Mbeya. Kufuatia Wakulima Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya kuchangamkia fursa ya matumizi ya mbegu bora ya viazi mviringo maarufu kama ‘Obama’, Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani ya zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa mwaka.
Hatua hiyo imetajwa kufanikisha kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 513,313, hadi tani 614,278 kwa kipindi cha mwaka 2021/2025 .
Ofisa Kilimo Halmashauri ya Rungwe, Majaliwa Mwalembe ameliambia Mwananchi Digital leo Agosti 6,2025 kwenye banda la Maonyesho ya Wakulima Nanenane katika Viwanja vya John Mwakangale mkoani hapa.
Maonyesho hayo yanahusisha taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wa sekta ya kilimo kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususani Njombe, Iringa, Rukwa, Katavi, Songwe na Mkoa mwenyeji wa Mbeya.
Amesema Wilaya ya Rungwe wananchi wengi wamegeukia shughuli za kilimo cha mazao ya chakula na biashara kama ndizi, parachichi, huku viazi mviringo vikipewa kipaumbele.
“Asilimia 75 ya mapato ya halmashauri hutokana na kilimo,lakini tutokana na mchango mkubwa tumeweka mazingira mazuri ya kuwasajili kwenye vikundi na kupewa elimu ya kilimo bora, upimaji wa afya ya udongo sambamba na upatikanaji wa mbolea za ruzuku na mikopo asilimia 10,”amesema.
Katika hatua nyingine amesema ili kufikia malengo ni Serikali ya kuongeza tija kuzalisha mazao ya kimkakati wamejipanga kukabiliana na changamoto za masoko kwa kudhibiti madalali na vifungashio vya mifuko la lumbesa.
Ametaja moja ya sifa iliyo wasukuma wakulima kutumia mbegu bora ya viazi mviringo aina ya Obama ni kutokana na kufanya vizuri katika uzalishaji ambapo kwa hekari moja wanavuna gunia 80 mpaka 100.
“Kiazi Obama kinafanya vizuri sana katika uzalishaji endapo mkulima akazingatia kanuni bora kuweka mbolea kwa wakati na kupima afya ya udongo kabla ya kuanza uzalishaji, lakini pia kinafanya vizuri sokoni,” amesema.
Amesema ili kuimarisha masoko na kuongeza tija ya uzalishaji wameweka mikakati kuhakikisha wakulima wanapata mikopo asilimia 10 kwa kuzingatia kilimo kinahitaji mtaji.
Mwalembe amesema wana wahimiza maofisa kilimo kuwafikia wakulima kutoa elimu ya uzalishaji ulio na tija kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi ili kufikia malengo ya Serikali kuwa na ziada ya chakula.
Amesema kwa msimu wa mwaka jana bei ya viazi mviringo ilikuwa juu kwa Sh 37,000 mpaka Sh50,000 kwa ujazo wa kilo 100 hadi 105 ,lakini msimu huu imeporomoka hadi kufikia Sh25,000 mpaka Sh30,000.
Ametaja sababu ya kuporomoka kwa soko ni kutokana na kujiendesha lenyewe hususani kuingiliwa na wimbi la madalali wanaotumia vifungashio vya mfumo wa lumbesa ambayo imepigwa marufuku na Serikali.
Kwa upande wake Ofisa Biashara Wilaya ya Rungwe, Renatus Nicolaus amesema masoko ya mazao yanayozalishwa masoko yake makubwa yako Jijini Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma na mikoa mingine inachukua, lakini sio kwa kiwango kikubwa.
“Ardhi ya Rungwe ni nzuri hata ukiangalia mazao yak e hususani viazi ingawa kuna shughuli za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ambayo pia yana masoko hususani kuanzishwa kwa viwanda vidogo vya kuchakata na kuongeza thamani,”amesema.
Naye Mkulima wa viazi katika Kata ya Simambwe Wilaya ya Mbeya, Sikujua Joram amesema kilio hao kikubwa ni madalali na ununuzi wa mifuko la kumbesa ambayo inawanyonya.
“Miaka nenda miaka rudi kilio chetu ni madalali na kumbesa tunaona jitihada za serikali, lakini kundi hilo ni kubwa tunaomba tutafutiwe soko la uhakika ili tuweze kunufaika na kilimo kwani tunatumia nguvu kubwa kuzalisha wengine wananufaika,”amesema.