Dar es Salaam. Unaweza kusema bundi bado amekita kambi ukanda wa Gaza hii ni baada ya lori lililokuwa likipeleka msaada wa chakula kupinduka na kuuwa watu 20.
Lori hilo lilipinduka katikati ya umati wa watu juzi Jumanne usiku ambapo kwa mujibu wa Shirika la Ulinzi wa Raia wakazi wa Gaza wamekuwa wakisubiri msaada wa chakula kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa RFI, Israel inawalazimisha madereva kutumia barabara zilizojaa watu wenye njaa ambao wamekuwa wakisubiri kwa wiki kwa mahitaji ya kimsingi huku Serikali ya Gaza inayoongozwa na Hamas ikishutumu hatua hiyo.
“Lori hilo limepinduka wakati mamia ya raia walikuwa wakisubiri msaada wa chakula katika eneo la Nusseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza,” msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Raia, Mahmoud Bassal ameliambia Shirika la Habari la AFP.
Taariza zaidi ya BBC inasema watu walikusanyika karibu na malori hayo kwenye barabara iliyo kusini mashariki mwa Deir al-Balah wakapanda juu ya malori hayo na kusababisha dereva kupoteza udhibiti.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Qu Dongyu, limesema Gaza sasa iko kwenye ukingo wa njaa kamili.
Kulingana na Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas, watu 193 wamekufa kutokana na njaa na utapiamlo tangu kuanza kwa vita.
Takriban asilimia 90 ya watu milioni 2.1 wa Gaza wamehama na wengi wao wanaishi katika mazingira magumu na hatari.
Umoja wa Mataifa umetoa wito mara kwa mara kwa kuruhusiwa kwa usambazaji kamili na endelevu wa misaada, lakini upatikanaji bado ni wa mara kwa mara na malori mengi ya misaada yanaibiwa.
Ikumbukwe Israel ilianzisha mashambulizi yake ya kijeshi huko Gaza kujibu shambulio la Hamas kusini mwa Israeli Oktoba 7, 2023, ambapo watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa kama mateka.
Kulingana na wizara ya afya ya Hamas, Wapalestina 61,020 wameuawa na vikosi vya Israeli huko Gaza tangu wakati huo.
Hata hivyo, zaidi ya mashirika 100 ya misaada na haki za binadamu wameonya juu ya njaa kubwa huko Gaza na kuishutumu Israeli kwa kuzuia usambazaji wa misaada.
Aidha, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, anakanusha madai hayo na kusisitiza kuwa nchi yake haizuii misaada.