Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe akifungua Mkutano
wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) kwa niaba ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf
Masauni jijini Dar es Salaam leo Agosti 07, 2025.
Mwenyekiti wa
Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu
Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) ambaye pia ni Mshauri wa Rais katika masuala ya
Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi akitoa neno la
utangulizi wakati wa Mkutano
wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) jijini Dar es Salaam leo Agosti
07, 2025.
Washiriki wakiwa katika Mkutano
wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) jijini Dar es Salaam leo Agosti
07, 2025.
Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya
Tabianchi (AGN) ambaye pia ni Mshauri wa Rais katika masuala ya
Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi. Kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Kanizio
Mannyika na Mjumbe wa Mkutano wa AGN kutoka Misri Bw. Khalid Mohamed wakati wa Mkutano AGN jijini Dar es Salaam leo Agosti 07, 2025.
…………………….
Tanzania imeweka msisitizo kwa nchi za Afrika kuungana
na kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unakuwa endelevu ili kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira)
Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe wakati akifungua Mkutano
wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN)
kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni jijini Dar es Salaam leo Agosti 07, 2025.
Prof. Msoffe amesema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa wadau wote
wa mazingira kuguswa na kupaza sauti ili kuokoa sekta hiyo kutoka kwenye
changamoto za uharibifu wa namna yoyote ile.
Alisema katika mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 60 utakuwa
na kazi ya kupokea
taarifa ya mijadala mbalimbali ili kuwa na
sauti moja kwa
lengo la kuwakilisha maslahi ya Bara la Afrika katika mazungumzo ya kimataifa
ya mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Prof. Msoffe alibainisha kuwa kuanzishwa
kwa Sekretarieti ya AGN ni hatua muhimu kwani itahakikisha kila nchi ya
Kiafrika, inapata utaalamu katika masuala ya hifadhi ya mazingira.
“Ingawa
lengo letu la msingi ni kuanzishwa kwa Sekretarieti ya AGN, tuchukue muda
kutafakari mambo muhimu kutoka kwa mikutano iliyopita ikiwemo wa AMCEN
uliofanyika jijini Nairobi, Kenya kwani taarifa hizi ni muhimu katika kuboresha
vipaumbele vya Afrika tunapojiandaa kwa Mkutano wa COP30 unaotarajiwa kufanyika
Belém, Brazili,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa AGN ambaye pia ni Mshauri wa Rais katika masuala ya
Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi alisema
mkutano huo unahusu nchi zote 54 wanachama wa Umoja wa
Mataifa kuhusu mabadiliko tabianchi.
Alisema miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa ni pamoja na kuifanya
AGN ilioanzishwa mwaka 1995 kuwa ni taasisi ya Afrika imara ya Afrika ambayo
imeweza kuusimamia Mkataba wa Kyoto unaozitaka
nchi wanachama kupunguza uzalishaji wa gesijoto.
Pia, Dkt. Muyungi alisema hatua nyingine ni kuwa na
ukusanyaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi ulio wazi na kuhakikisha inakuwa
chini ya Umoja wa Afrika na kuweka uelewa, kumbukumbu na historia ya mambo
yanayofanyika.
Naye Mshauri Maalumu wa Masuala ya Mabadiliko ya
Tabianchi Bi. Kholuthm Omar alisema mkutano huo ni muhimu kujadili namna bora
ya kuwasaidia wakulima, wavuvi na wafugaji wanaoathirika zaidi na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo wa Pili wa AGN ulioandaliwa chini ya uongozi wa Tanzania
kwa ushirikiano na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) ni hatua kubwa ya kuunda
mikakati ya Afrika ya mazungumzo ya hali ya hewa kwa mwaka 2025
Mkutano
huo utajikita katika kuimarisha uratibu miongoni mwa nchi wanachama kwa
kujadili na kukamilisha Vifungu vya Uanzishaji wa Taasisi kwa Sekretarieti ya
AGN.
Halikadhalika,
itajiandaa kwa Mkutano ujao wa Pili uliopangwa kufanyika Septemba 8 hadi 10,
2025, jijini Addis Ababa, Ethiopia, huku ikiunganisha vipaumbele vya Afrika kwa
kuzingatia mwongozo wa Kikao cha 20 cha Mkutano wa Mawaziri wa Afrika kuhusu
Mazingira (AMCEN-20).