Vedastus Masinde sasa atajwa Msimbazi

BAADA ya mabosi wa JKT Tanzania kuweka ngumu juu ya upatikanaji wa beki wa kati aliyekuwa akiwindwa na Simba, Wilson Nangu inadaiwa mabosi wa Msimbazi wameanza kumpigia hesabu na kufanya mazungumzo na beki wa kati wa TMA Stars, Vedastus Masinde.

Simba inapambana kunasa saini ya Nangu anayetajwa kuwa na mkataba na maafande hadi 2028, huku ikielezwa klabu yake imegoma kumuachia na kuwalazimisha mabosi wa Msimbazi kufanya mazungumzo yaliyofikia pazuri dhidi ya Masinde ambaye yupo katika kikosi cha Taifa Stars kinachoshiriki michuano ya CHAN.

Chanzo cha kuaminika kutoka Simba na rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa timu hiyo imeonyesha nia ya kumhitaji Masinde ambaye hana mkataba na TMA baada ya aliokuwa nao kumalizika Ligi ya Championship ilipomalizika.

“Ni kweli Simba wamefanya mazungumzo na Masinde juu ya kuhitaji huduma yake. Hadi sasa haijafahamika wamefikia wapi, lakini nia hiyo wameionyesha na walituma wawakilishi wao mchezaji huyo akiwa ndani ya kambi ya Stars,” alisema rafiki wa mchezaji huyo.

Chanzo kutoka Simba kilisema juhudi za upatikanaji wa mchezaji huyo zinaendelea na wanaamini endapo watamkosa Nangu, basi huyo atakuwa ni mchezaji sahihi kuongeza namba eneo la ulinzi.

“Masinde ni mchezaji mzuri na anaweza kutuofa vitu vingi endapo tutafanikiwa kumsajili, kwani anaweza kucheza ukuta wote wa nyuma – beki namba mbili, tatu, nne na tano. Lakini ni kijana mdogo ambaye anaweza kujengwa sasa hadi hapo atakapofika wakati wa kuaminiwa na kupewa namba ya kudumu kikosini,” ,” kilisema chanzo kutoka Simba.

Mwanaspoti lilimtafuta Masinde ili kuzungumzia ofa hiyo ambapo alisema hana mkataba na timu yoyote isipokuwa amepokea ofa kutoka timu nyingi na kwamba hawezi kuweka wazi hadi hapo mambo yatakapokamilika.

“Mimi ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na TMA Stars. Kuhusu ofa ni nyingi na siwezi kutaja timu kwa sababu bado hatujafikia makubaliano rasmi. Naamini mambo yakiwa tayari kila mmoja atafahamu nitacheza wapi,” alisema beki huyo ambaye amecheza sambamba na Nangu kabla ya kutimkia JKT Tanzania.