Ajali ya helikopta yaua Waziri wa Ulinzi, Mazingira Ghana

Dar es Salaam. Ajali ya helikopta imetoka jana Jumatano asubuhi katika eneo la Ashanti nchini Ghana na kusababisha vifo vya watu wanane huku kati ya hao kuna mawaziri wawili.


Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Ghana, watu wote wanane waliokuwamo kwenye helikopta hiyo wamefariki dunia huku miongoni mwao ni Waziri wa Ulinzi, Edward Boamah na Waziri wa Mazingira Ibrahim Murtala.

Kituo cha televisheni cha Joy News kilionyesha mkanda wa video iliyorekodiwa na simu kutoka eneo la ajali ikionyesha mabaki ya ndege yakiwaka moto na kufuka moshi katika eneo la msitu mkubwa mapema jana.

Wengine ni Mohammad Limuna, Naibu Mratibu wa Usalama wa Kitaifa na waziri wa zamani wa kilimo na Samuel Sarpong, makamu mwenyekiti wa Chama cha National Democratic Congress (NDC).

Katika ajali hiyo, Jeshi la Wananchi wa Ghana liliripoti mapema Jumatano kuwa helikopta ya Jeshi la Anga ilitoweka kwenye rada muda mfupi baada ya kupaa kutoka Accra saa 3:00 asubuhi kwa saa za Ghana (09:00 GMT), ikielekea mji wa Obuasi, kaskazini-magharibi mwa mji mkuu.


Taarifa hiyo ilieleza kulikuwa na wahudumu watatu na abiria watano ndani ya ndege hiyo.

Ikielezwa zaidi kuhusu Waziri Boamah alikuwa akiongoza Wizara ya Ulinzi ya Ghana wakati ambapo makundi yenye silaha yamekuwa yakisumbua mipaka ya kaskazini na Burkina Faso. Al Jazeera.

Ingawa Ghana haijakumbwa na waasi kutoka Sahel kama majirani zake Togo na Benin, wachambuzi wameonya juu ya kuongezeka kwa biashara haramu ya silaha na wapiganaji kuvuka mpaka kutoka Burkina Faso na kutumia Ghana kama kambi ya nyuma.


Kufuatia ajali hiyo, Umoja wa Afrika AU, umetuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Ghana, John Mahama, serikali ya nchi, watu wa Ghana, pamoja na familia za wafiwa, kufuatia ajali hiyo iliyotokea Agosti 6, 2025.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf amesikitishwa na ajali hiyo iliyogharimu maisha ya watu wote waliokuwamo.

“Umoja wa Afrika upo pamoja na Ghana katika wakati huu mgumu. Roho za marehemu zipumzike kwa amani,” amesema.