Wizara Kilimo yakubali kazi e-GA

Dodoma. Serikali imetaja Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuwa imepeleka mapinduzi makubwa ya kidijitali katika sekta ya kilimo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Agosti 6,2025 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Athumani Kilundumya alipotembelea banda la e-GA katika Maonyesho ya Kilimo, Wavuvi na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Kilundumya amesema Wizara ya Kilimo imeshuhudia jitihada zinazofanywa na e-GA katika ujenzi wa mifumo ya Tehama kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya sekta ya kilimo ili kuimarisha sekta hiyo.

“Natambua jitihada za e-GA katika ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa mbolea kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), ambao unawezesha usajili na utoaji wa leseni kwa wauzaji na wasambazaji wa bidhaa hiyo, utambuzi wa maghala ya utunzaji na udhibiti wa soko.

Amesema kupitia mfumo huo Serikali inaweza kudhibiti soko la mbolea na kuhakikisha inauzwa kwa bei rafiki kutokana na ruzuku ya Serikali.

Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga amesema wanaendelea kufanyia kazi changamoto zote zinazojitokeza ili kuhakikisha mifumo ya Serikali inafikia kwenye malengo tarajiwa.

Kaswaga amesema e-GA itaendeleza ushirikiano na sekta ya kilimo ili kuimarisha Tehama katika taasisi hiyo ambayo inakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya mifumo ya kiutendaji nchini.