Foba kiroho safi kwa Manula

KIPA wa Azam FC, Zuberi Foba amesema ni furaha kwake kucheza timu moja na Aishi Manula aliyemtaja kuwa ni mwalimu kwani ndiye aliyekuwa anamtazama kabla ya kuanza kucheza soka la ushindani huku akitaja sababu za kumuachia jezi namba 28.

Manula atakuwa sehemu ya kikosi cha Azam msimu ujao baada ya kujiunga akitokea Simba na ameachiwa jezi namba 28 ambayo amekuwa akiivaa tangu ameanza kucheza Ligi kuu akiwa timu hiyo na baadae Azam FC.

Akizungumza na Mwanaspoti, Foba alisema ameongea na meneja wa Azam FC juu ya kumuachia Manula jezi namba 28 ambayo ameweka wazi kuwa aliiomba apewe jezi hiyo kutokana na heshima aliyonayo kwa kipa huyo aliyemtaja kuwa ni namba moja kwake.

“Manula ndio mfano wangu wa kuigwa ‘Role model’ nilipotua Azam FC niliomba jezi namba 28 kwasababu ya heshima ya Manula ambaye kipindi naanza  mpira nilikuwa namuangalia. Nafurahi kucheza naye pamoja kwani ni mwalimu nina mengi ya kujifunza,” alisema na kuongeza:

‘’Nilipopata taarifa kuwa amejiunga na Azam FC kama nilivyofanya mwanzo kuomba nikafanya hivyo kuirudisha kwa sababu amekuja mwenye namba yake. Namuachia nitaendelea kutumia namba yangu ya mwanzo na kuhusu namba kila namba ina maana yake kuna bahati, tarehe za kuzaliwa kwangu nilitumia 28 kwa sababu ya Aishi.”

Foba alisema anarudi kutumia namba 32 ambayo ameitaja kuwa ni namba ya bahati kwake kwa sababu alianza kuivaa akiwa timu ya vijana hadi anapanda.

Akimzungumzia furaha ya kucheza timu moja na Manula, alisema ni jambo ambalo hakulitarajia kwani alianza kumtazama kabla ya kutimkia Simba.