Siku zangu 100 za kwanza Mkurugenzi Mtendaji wa MCL

Ilikuwa jioni ya Jumatatu, Aprili 28, 2025 katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Ukumbi ulijaa viongozi wa juu wa Nation Media Group na Mwananchi Communications Limited (MCL). Ilikuwa ni siku ya kihistoria, matarajio na imani kubwa.

Mbele yangu waliketi Mwenyekiti wa NMG Wilfred Kiboro; Mwenyekiti wa Bodi ya MCL David Nchimbi; wajumbe wote wa Bodi na menejimenti yote. Haikuwa tu hafla rasmi ya makabidhiano ilikuwa ni wakati wa urithi wa kihistoria. Nilihisi kunyenyekea na kutambua kwa undani kwamba dhamana hii ni kubwa zaidi kuliko mimi binafsi.

Asubuhi iliyofuata, Aprili 29, nilisimama mbele ya wafanyakazi mahiri wa MCL.

Nilitambulishwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi yetu, huku taarifa za uteuzi wangu zikiwa tayari zimeenea kwa umma.

Simu yangu iliwaka simu, ujumbe mfupi na taarifa kwenye mitandao ya kijamii. Pongezi zilimiminika kutoka kwa marafiki, wafanyakazi wenzangu, wadau wa sekta yetu na hata watu nisiofahamu. Nilihisi kama mkataba wa kimya kimya ulikuwa umetiwa saini na kila Mtanzania anayeamini katika uandishi wa habari wa ukweli na kila mfanyakazi anayehakikisha chumba chetu cha habari kinabaki hai.

Kuaminiwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza mwanamke wa MCL kampuni inayochapisha Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti, pamoja na majukwaa ya kidijitali ni jukumu ninalolibeba kwa fahari na dhamira thabiti. Hili linaonesha azma ya NMG katika kukuza utofauti, ubunifu na uongozi wa kuthubutu.

Brené Brown aliwahi kusema, “Uwazi ni wema. Kutokuwa wazi ni ukatili.” Tangu siku ya kwanza, nimejikita kuongoza kwa uwazi—kuhusu tulipo na tunakotakiwa kuelekea.

Nikitafakari siku hizi mia moja, neno moja linajirudia akilini mwangu: shukrani. Ninamshukuru Mungu kwa mapokezi ya upendo kutoka kwa wafanyakazi wetu, miongozo ya busara kutoka kwa bodi yetu na ukarimu wa wadau wetu—kuanzia wizara na Bunge hadi washirika wa kibiashara na asasi za kiraia—waliotufungulia milango yao, kushiriki nasi mawazo yao na kuunga mkono maono yetu.

Moja ya nyakati zenye uzito mkubwa ilikuwa kusimama bega kwa bega na wakurugenzi wote wanne waliowahi kuongoza MCL Tido Mhando, Francis Nanai, Bakari Machumu na mimi mwenyewe. Picha ile ilibeba maana ya mwendelezo, tafakuri na ahadi ya kesho. Kama Jim Collins anavyotukumbusha, “Ukuu si matokeo ya mazingira. Ukuu, kwa hakika, ni matokeo ya uamuzi wa makusudi.” Na kwangu mimi, uamuzi huo unaongozwa na imani imani kwamba uongozi si wito tu, bali ni dhamana aliyoikabidhi Mungu kwa mikono ya mwanadamu.

Siku chache tu baada ya kuanza rasmi jukumu hili, nilishuhudia upekee wa timu yetu pale Mwananchi ilipotangazwa kuwa Chapisho la Karatasi Linaloaminika na Kupatikana kwa Urahisi Zaidi katika Tuzo za Samia Kalamu 2025.

Julius Maricha alitunukiwa kuwa Mwandishi Bora katika Ripoti za Nishati Safi ya Kupikia. Haya hayakuwa mafanikio ya kawaida—yalikuwa uthibitisho wa dhamira yetu ya kusimamia uandishi wa habari wenye mguso wa kweli. Yalitukumbusha kwamba ukweli bado ni jambo la msingi. Uadilifu bado ni nguzo kuu.

Tangu wakati huo, tumeendelea kushirikiana kwa ukaribu na viongozi wa serikali, wabunge, wasimamizi wa sekta, wawekezaji wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo. Maoni yao yamekuwa yakitupatia dira mpya. Wametukumbusha kwamba MCL si nyumba ya habari pekee ni taasisi ya kitaifa yenye uwezo wa kuhabarisha, kushawishi na kuchochea mabadiliko.

Tunapoadhimisha siku 100, tunajenga msingi wa siku 1,000 zijazo. Dhamira yetu iko wazi: Kufikiria Upya Mustakabali wa Vyombo vya Habari Tanzania. Hii inamaanisha kuharakisha mabadiliko ya kidijitali, kukuza simulizi zenye uwezo wa kuhamasisha na kuunda majukwaa jumuishi ambapo kila sauti ina nafasi yake—iwe kwa Kiswahili au Kiingereza, iwe kwenye karatasi au mtandaoni.

Simon Sinek anaandika, “Viongozi hawawajibiki kwa matokeo. Viongozi wanawajibika kwa watu wanaowajibika kwa matokeo.” Siwezi kukubaliana zaidi. Vipaji vilivyopo ndani ya MCL vinanipa matumaini makubwa. Pamoja, tunabuni upya mifumo yetu, tunajenga imani na kulea ubunifu mpya.

Kwa wasomaji wetu, washirika wetu na jamii zetu asanteni. Imani yenu ndiyo inayochochea fikra zetu bunifu. Na kwa familia nzima ya MCL: Ninyi ndio moyo wa taasisi hii.

Hivyo basi, tupo hapa. Siku 100 ndani ya safari hii. Huu ni mwanzo tu.

Natembea safari hii nikiwa na imani thabiti na maombi ya kimya kimya, nikiamini kwamba njia iliyo mbele haitachongwa tu na maono na juhudi, bali pia kwa neema.

Sasa, ni zamu yako. Ikiwa ungekuwa na dakika moja kuongea namiungeuliza swali gani, au ungenishauri nini? Tushirikishe mawazo yako. Safari hii ni yetu ya pamoja.