Chadema katika kibarua kingine mahakamani leo

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, leo Alhamisi, Agosti 7, 2025 inatarajiwa kusikiliza shauri la maombi ya marejeo lililofunguliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) la kupinga amri za kukizuia kufanya shughuli za siasa na kutumia mali zake.

Amri hizo za zuio dhidi ya chama hicho zilitolewa na Jaji Hamidu Mwanga, Juni 10, 2025, kufuatia shauri la maombi lililofunguliwa na walalamikaji katika kesi ya madai dhidi yake kuhusu mgawanyo wa rasilimali kati ya Bara na Zanzibar.

Kesi hiyo namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, makamu mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Sambamba na kesi hiyo pia walalamikaji hao walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba Mahakama itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo ya msingi itakapoamuliwa.

Awali, walalamikiwa walipambana kuimaliza kesi hiyo kwa mbinu za kiufundi baada ya kuwasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi ya msingi na dhidi ya shauri dogo la maombi ya zuio lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda kwani Juni 10, 2025 Mahakama hiyo iliyatupilia mbali.

Vilevile, ilisikiliza shauri la maombi ya zuio ambayo katika uamuzi wake ilikubaliana na hoja za walalamikaji na kukizuia chama hicho shughuli zote za kisiasa.

Hivyo Mahakama mbali na amri ya zuio kwa walalamikiwa kujishughulisha na shughuli zozote za kisiasa, pia iliwazuia waadawa hao binafsi, wakala wao au mtu yeyote anayefanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao, kutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Walalamikiwa hawakukubaliana na uamuzi huo, hivyo wakafungua shauri la marejeo, wakiiomba Mahakama irejee na kisha iondoe amri hizo wakidai zilitolewa isivyo halali.

Sambamba na shauri hilo la marejeo pia waliandika barua ya kumkataa Jaji Mwang,a wakimtaka ajiondoe kusikiliza kesi hiyo wakidai kuwa hawana imani naye.

Jaji Mwanga baada ya kusikiliza sababu zao za kumkataa katika uamuzi wake alioutoa Julai 28, 2025, alikataa kujiondoa katika kesi hiyo na maombi ya marejeo akisema hoja zao hazikuwa na msingi wa kisheria. Aliamua kuwa ataendelea kusikiliza keai hiyo na akapanga kusikiliza shauri lao la marejeo leo Agosti 7, 2025. Hivyo wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mawakili wa Chadema watakuwa na kibarua kizito kuishawishi mahakama kuwa ilikosea katika kutoa amri hizo na hatimaye iziondoe.

Vilevile watakabiliwa na upinzani kutoka kwa mawakili wa walalamikaji ambao nao watajibu hoja zao kabla ya Mahakama kutoa uamuzi. Wakati walalamikiwa wakiwa wameshafungua shauri hilo la kupinga amri hizo na kumkataa jaji, nje ya mahakama kuliibuka msigano wa tafsiri za amri hizo za zuio baina ya pande hizo mbili kwenye kesi hiyo.

Viongozi wa Chadema hususani Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika mara kadhaa walinukuliwa na vyombo vya habari wakidai amri hizo zinawahusu wadaiwa pekee yaani Bodi ya wadhamini na Katibu Mkuu. Walalamikaji kwa upande wao kupitia jopo la mawakili wao, Shaban Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis wamekuwa wakipinga tafsiri hiyo ya amri hizo wakidai kuwa linawahusu viongozi na wanachama wote.

Kutokana na msigano huo, Julai 2, 2025 mawakili wa walalamikaji walimwandikia barua naibu msajili wa mahakama hiyo, kuomba ufafanuzi wa wigo wa amri hizo. Naibu Msajili katika barua yake ya Julai 14, 2025 kwenda kwa pande zote ilitoa ufafanuzi ilibainisha makundi 10 ya watu ambao amri hizo zote zinawafunga. Alibainisha viongozi wote kuanzia ngazi ya kitaifa mpaka ngazi ya chini kabisa na wanachama wote wa kawaida pamoja na mawakala.

Endelea kufuatilia Mwananchi