Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimezindua Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, leo Alhamis Agosti 7, 2025.
Chauma kimekuja na ilani ambayo inaahidi mageuzi makubwa katika maendeleo ya watu kwa kutumia rasilimali za ndani, kupambana na umaskini na kujenga utawala unaosimamia haki, uwajibikaji na sheria.
Msemaji wa chama hicho, John Mrema akiwasilisha ilani hiyo mbele ya Mkutano Mkuu kwa niaba ya uongozi wa juu wa Chaumma, amesema ilani hiyo imeandaliwa baada ya kupitia maoni ya wananchi na kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema Ilani ya Chaumma inalenga kujenga taifa la watu walio huru kiuchumi na kisiasa, kupitia mageuzi ya sekta za kilimo, elimu, afya, teknolojia, miundombinu, pamoja na kuimarisha muundo wa Muungano ili kuhakikisha pande zote zinanufaika kikamilifu.
Pia ilani hiyo imebaini mambo yatakayotekeleza haraka na mpango wa muda mrefu katika utekelezwaji wake.

Mageuzi ndani ya siku 100
Mara tu baada ya kuingia madarakani, Serikali ya Chaumma inapanga kuwasilisha bungeni muswada wa kuhuisha mchakato wa Katiba mpya, hatua inayoelezwa ya msingi katika kuweka utawala wa kidemokrasia na haki za kiraia.
“Serikali itaanzisha Tume huru ya kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu utekaji, unyanyasaji, madai ya watumishi wa umma na migogoro ya ardhi,” amesema Mrema.
Huduma ya lishe bora shuleni na hospitalini kupitia mpango wa “Ubwabwa kwa wote” ni miongoni mwa mambo ya haraka yatakayotekelezwa ndani ya siku 100.
Pia amesema, tozo zote kandamizi katika sekta ya kilimo na mifugo zitaondolewa ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa chakula bora.
“Serikali pia itatunga sheria ya kuruhusu serikali za mitaa kuwa na vyanzo huru vya mapato kwa maendeleo ya ndani ili ziweze kuhudumia wananchi vyema,” amesema Mrema.
“Kwa upande wa teknolojia, sheria ya kusimamia matumizi ya akili unde (AI) itatungwa, ili kuifanya teknolojia hiyo kuwa fursa ya maendeleo badala ya tishio,” ameongeza.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, Chaumma inasisitiza kuweka muundo wa serikali tatu; yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kila upande utakuwa na bunge lake, huku Bunge la Muungano likibaki na majukumu ya masuala ya pamoja pekee. Msingi wa hoja hii ni kuleta usawa wa mamlaka na rasilimali kati ya pande mbili za Muungano.
Kuhusu maadili, rrdhi na kodi
Katika eneo la maadili, Chaumma inapanga kuanzisha taasisi ya kusimamia maadili ya viongozi ili kupambana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
“Serikali ya Chaumma, itaondoa kodi zote za vifaa vya ujenzi ili kuwezesha wananchi kuboresha makazi yao kwa gharama nafuu,” amesema Mrema.
Ilani hiyo imeweka bayana kuwa, kwa upande wa ardhi, usajili wa hati utakuwa bure, na ardhi itapimwa ili kuwezesha wananchi kuitumia kama dhamana ya mikopo na miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, bidhaa muhimu kama chumvi, sukari, mafuta, pembejeo za kilimo, mchele na viberiti hazitatozwa kodi, lengo likiwa ni kupunguza gharama za maisha kwa wananchi wa kipato cha chini.

