Dar es Salaam. Katika kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi unamfikia kila mtu, Airtel Money kwa kushirikiana na Benki ya I&M wamezindua mpango unaolenga wanawake wajasiriamali wenye lengo la kuwawezesha wanawake nchini.
Mpango huo unawapa elimu ya kifedha na nyenzo muhimu za kukuza biashara zao hivyo kuweza kuboresha maisha yao.
Mpango huo ni sehemu muhimu ya mkakati wa uendelevu wa Benki ya I&M Tanzania unaojikita kwenye nguzo tatu kuu ambazo ni ujumuishaji wa kifedha, elimu ya kifedha, na uwajibikaji wa mazingira, ukiendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan SDG 5 (Usawa wa Kijinsia) na SDG 13 (Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi).
Kupitia huduma ya Kamilisha, iliyoundwa kwa pamoja kati ya Airtel Money na Benki ya I&M, huwapa wateja uwezo wa kupata mikopo midogomidogo kupitia simu zao ili kukamilisha miamala muhimu kama kutuma pesa au kulipa bili, hata wanapokosa salio kwenye akaunti zao za Airtel Money.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jana Jumanne, Agosti 5, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto amesema; “kuna matumizi makubwa ya Airtel Money na ndio tunalenga kujenga uwezo ili kupunguza pengo la matumizi, tunataka kuhakikisha kuwa wateja wetu, hasa wanawake, wana ujasiri na ujuzi wa kutumia huduma za kifedha kidijitali kwa ufanisi.”
“Kupitia mpango huu, tunasaidia kupunguza pengo la elimu ya kifedha na kusaidia uimara wa kifedha wa muda mrefu, kwa kuwa chini ya asilimia 30 ya wanawake Tanzania wanamiliki simu janja, tumejumuisha mafunzo ya moja kwa moja ya matumizi ya programu za kifedha ili kuwajengea ujasiri watumiaji wapya,” aliongeza Kamoto.
Katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kama sehemu ya uzinduzi wa mpango huu, zaidi ya wanawake 50 walikusanyika kwa mafunzo shirikishi juu ya usimamizi wa fedha, matumizi ya fedha kidijitali, na mbinu endelevu za biashara, lengo ikiwa siyo tu kutoa ujuzi wa kiufundi, bali pia kuunganisha uwezeshaji wa kiuchumi na maendeleo jumuishi yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, Zahid Mustafa amesema, “Hii ni sehemu ya dhima yetu ya kufanya benki kuwa jukwaa la kuleta mabadiliko, tunajivunia kuongoza mpango huu kwa ushirikiano na Airtel Tanzania.
“Leo tukianza safari hii kwa kutoa mafunzo ya siku moja ya elimu ya kifedha kwa wanawake 60 hapa Dar es Salaam, kwa udhamini kamili, mtaala wa mafunzo haya umetayarishwa kwa kushirikiana na Grant Thornton na utaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia mrejesho kutoka kwa washiriki,” amesema.
Mpango huo unalenga kuziba pengo la wanawake kutofikiwa na mfumo wa huduma za kifedha kwa kuwapa ujuzi wa vitendo na ujasiri zaidi kushiriki katika mfumo huo.
“Tangu kuanzishwa kwake, huduma ya Kamilisha imekwisha toa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh392 bilioni, ambapo asilimia 46 ya mikopo hiyo imekwenda kwa wanawake. Hadi sasa, zaidi ya Watanzania milioni tano wameingia kwenye mfumo rasmi wa kifedha kupitia huduma hii,” ameongeza.
Kama sehemu ya mpango huu, Benki ya I&M imeahidi kupanda mti mmoja kwa kila wanawake 100 watakaokopeshwa, na inalenga kupanda miti 8,000 kwa mwaka.
Jitihada hizi za kimazingira zinatekelezwa kwa kushirikiana na taasisi ya Africa Transformation Initiative (ATI), ambayo itasimamia upatikanaji, upandaji, na ufuatiliaji wa miti hiyo nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.