Dar es Salaam. Ni nini hatima ya wabunge zaidi ya 50 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliomaliza muda wao bungeni, lakini hawakufanikiwa kuibuka kidedea kwenye mchakato wa kura za maoni? Je, ndoto zao za kisiasa zimezimwa rasmi au bado kuna dirisha dogo la matumaini?
Swali hilo linawahusu pia wabunge kama hao, lakini majina yao si sehemu ya yaliyoteuliwa na Kamati Kuu kuingia katika mchujo wa kura za maoni, kadhalika wale walioshindwa kwenye viti maalumu.
Maswali hayo yanajenga msingi wa mitazamo ya wachambuzi wa siasa wanaotabiri kuwa kati ya kundi hilo la wanasiasa waliohudumu katika Bunge la 12, wapo watakaohama vyama, watakaosubiri teuzi na wengine hawatasikika kabisa.
Angalau walioshindwa kuongoza kwa kura za maoni bado wana matumaini ya huruma ya vikao vya kitaifa vya chama hicho kuwateua kuwa wagombea wa ubunge, kama ilivyowahi kufanyika mara kadhaa, ingawa kuna mstari mwembamba kwa hilo kutokea.
Lakini wale ambao majina yao hayakuingia hata hatua ya kura za maoni, zaidi ya 40 nafasi pekee waliyonayo kwenda bungeni ni kupitia nafasi 10 za uteuzi wa ubunge wa Taifa kwa utashi wa Rais.
Kati ya walioshindwa kuongoza kwa kura za maoni, wapo manaibu mawaziri wanane ambao ni Geoffey Pinda (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Exaud Kigahe (Viwanda na Biashara), Danstan Kitandula (Maliasili na Utalii), Jumanne Sagini (Katiba na Sheria) na Stanslaus Nyongo (Mipango na Uwekezaji).
Wengine ni Alexander Mnyeti (Mifugo na Uvuvi), Khamis Hamza Chilo (Muungano na Mazingira) na Cosato Chumi (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Katikati ya yote hayo, wapo walioonesha nia ya kukatia rufaa matokeo ya kura za maoni, wakilalamikia kuchezewa rafu, zikiwemo za madai ya rushwa kutolewa kwa wajumbe.
Tafakuri hizo zinakuja wakati ambao CCM inaendelea na vikao vilivyoanza Agosti 5, kutafakari na kupendekeza watiania wa udiwani, uwakilishi na ubunge waliopigiwa kura za maoni Agosti 4.
Vikao hivyo ni kuanzia ngazi ya kata, wadi, majimbo, wilaya, mikoa na hatimaye Halmashauri Kuu (NEC) Agosti 22, 2025 kwa ajili ya uteuzi wa mwisho wa wagombea.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Philemon Mtoi amesema kutokana na matokeo hayo, wapo baadhi ya wabunge watakaoshuhudiwa wakiihama CCM kwenda vyama vingine.
Lakini amesema, hamahama hiyo haitashuhudiwa ndani ya wiki mbili ambazo CCM inaendelea na vikao vya uteuzi wa mwisho, kwa sababu bado kuna wanaoamini watateuliwa licha ya kushindwa kuongoza kura.
Mtoi ameeleza kuwa wabunge hao wa zamani watashuhudiwa wakihama na kufanya uamuzi mbalimbali, hasa baada ya vikao vya uteuzi wa mwisho na iwapo watajiona si sehemu ya walioteuliwa kugombea.
“Hawatahama ndani ya wiki mbili hizi kwa sababu Katiba ya CCM inazungumza wazi kuwa mchakato wa kura za maoni si uamuzi wa mwisho. Kuna historia ya kwamba ameongoza mwingine kwa kura, lakini ameteuliwa mwingine kugombea, kwa hiyo watu wana matumaini,” amesema.
Ukiacha wanaofikiria kuhama chama, amesema watakuwepo pia watakaosubiri fursa zitakazotoka serikalini kwa maana ya uteuzi wa nafasi mbalimbali, kwa sababu wana uhakika wa kujulikana kutokana na majina yao kujadiliwa ngazi mbalimbali.