Kilimo, mifugo na uhuru wa soko
Chaumma imeweka bayana kwamba Serikali yake itatenga sehemu kubwa ya bajeti kwa kilimo, kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na ofisa ugani na kuanzisha maeneo rasmi ya umwagiliaji.
“Wakulima hawatalazimishwa kuuza mazao yao kupitia vyama au kwa bei wanayoamriwa na Serikali. Kwa mfano, korosho haitalazimika kuuzwa kupitia vyama vya msingi (AMCOS), na karafuu haitatawaliwa tena na mfumo wa serikali kuu,” amesema Mrema.
“Katika sekta ya mifugo, maeneo maalumu yatatengwa ili kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji, na kuwezesha shughuli hizo kufanyika kwa ufanisi bila mivutano ya ardhi,” ameongeza.
Biashara, madini na utalii
Chaumma imesema mizigo bandarini itatolewa ndani ya siku 14 bila urasimu wa ushuru. Hii ni hatua ya kuondoa usumbufu wa kikodi na kuongeza kasi ya biashara.
Kwa upande wa madini, sheria mpya itaweka sharti kuwa wananchi wanaoishi maeneo ya migodi wanapewa hisa katika migodi hiyo. Mmiliki wa ardhi atapewa mamlaka kamili ya kunufaika na rasilimali hiyo.
“Katika utalii, Chaumma itahakikisha wananchi wanaopakana na hifadhi na vivutio wanashirikishwa kunufaika. Kodi kwenye sekta ya utalii zitapunguzwa ili kuvutia watalii wa ndani na wa nje, ili binadamu asibezwe zaidi ya wanyama,” amesisitiza Mrema.

Mazingira, tehama na nishati
Chaumma imeeleza dhamira ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa elimu na teknolojia kwa wakulima na wafugaji.
“Katika teknolojia ya habari, gharama za vifurushi vya intaneti vitashushwa, na huduma za afya zitaanza kupatikana kwa njia ya mtandao ili kupunguza misururu hospitalini,” amefafanua Mrema.
Amesema huduma ya umeme pia itaboreshwa kwa kupunguza gharama za kuunganishwa, ambapo wananchi watalipia kwa awamu kupitia mfumo wa luku.
“Chaumma itaweka mpango wa utoaji wa taulo za kike shuleni bila malipo, huduma za vyoo shuleni zitaboreshwa na somo la lishe litarejeshwa ili kuwajengea wanafunzi tabia ya ulaji bora,” amesema Mrema.
Ilani hiyo imaweka mipango kuwa huduma za afya zitapanuliwa kwa kuanzisha bima ya afya kwa wote, huku chakula kwa wagonjwa hospitalini kikijumuishwa kama sehemu ya tiba.
Kwa mujibu wa ilani hiyo, Serikali ya Chaumma inapanga kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salam hadi Mtwara na Ruvuma ili kufungua fursa za biashara na usafirishaji wa makaa ya mawe.
Kuhusu huduma za bandari, Mkataba wa DP World utapitiwa upya, ili kuhakikisha unazingatia masilahi ya Watanzania.
Sanaa, michezo na utamaduni
Chaumma imeahidi kuwezesha vilabu vya michezo, timu za taifa na ushirikisho kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa. Sanaa na utamaduni wa Kitanzania vitapewa msukumo kama uti wa mgongo wa taifa.
Ilani hiyo ya Chaumma inaweka msisitizo mkubwa kwa Zanzibar, ikitaka irejeshewe mamlaka kamili ya ndani na ya kimataifa. Zanzibar itakuwa na kiti chake Umoja wa Mataifa, uwezo wa kukopa kutoka nje, na mapato yake yasigawiwe kwa kibali kutoka Tanganyika.
Chaumma imesema Zanzibar itanufaika na uchumi wa buluu kwa kutoa ajira zaidi ya 400,000 kwa vijana kupitia ununuzi wa boti za uvuvi, kuanzisha vituo vya ujasiriamali Unguja na Pemba, pamoja na kuimarisha utalii kwa kuwajengea vijana uwezo wa lugha za kigeni.
“Rasilimali za mafuta na gesi chini ya bahari zitatambuliwa kama mali ya Zanzibar, na vijana wa visiwani wataandaliwa kunufaika nazo,” amesema Mrema.
“Zanzibar itapewa fursa ya kushiriki michezo ya kimataifa kama Fifa na CAF kwa jina lake, badala ya kupitia Tanganyika,” amesisitiza.
Ilani hiyo, imewasilishwa na kupitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu kwa sauti moja.
Hatua hii inafungua fursa kwa chama hicho kuingia katika kinyang’anyiro cha urais kushawishi wa Tanganzania kukipa ridhaa chama hicho kuongoza Serikali.