Yanga ni mwendo wa dozi

UNAJUA maisha yanayoendelea pale  Jangwani kwa sasa? Kama huelewa, basi taarifa ikufikie kwamba mambo ni moto kwelikweli huku utambulisho wa mastaa wapya ukiendelea.

Nyuma ya utambulisho huo kuna sapraizi moja matata inapikwa na kinachoelezwa ni kwamba mastaa wa timu hiyo kwa sasa wanaifanyia kazi ya maana tu.

Kwa mashabiki wa Yanga watakuwa wamemisi kuiona timu hiyo tangu ilipocheza mechi ya mwisho dhidi ya Simba msimu uliopita, lakini unawaambiwa kinachoendelea ni balaa kwani kocha mpya Romain Folz anawanoa mastaa kwa dozi ya kiwango cha juu.

Iko hivi. Tangu Yanga ianze mazoezi Agosti Mosi, wiki hii dozi ya mazoezi imeongezeka, huku mastaa hao wakipiga tizi mara mbili kwa siku.

Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti kuwa ratiba ya Folz ni kwamba asubuhi timu hiyo inaanzia gym ikijifua huko kwa mazoezi tofauti ikiwemo kunyanyua vitu vizito na  kuimarisha misuli ya mwili.

“Katika ratiba hiyo Folz hapo anageuka kuwa msimamizi tu kazi kubwa inakuwa kwa kocha wa mazoezi ya viungo Tshephang Mokaila na uwepo wake ni maalumu kwa wale watakaolegea mazoezini.

“Mokaila amekuwa na mazoezi makali yaliyowafanya wachezaji wa Yanga kutoona tofauti kati yake na Lagrouni raia wa Morocco.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga wanafichua kwamba, kocha huyo anatangulia kufanya mazoezi hayo hayo ili kuwataka wachezaji kufanya kama yeye.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, ratiba hiyo hutumia masaa mawili, ambapo baada ya hapo kila mchezaji husisitizwa kwenda kupumzika na kunywa maji mengi.

Mokaila ndiye kocha mpya wa viungo wa Yanga aliyechukua nafasi ya Taibi Lagrouni, ambaye ameondoka ndani ya timu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika.

Ratiba hiyo inaendelea tena jioni ambapo sasa wanarudi uwanjani KMC Complex na wakiwa huko Mokaila ndiye anayetangulia kulianzisha kwa mazoezi mengine ya kuimarisha mwili.

Mazoezi hayo humaliziwa na mengine ya kucheza mpira ambayo yanasimamiwa na Folz na wasaidizi wake wengine huku Mokaila akiwa pembeni.

Jana Folz alipunguza dozi hiyo kwa timu hiyo kufanya mazoezi mara moja pekee yakifanyika asubuhi akitaka wachezaji wake kupata nafasi ya kwenda kuangalia mchezo wa Taifa Stars inayoshiriki fainali za Ubingwa wa Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024.