Funza mwekundu tishio, mikoa tisa yasitisha kilimo cha pamba

Morogoro. Bodi ya Pamba Tanzania ikishirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) inaendela kufanya utafiti wa kumdhibiti funza mwekundu baada ya kuwa kikwazo na tishio katika uzalishaji wa zao la pamba kwa badhi ya mikoa nchini.

Tayari mikoa mikoa sita imeshasitisha kilimo hicho kutokana na uharibifu wa mimea na kushuka kwa uzalishaji.

Watafiti na watalaamu wa zao la pamba bado wanakuna vichwa kupata mbinu za kumdhibiti funza huyo hatari huku wakitoa elimu kwa wakulima njia bora na ya kisasa za kupata mafanikio kupitia zao la Pamba.

Elimu hiyo inatolewa katika maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi Kanda ya Mashariki Nanenane yanayoendelea kwenye Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere mkoani Morogoro. 

Akizungumza na Mwananchi katika viwanja hivyo leo Alhamisi Agosti 7, 2025, Mtafiti wa Pamba kutoka Tari, Methusela Obedy amesema funza mwekundu aliingia nchini mwaka 1946 kupitia mikoa ya Lindi na Mtwara na tangu wakati huo, amekuwa tishio kwa wakulima wa zao la pamba katika mikoa hiyo na mingine minne nchini.

Obedy ametaja mikoa hiyo kuwa ni Rukwa, Njombe, Ruvuma na Mbeya huku utafiti ukigundua kuwa kukosekana kwa pambapori katika mikoa hiyo ndio sababu kuu ya kuvamia zao la pamba kwa kushambulia vitumba na vibahasha na kufanya mmea kuwa dhaifu.

“Mwaka 1999 alionekana Wilayani Chunya, Mbeya na sasa yupo Rukwa, Njombe na Ruvuma. Mikoa hii sita imeacha kulima pamba kutokana na athari kubwa za mdudu huyo anayeangamiza mimea hasa baada ya kukosa pambapori, hushambulia pamba inayolimwa,” amesema Obedy.

Amesema funza mwekundu hutegemea zaidi pambapori kwa chakula na hushambulia sehemu muhimu za mmea wa pamba kama vibahasha na vitumba, hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wakulima.

Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Alfonce Ngawagala amesema kilimo cha pamba nchini huzalishwa katika kanda mbili ya Magharibi na Mashariki huku kanda ya Magharibi ikiongoza kwa uzalishaji mkubwa wa pamba mbegu kwa asilimia 98.8.

“Kanda ya mashariki huzalisha asilimia 1.2 pekee, lakini bado jitihada zinaendelea kuhakikisha wakulima wote wanapata pembejeo, elimu ya kitaalamu na mbegu bora ili kuongeza uzalishaji,” amesema Ngawagala.

Amebainisha kuwa uzalishaji wa pamba mbegu katika misimu 10 ya kilimo kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2025/2026 umeendelea kupanda, mwaka huu wanatarajia kuvuna tani 437,219.

Mwaka 2018/2019 walivuna tani 222,725, 2019/2020 tani 348,963, 2023/2024 tani 282,316 na mwaka uliopita 2024/2025 tani 174,033.

Gabriel Mbwambo, mkulima wa pamba kutoka Kijiji cha Mkongaigunyu, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro amesema zao hilo lina faida kubwa iwapo mkulima atazingatia ushauri wa kitaalamu.