DKT. JINGU AITAKA BODI YA MITIHANI VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII KUZINGATIA WELEDI.

Na WMJJWM – Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu ameitaka Bodi ya Mitihani ya Vyuo vya Maendeleo na Maendeleo ya Jamii ufundi kuhakikisha weledi unazingatiwa katika mitihani ya wanafunzi ili waweze kuwa wahitimu mahiri wenye tija kwa Maendeleo ya taifa.

Dkt Jingu amesema hayo Agosti 7, 2025 Jijini Dodoma, wakati akizindua Bodi mpya ya mitihani ya Vyuo vya Maendeleo na Maendeleo ya Jamii Ufundi, baada ya Bodi ya awali kumaliza muda wake.


Dkt. Jingu amesema kuwa ni muhimu Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Maendeleo ya Jamii Ufundi kuzingatia usimamizi na ubora wa Mitihani ya wanafunzi ili kuzalisha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ambao watakuwa na ujuzi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Nawapongeza kwa kukubali uteuzi wa kutumika katika bodi hii, nawaomba muendelee kusimamia kwa weledi taratibu na sheria za mitihani, kwa sababu kada ya Maendeleo wa Jamii ni moyo wa taifa, hivyo ni lazima tuwe na Wataalam wenye tija kwa Maendeleo ya jamii” amesema Dkt Jingu.

Aidha Dkt. Jingu amewataka wakufunzi wa Vyuo hivyo kufundisha kwa kutumia teknolojia ya TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na wanafunzi waweze kuitumia kwa tija katika kupata ujuzi na utaalam.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi anayemaliza muda wake Dkt. Christina Mandara ameshukuru Menejimenti ya Wizara kwa kumpa nafasi ya kutumikia bodi hiyo tangu mwaka 2018/2019 hadi 2024/2025 na kwa kumpa nafasi ya kutoa ushauri katika uendeshaji wa Mitihani katika Vyuo hivyo.

Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Mitihani ya Vyuo vya Maendeleo na Maendeleo ya Jamii ufundi Dkt. Sanford Sanga ameshukuru kwa uteuzi wa nafasi hiyo na kuahidi kuzingatia sheria , kanuni na taratibu kuhakikisha Bodi hiyo inafanya kazi kwa weledi ili wanafunzi waweze kuhitimu wakiwa na maarifa stahiki kwa Maendeleo ya taifa.