamefanya mazungumzo na kampuni za simu kwa ajili ya kuunganisha intaneti katika shule hizo.

Baadhi ya walimu na wanafunzi wanaosoma shule zenye mifumo ya kisasa ya ufundishaji wamesema mifumo hiyo imerahisisha ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza ufaulu.

Mohamed Ali Mohamed, mmoja wa walimu wanaosimamia chumba maalumu cha Tehama ‘smart room’ katika Sekondari ya Mtakuja, amesema chumba hicho husaidia walimu kumaliza mada na kurahisisha ufundishaji kwa kutumia hata picha mjongeo.

“Hakuna haja ya kutoa kopi nyingi kisha kuwasambazia wanafunzi, unakuwa na moja na kuiweka kwenye mfumo kisha mnaendelea na somo. Imesaidia kumaliza mada za masomo kwa wakati. Tunaendelea kuitumia vyema ili kuongeza ufaulu Zanzibar,” amesema.

Naye mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa sekondari hiyo, Suleisa Iddi Ali amesema mfumo huo unawasaidia kuona kwa ushahidi wanachojifunza, tofauti na kutumia makaratasi, hivyo kuongeza uelewa.

“Kinachotakiwa ni sisi wanafunzi kuongeza kasi. Tunashukuru Serikali kwa kutujengea mazingira mazuri ya kujifunza. Tunachoahidi ni kuleta madaraja ya kwanza mengi zaidi,” amesema.

Mwanafunzi mwingine, Sabrina Mahsin amesema katika ufundishaji wa kawaida walikuwa wanapata ugumu kuelewa, lakini tangu kuanza kwa mfumo huo katika chumba maalumu wanaelewa haraka na kutumia muda mfupi.

“Mwanzoni ilikuwa ngumu kuelewa lakini tangu kufika katika chumba hiki maalumu tunajifunza teknolojia na maneno mapya ya Kiingereza, hata mwalimu hatumii muda mrefu kuandaa notisi.”

Mwanafunzi mwingine, Mohamed Mwinyi Habib, ameongeza: “Kwenye mfumo kinawekwa kila kitu. Tunajifunza kutumia teknolojia na kuna maneno mapya tunayapata. Hata mwalimu hatumii muda mrefu kuandaa notisi.”

Sh35 bilioni elimu ya juu

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Zanzibar, Umrat Suleiman Mohamed amesema Serikali ya Awamu ya Nane imeongeza bajeti ya mikopo kutoka Sh25 bilioni mwaka 2023/24 hadi kufikia Sh35 bilioni mwaka 2024/25.

Kiwango hicho cha fedha kitaweza kuwahudumia wanafunzi takribani 4,877.

“Kwa hiyo hili ni jambo kubwa sana maana wanafunzi wengi watapatiwa mikopo na kwenda vyuo vikuu,” amesema.

Amesema katika kipindi hiki Serikali pia imeanzisha dirisha maalumu kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma stashahada.

“Wale wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na hawana uwezo wa kuendelea na kidato cha sita, wao wana dirisha maalumu la kuomba mikopo kwa ajili ya kuendelea na masomo yao ya diploma. Mpaka sasa wanafunzi 3,336 tayari wamepewa,” amesema.