Baada ya kuanza vyema Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo inatupa karata muhimu katika kundi B la mashindano hayo wakati itakapokabiliana na Mauritania katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 usiku.
Kabla ya mechi hiyo, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika Kati zitatangulia kwa kukabiliana katika mechi ya kwanza itakayochezwa uwanjani hapo kuanzia saa 11:00 jioni.
Matokeo ya mchezo wa kwanza na msimamo wa kundi B ulivyo ni mambo mawili yanayoilazimisha Taifa Stars kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ya leo ili ifikishe pointi sita ambazo zitaifanya izidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa kundi B.
Na ikiwa itafanikiwa kupata ushindi leo, Taifa Stars itahitaji ushindi angalau katika mechi moja tu au matokeo ya sare katika mechi mbili zitakazobaki dhidi ya Madagascar na Jamhuri ya Afrika ya Kati ili ijihakikishie kutinga hatua ya robo fainali.
Taifa Stars dhidi ya Mauritania ‘Les Mourabitounes’ ni mchezo unaokutanisha timu mbili ambazo zinafanana kwa baadhi ya mbinu kiuchezaji lakini pia zina utofauti kwa namna nyingine.
Ni timu mbili ambazo zinapendelea zaidi kutawala mchezo hasa katika safu ya kiungo lakini wakati Taifa Stars ikiwa bora zaidi katika kujilinda pindi wapinzani wanapokuwa na mpira huku Mauritania ikiwa ni timu inayopenda kushambulia kwa muda mrefu wa mchezo.

Wenyeji Taifa Stars wanaingia katika mchezo wa leo wakimtegemea zaidi Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye alikuwa mchezaji bora wa mechi ya kwanza kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchezesha timu na kuvunja mistari ya ulinzi ya timu pinzani.
Nyota mwingine wa Taifa Stars ambaye Mauritania inapaswa kumtazama zaidi leo ni kiungo Mudathir Yahya ambaye ni mzuri katika kuilinda timu na kujenga mashambulizi na pia hata kufunga mabao pindi anapolisogelea lango la timu pinzani.
Kiungo wa Mauritania, El Hacen El Id ni mchezaji ambaye Taifa Stars inapaswa kumpa uangalizi wa ziada ili asilete madhara kwani ndiye nyota hatari zaidi katika kikosi chao.
Mbali na uzoefu mkubwa wa soka la kimataifa ambao El Id anao akiwa amewahi kucheza soka la kulipwa Hispania katika klabu za Levante na Lugo, kiungo huyo anasifika kwa ufundi wa hali ya juu uwanjani hasa katika kumiliki na kutembea na mpira lakini pia utulivu pindi awapo na mpira.

Matokeo ya timu hizo katika mechi sita zilizopita ambazo kila moja imecheza, yanaweza kuongeza hali ya kujiamini ya Taifa Stars katika mechi ya leo kwani imeonyesha uimara katika idara muhimu za ulinzi na ushambuliaji kulinganisha na Mauritania lakini hata kwa matokeo yaliyopatikana.
Katika mechi hizo sita zilizopita, Mauritania imepata ushindi mara moja tu, ikitoka sare nne na kupoteza mechi moja.
Mauritania katika mechi hizo sita zilizopita hivi karibuni, imefunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Taifa Stars katika mechi sita zilizopita, imeibuka na ushindi mara nne, kutoka sare mchezo mmoja na imepoteza mechi moja. Mabao ambayo Taifa Stars imefunga katika mechi zake sita zilizopita ni saba na yenyewe imefungwa mabao matatu tu.
Ikumbukwe timu hizo hii ni mara ya kwanza zinakutana katika mechi ya kimashindano hivyo timu itakayoibuka na ushindi, itaanza kuweka alama ya ubabe dhidi ya nyingine.

Bao lolote ambalo Taifa Stars italifunga katika mechi ya leo, litaihakikishia kitita cha Sh10 milioni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Lakini kuna zawad kubwa ya Sh1 bilioni kutoka kwa Rais Samia ikiwa Taifa Stars itafanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Akizungumzia mchezo huo, nahodha wa Taifa Stars, Dickson Job alisema wamejipanga kucheza kwa ajili ya nchi na kwamba wanachotaka ni Watanzania kuwapa sapoti ili watimize jambo hilo.
Job alisema kikosi kipo fiti na tayari kwa ajili ya mchezo.