Vurugu zaibuka mkutano wa CUF, wajumbe wazichapa

Dar es Salaam. Ndani mtiti nje mtiti. Ndivyo tunavyoweza kusema, baada ya ukumbi wa Shabani Mloo wa Chama cha Wananchi (CUF), uliotakiwa kutumiwa na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho ili kupitisha ilani na kuteua majina ya wagombea urais wa Tanzania na Zanzibar, kugeuka uwanja wa ngumi.

Mtiti huo uliodumu kwa takribani dakika 10 na sekunde kadhaa leo Jumatano, Agosti 6, 2025 ambapo ilishuhudiwa baadhi ya wajumbe wakisambaziana ngumi huku baadhi wakilia kwa nguvu na wengine wakihangaika kutaka kujinusuru kutoka lakini ilikuwa ngumu kwao kwa sababu milango na madirisha ilikuwa imefungwa na waliosababisha tafrani hiyo walikuwa wamejipanga sehemu za kutokea.

Wakati wa vurugu hizo hapakuwa na mtu wa kutia mguu wa kutuliza zaidi ya kila mtu kuhangaika apate upenyo wa kutokea.

Purukushani hizo zilianza muda mfupi baada ya viongozi waandamizi kuwasili akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa  Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Husna Abdallah, Naibu Katibu Mkuu-Bara, Magdalena Sakaya kutinga ndani ya ukumbi huo.

Chanzo cha vurugu hiyo, kinatajwa ni kitendo cha kuingizwa ukumbini wajumbe ambao si halali, jambo lililosababisha baadhi ya wajumbe kuanzisha vurugu ili watoke ndani ya ukumbi huo.

Wakati vurugu hizo zinaendelea na kelele zinakuwa nyingi ndipo baadhi ya walinzi waliokuwa ndani ya ofisi ya chama hicho kwenda kufungua mlango na madirisha ndipo Profesa Lipumba na viongozi wenzake walipata upenyo wa kutoka na kuwaacha wajumbe wakichapana ngumi.

Endelea kufuatilia Mwananchi