Hisia tofauti kifo cha Ndugai

Dodoma. Serikali imekemea tabia ya baadhi ya watu wanaoshangilia kifo cha Spika mstaafu, Job Ndugai na kusema watu hao hawana utu.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Simon Mayeka amesema wote wanaoshangilia msiba huu ni kwa sababu hawajui na hawajitambui huku akibainisha kuwa, wamekosa utu.

Mayeka amekemea tabia hiyo leo Alhamisi Agosti 7,2025 alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Ndugai baada ya kushuka kwenye gari kabla hajaingia ndani.

Katika moja ya mitandao ya kijamii tangu jana usiku, inasambaa picha mjongeo inayoonesha  kikundi cha watu wachache waliojirekodi wakishangilia msiba huo huku wakilitaja jina la Ndugai wazi wazi.

“Ile ni sehemu ndogo ya kijiji ambayo vijana wamejitokeza kushangilia, hiki kitu kinashangaza kwani si mila za Kitanzania wala utamaduni wetu na jambo hili halikubariki kabisa linapaswa kukemewa,” amesema Mayeka.

Mkuu huyo wa wilaya amewaomba wananchi wa Kongwa kuwa watulivu wakati huu wa msiba akiwataka wazazi wawakemee vijana wao kwa kuwa hakuna uadui wa kushangilia mauti ambayo ni mpango wa Mungu.

Amesema msiba wa mwanasiasa huyo mkongwe umekuwa wa ghafla na umeleta simanzi kwa familia, Taifa na wananchi wa Wilaya ya Kongwa.

Amesema vijana wanapaswa kukumbuka fadhila ya mwanasiasa huyo aliyekuwa mstari wa mbele kupigania suala la elimu wilayani Kongwa huku akihimiza ujenzi wa shule za msingi na sekondari.

“Mara zote aliona urithi mzuri kwa vijana ni elimu, ndiyo maana alipambana kuona shule zinajengwa kwa wingi ili vijana waende wakasome kwa manufaa yao ya baadaye,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

“Ndugai amefanya mambo mengi ya maendeleo kwa wananchi wa Kongwa, aliamini elimu ni nyenzo muhimu ya kuwainua kiuchumi na katika kata 22, tayari shule 43 za sekondari zimeshajengwa.”

Akiunga mkono hoja hiyo, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili l Kirutheri Tanzania (KKKT), Job Kihombo amesema kauli ya kiongozi huyo inapaswa kuungwa mkono na wengine ili kukemea vitendo hivyo.

Mchungaji Kihombo ambaye alisoma na Ndugai Shule ya Sekondari Kibaha, amesema tabia kama hizo zikiachwa, zinaweza kuzalisha kizazi cha malipizi ambayo ni hatari kwa nchi.

“Huyu alikuwa wajina wangu pale Kibaha, amekuwa mtu wa karibu na mimi miaka yote na nikiwa huko mikoani nilikuwa nafuatilia kwa karibu sana siasa zake, sijui kawakosea nini hadi wafanye hayo mambo, siyo jambo jema kabisa,” amesema Mchungaji Kihombo.

Dickson Malayi ambaye alikuwa mfanyakazi katika makazi ya Ndugai, amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimekuwa ghafla sana kuliko walivyotarajia.

Kuhusu baadhi ya watu kushangilia msiba huo, Malayi amesema ni jambo la aibu na fedheha kwa sababi alichokuwa akishuhudia ni jinsi Ndugai alivyokuwa anaishi na watu hasa wenye mahitaji kutoka jimboni Kongwa.

“Kweli hata mimi nimeshangaa, nilitegemea kuona vilio na simanzi lakini nikaoneshwa video eti wanaoshangilia, kweli duniani hapa tenda wema uende zako wala usingoje shukrani, mzee amewasaidia mamia kwa mamia ya wakazi wa hapa Kongwa, sijui nini kimetokea, ila watu hawa hawana utu,” amesema.

Wakati huohuo, Malayi akizungumzia kifo hicho, amesema kimekuwa cha ghafla kwa sababu kwa muda mrefu sasa, hajawahi kumshuhudia Ndugai afya yake ikitetereka.

