Dau la Ecua Yanga kiboko

YANGA imemtambulisha mmoja ya washambuliaji wapya kutoka Ivory Coast, Celestin Ecua aliyemaliza Ligi ya nchi hiyo akiwa na mabao 15 na asisti 12 na huku mtandaoni mashabiki wa klabu hiyo wanatamba, lakini ni kwamba dau lililomfanya atue Jangwani sio la kitoto.

Straika huyo aliyepewa mkataba wa miaka mitatu inaelezwa ni mmoja ya nyota wanaokunja mkwanja wa maana klabuni hapo kutioka na dau alililowekwa mezani kuanzia fedha za usajili hadi mshahara atakaokuwa akilipwa kila mwezi.

Ecua aliyekuwa akiwindwa pia na Simba, inaelezwa kuwa mkataba aliosainiwa una thamani ya Dola 438,000 (zaidi ya Sh 1 bilioni) likijumuisha dau la usajili na mishahara atakayovuna kwa miaka mitatu.

Kwa mwaka wa kwanza ambao Ecua atachukua Dola 70,000 (zaidi ya Sh 175 Milioni) kama ada ya usajili, huku akibeba mshahara wa Dola 7,000 (zaidi ya Sh 17 milioni) kwa mwezi

Kiasi hicho cha msharaha ndani ya mwaka wa kwanza mwamba atakunja si chini ya Dola 84,000 (zaidi ya Sh 211 milioni) kwa muda wa miezi 12 atakayoichezea Yanga.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka Yanga ni kwamba mwaka wa pili sasa kama kiwango chake kitaongezeka na kuwaridhisha mabosi wa Yanga, basi kutakuwa na ongezeko la mshahara kwa Dola 1000 zaidi hadi kufikia 8000 (zaidi ya Sh 20 milioni) kwa mwezi. Hii ikiwa na maana kwa miezi 12 ya mwaka wa pili wa mkataba atakusanya Dola 96,000 ( zaidi ya Sh 241 milioni) kwa miezi 12.

Msimu wa mwisho wa mkataba huo Ecua, aliyekuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, atapandishiwa mshahara kwa dola 1000 tena na kufikia 9000.

Lakini msimu huo atachukua pia sehemu ya mwisho ya ada ya usajili akipokea kiasi cha Dola 80,000 na kufikisha jumla Dola 150,000 kwa mkataba huo wa miaka mitatu.

Kama mshambuliaji huyo atafunga mabao zaidi ya 10 atavuna Dola 10000 kama bonasi, ambapo kama atafikisha 20 atachukua kiasi cha Dola 15000.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa;”Hata hivyo Yanga imemtega Ecua, ikimtaka kuhakikisha kila msimu unapomalizika ahakikishe kiwango chake kinapanda, ambapo hakutakuwa na ongezeko kama atakuwa ameonyesha kiwango cha kawaida kwenye mkataba huo.

“Mbali na suala la kiwango pia Yanga imemtaka mshambuliaji huyo kujipanga kufanya makubwa, endapo kiwango chake kitakuwa cha kawaida na kusitishiwa mkataba anaweza kukosa mgao wa pili wa ada yake ya usajili ya Dola 80,000,” kilisema chanzo hicho.

Yanga imeshaanza maandalizi ya kuelekea msimu ujao, ikiwa na baadhi ya wachezaji huku wengine wakiwa katika majukumu ya timu ya taifa, inayoshiriki fainali za CHAN 2024.