Bodaboda aliyoepa kitanzi kesi ya mauaji ya mkewe

Arusha. Mahakama ya Rufaa imemuachia huru Baraka Jeremiah, dereva wa bodaboda aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya mkewe, Hawa Baraka.

Jeremiah alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Novemba 28, 2022 alipotiwa hatiani kwa mauaji ya Hawa yaliyotokea Septemba 24, 2017 katika eneo la Sing’isi wilayani Arumeru, mkoani Arusha.

Mahakama ya Rufaa imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka kuwa ndiye aliyehusika na mauaji.

Hukumu ya rufaa imetolewa Agosti 6, 2025 na jopo la majaji lililoketi Arusha, ambao ni Rehema Mkuye, Lucia Kairo na Gerson Mdemu. Nakala ya hukumu imewekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jopo hilo baada ya kupitia rekodi na sababu za rufaa ambazo ziliungwa mkono na upande wa Jamhuri, limeeleza kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa kupitia ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa mahakamani.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watatu na kielelezo kimoja.

Ilielezwa mrufani na Hawa (marehemu) walikuwa mke na mume na kwamba, siku ya tukio haijabainika wazi nini kilitokea ila asubuhi mrufani alikwenda kwa majirani zake (Samwel Jeremiah na Richard Jeremiah) kutafuta msaada ili ampeleke mkewe hospitali kwa kuwa alikuwa mgonjwa.

Walipofika nyumbani kwa mrufani walimkuta Hawa akiwa amelala chini na hana fahamu, mwenye majeraha kichwani na usoni, huku jicho la kulia likiwa limevimba.

Shahidi wa tatu, ACP Daud Mapunda, alisema alipokea taarifa kuwa mrufani alimshambulia mke wake na anafanya jitihada za kuficha ukweli, kwani hakuripoti polisi.

Alieleza wakiwa wanajadiliana ndugu wa Hawa (marehemu) na mrufani walikwenda ofisini kwao, Kituo cha Polisi cha Usa River kutoa taarifa, hivyo mrufani alikamatwa pamoja na shahidi wa pili, Gabriel Ephrahim (askari polisi mstaafu wa kituo hicho).

Mwili ulipofanyiwa uchunguzi na shahidi wa kwanza, Dk Abel Ndago ilibainika chanzo cha kifo ni kushindwa kupumua kutokana na kuumia kichwani na kukosa hewa ya oksijeni.

Shahidi wa tatu akiwa mpelelezi wa kesi hiyo, alitembelea nyumba ya mrufani na kukuta ikiwa safi, haina dalili za damu wala mapambano akatafsiri kuwa ni jaribio la kuficha ushahidi.

Mshtakiwa (mrufani) alikana kutenda kosa hilo na kueleza siku ya tukio alimtembelea dada yake Fatuma Juma, eneo la Sanawari na hakupatikana kwa simu usiku huo, asubuhi alimkuta (marehemu) akiwa amejeruhiwa nje ya nyumba yao baada ya kuletwa na mtu asiyejulikana na pikipiki.

Mrufani alikana kumjeruhi kwa madai kuwa alimpeleka Hospitali ya Tengeru kisha akaenda Kituo cha Polisi cha USA River kuripoti tukio hilo na kupata fomu namba tatu (PF3) lakini aliishia kukamatwa.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili mahakama ya chini iliona upande wa mashtaka ulithibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote, ikamtia hatiani na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa.

Mrufani hakuridhika na hukumu hiyo akakata rufaa akiwa na sababu tano. Aliwakilishwa na wakili Richard Manyota, huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Naomi Mollel.

Naomi alieleza ni msimamo wao kuwa, wanaunga mkono rufaa kwa msingi kuwa, kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa kwa kiwango kinachohitajika.

Aliielekeza mahakama katika ukurasa wa 108 wa kumbukumbu za rufaa iliyotokana na ushahidi wa kimazingira kuwa, mrufani alishindwa kuripoti tukio hilo kituo cha polisi mara moja, nyumba yake ilisafishwa na yeye mwenyewe au watu wengine jambo ambalo lilizua shaka na mrufani alishindwa kuripoti kutoweka kwa mkewe kwa wakati.

Alieleza ili ushahidi wa kimazingira utegemewe ni lazima uelekeze bila kupingwa, lakini katika kesi hiyo ushahidi unaoitwa wa kimazingira ni tuhuma tu na mtoa taarifa kwa shahidi wa tatu hakutoa ushahidi wake mahakamani jambo ambalo limeibua shaka.

Kuhusu usafi wa nyumba ya mrufani, Naomi alisema hakuna shahidi aliyetoa ushahidi kuwa alimuona mrufani au ndugu zake wakifanya usafi wa nyumba hiyo ili kuficha kitu na kuhitimisha kuwa, mrufani alitiwa hatiani kwa tuhuma tu.

Alidai kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa bila ya kuacha shaka yoyote na kuwasihi majaji kuondoa hatia, kutengua hukumu dhidi ya mrufani na kumuachia huru.

Wakili wa mrufani alikubaliana na hoja za wakili wa Jamhuri na kusisitiza kuwa, mrufani alitiwa hatiani kwa tuhuma tu hivyo kuomba rufaa hiyo iruhusiwe, hukumu ifutwe, adhabu itenguliwe na mrufani aachiwe.

Majaji baada ya kuchunguza sababu za kukata rufaa na mawasilisho ya pamoja kutoka kwa pande zote mbili, walisema wanaona suala kuu la kuzingatia ni iwapo kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Jaji Mkuye amesema ni jambo la kawaida kwamba hukumu ya mrufani kulingana na ushahidi wa kimazingira kwani hapakuwa na shahidi aliyeshuhudia wakati kosa hilo lilipotekelezwa.

Amesema ili ushahidi wa kimazingira utegemewe kuweka hatia, kuna kanuni elekezi ambazo zinapaswa kutimizwa, akinukuu kesi ya Manoja Masalu na mwenzake dhidi ya Jamhuri.

Amesema ushahidi uliowezesha mrufani kutiwa hatiani ni kwamba, alimkimbiza (marehemu) hospitalini bila kuripoti tukio hilo polisi na kupata PF3 na kwamba, nyumba yake ilipatikana kuwa safi isivyo kawaida ikipendekeza alikuwa akificha ushahidi.

“Hata hivyo, tunakubaliana na hoja ya Naomi ambayo ilikubaliwa na wakili Manyota kwamba, ushahidi huo pekee hauwezi kuwa wa kimazingira chini ya sheria. Tumechunguza ushahidi ambao ilitegemewa kutoa hatia dhidi ya mrufani,” amesema.

Amesema wakati wa usikilizwaji wa awali, Absalom Charles pia aliorodheshwa kuwa miongoni mwa mashahidi ila kwa sababu zisizojulikana mashahidi waliotajwa hawakuitwa kutoa ushahidi mahakamani.

Jaji huyo kwa niaba ya jopo alihitimisha kuwa, wanaona kesi dhidi ya mrufani haikuthibitishwa bila kuacha shaka, hivyo wanaruhusu rufaa, kufuta hukumu na kuamuru mrufani aachiwe huru.