DR Congo yazinduka CHAN, yainyoa Zambia

BAADA ya kupoteza mechi ya kwanza ya mashindano ya CHAN 2024 inayoendelea kutimua vumbi ukanda wa Afrika Mashariki, DR Congo imepata ushindi wa kwanza jioni hii dhidi ya Zambia. 

DR Congo ilianza michuano hiyo ilichapwa katika mechi ya kwanza dhidi ya wenyeji, Kenya ambao usiku huu wapo uwanjani kutupa karata ya pili katika michuano hiyo.

Mabao ya DR Congo katika mechi ya leo ya kundi A  yamefungwa na Ibrahim Matobo Mubalu dakika ya 51 na Malanga Horso Mwaku dakika ya 71, ushindi huo umefufua matumaini ya Wakongomani kutinga hatua ya robo fainali.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi Kenya, Les Leopards ambao ni mabingwa mara mbili wa CHAN, walipiga mashuti 13 huku manne yakilenga lango.

Zambia yenyewe licha ya kuwa umiliki mkubwa kwa asilimia 60 dhidi ya 40 za DR Congo, ilipiga mashuti sita, huku mawili tu ndio yakilenga lango la wapinzani wao.

Kwa Zambia inayonolewa na kocha wa zamani wa Chelsea, Avram Grant na iliyocheza mechi kwanza, kipigo hicho ni cha kwanza kwao na bado ina nafasi katika mechi ijayo ambayo itachezwa Jumapili dhidi ya Angola.