“Hakuonesha unyonge na hata kwenye kampeni za kugombea ubunge kwa awamu ya sita, bado alikuwa imara na hata kampeni za juzi, hajawahi kusema anaumwa au kuonesha unyonge, alikuwa mzima kabisa, sijui sasa,” amesema Malayi.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Mikalile ya Wanyausi, Clement Ndahani amemtaja Ndugai kuwa alama ya wazawa ambayo haitafutika na kwamba, wangetamani kuwa naye zaidi.

Ndahani amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimewapa maumivu na pengo ambalo halitazibika, ikizingatiwa alikuwa mtu anayependa kuhimiza elimu.

Akizungumzia msiba wa Ndugai, mkuu wa Wilaya ya Kongwa amesema umekuwa wa ghafla na umesababisha simanzi kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Mayeka amesema anakumbuka karibu wiki nzima Ndugai alikuwa kwenye shughuli zake za kisiasa za mchakato wa kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM) na alionekana akiwa na afya njema.

“Maisha ya binadamu yako mikononi mwa Mungu, kwa hiyo hatuwezi kuhoji sana,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Ameeleza jinsi mbunge huyo wa pili katika Jimbo la Kongwa ambaye ameongoza kwa miaka 25 na kusema yeye na wananchi wamepata simanzi kubwa.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Jawadu Mohammed amesema chama hicho kimepoteza mtu aliyetegemewa kwa busara, hekima, maarifa na namna alivyojitoa kwa chama chake.

Amesema kwa kifupi, CCM mkoani Dodoma imepoteza maktaba yake.

Jawadu ameiambia Mwananchi kuwa, Ndugai alikuwa mtu asiye na usaliti na pale inapohitajika maarifa makubwa kwa jambo linalohusu chama, alikuwa anajitoa.           

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema moja ya mambo atakayomkumbuka Ndugai ni namna alivyokuwa na misimamo.

“Mimi binafsi nitamkumbuka mheshimiwa Ndugai kwa misimamo yake, nilifanya kazi chini yake na alikuwa akisimamia jambo hawezi kurudi nyuma, hilo nalikumbuka sana na tuendelee kumwombea kwa mema mengi.”

Dk Tulia aliyekuwapo nyumbani kwa Ndugai Mtaa wa Njedengwa ametoa ratiba ya mazishi akisema Jumapili mwili wa Ndugai utapelekwa viwanja vya Bunge, baada ya hapo mwili utasafirishwa kwenda Kongwa ambako wananchi watamuaga.

Amesema Jumatatu, Agosti 11, 2025 mwili wa Ndugai utapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.

Ndugai ambaye ni spika mstaafu alifariki dunia jana Jumatano, Agosti 6, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika moja ya hospitali jijini Dodoma.

Taarifa Dk Tulia inaeleza kuwa: “Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na spika mstaafu wa Bunge, Job Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma.”

Mchana wa leo makatapila mawili yalikuwa yakichonga kipande cha barabara kutoka njia Kuu ya UDOM – Ihumwa katika mchepuko wa kuingia nyumbani kwa Ndugai  kisha wakamwaga maji.

Mahali walipokaa waandishi wa habari imekuwa vigumu kutambua nani anaingia kwa kuwa, wengi wanaingia moja kwa moja na magari hadi ndani.

Utaratibu wa mahali penye msiba uliowekwa ni waandishi kutoingia ndani kwa kuwa, msiba ni wa kitaifa, hivyo ilibidi kusubiri utaratibu wa Serikali katika kupanga ratiba.

Magari ya viongozi yaliyoonekana ni ya wakuu wa mikoa ya Singida na Dodoma yaliyotambuliwa kwa maandishi ya vibao vya usajili.

Wabunge waliomaliza muda wao ambao wameoneka eneo la msibani ni Dk Pius Chaya aliyekuwa mbunge wa Manyoni Mashariki na mbunge wa kuteuliwa Bashiru Kakurwa.

Waziri wa Utumishi George Simbachawene alifika msibani hapo saa 12.10 jioni na kuzungumza kifupi na vyombo vya habari akisema  walikuwa marafiki na waligombea pamoja ubunge mwaka 2000 ingawa yeye (Simbachawene) hakushinda hadi aliporudi tena 2005.