Katika nyakati kama hizo, amesema si ajabu kushuhudia watakaojitokeza kushutumu mchakato wa chama husika, yote ni matokeo ya kushindwa kufurukuta katika kura za maoni.
“Utashangaa wataibuka watakaosema ovyo kuhusu chama chao, wapo watakaokaa kimya kuwa wanyenyekevu, wengine watajitegesha kusubiri uteuzi,” ameongeza.
Hata hivyo, Mtoi amesema kundi la walioshindwa kuongoza katika kura za maoni, wengi walishakuwa kwenye mifumo ya Serikali na chama hicho, na baadhi yao kulikuwa na dalili za kilichowatokea.
“Chama kama CCM kinapomhitaji mtu kina mifumo yake ya kumfanya huyo mtu apite huko chini,” amesema.
Amesema hata kiongozi yeyote anayetaka kushika dola, mara nyingi hutengeneza uwanda mpana wa wabunge ambao hatapata tabu iwapo atahitaji kuunda baraza la mawaziri.
“Kuna wakati ilimpa shida (Rais Samia) kuwateua watu wawe wabunge wa kuteuliwa kwanza ndiyo awape nafasi ya uwaziri, hiyo ni kwa sababu waliokuwepo hakuwaona kuwa wanastahili nafasi husika,” amesema.
Ameeleza wabunge wengi walioshindwa kuongoza katika kura za maoni ni kwa sababu wamekosa mvuto dhidi ya walioshindana nao katika majimbo mbalimbali.
“Watu wanataka mtu anayeweza kutetea hoja na kusimamia maslahi ya wananchi. Kuna watu wamekuwa wabunge wakauzoea ubunge, lazima waangushwe,” amesema.
Kwa upande wa mchambuzi wa masuala ya siasa, Said Msonga amesema kukihama chama hicho ni suala linalopaswa kutarajiwa, hasa ukizingatia tayari kuna waliofanya hivyo baada ya majina yao kukatwa mapema.
Hata hivyo, ameeleza si ajabu na ni haki ya mwanachama husika, kama ana nia ya kugombea nafasi na ameshindwa kupitia jukwaa alilopo, basi atatafuta lingine kutimiza malengo yake.
“Kwa sababu imeshatokea kwa mmoja wa watiania kuhama chama, basi itarajiwe kushuhudiwa kwa wengine wengi hasa wabunge watakaoshindwa katika kura za maoni,” ameeleza.
Ingawa kwa mtu aliyekuwa madarakani hasa katika nafasi nyeti, amesema kushindwa uchaguzi sio kushindwa kila kitu, wanapaswa wavumilie na kubaki kwenye vyama vyao.
Amesema wapo walioshindwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 lakini sasa wamejitokeza na kuongoza katika kura za maoni, kwa sababu hawakukata tamaa.
“Badala ya kuhama chama, ni vema hata ukasubiri, kwa sababu ukihama na ukashindwa huko, utapoteza zaidi,” amesema Msonga.
Kuhusu vikao vya uteuzi, Msonga amesema anaamini vitaheshimu uamuzi wa wajumbe katika ngazi za chini kwa sababu ndio wanaowajua wagombea, udhaifu na mazuri yao.
Amesema vikao vitakuwa na nafasi ya kubadilisha iwapo kuna mazingira ya ukiukwaji wa taratibu katika kupata ushindi wa kura za maoni, yaliyothibitika.
Kinyume na hivyo, amesema kuwanyima nafasi walioongoza kwa kura za maoni na kuwapitisha wengine italeta mtafaruku ndani ya chama husika.
“Nyakati zimebadilika sana, zamani chama kikiamua watu walisema chama kimeamua, lakini siku hizi uamuzi wowote unahojiwa na wananchi. Kwa hiyo CCM iwe makini,” amesema.
Walioongoza kwa haki, amesema wanapaswa kupewa nafasi kwa sababu ndio pendekezo la wajumbe ambao kimsingi wanawajua na wanawahitaji.
Kabla ya kauli hizo za wachambuzi wa siasa, tayari aliyekuwa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amehamia ACT-Wazalendo wiki moja baada ya jina lake kukatwa kwenye mchujo wa watiania wa CCM.
Mpina ametangazwa kuwa mwanachama mpya wa chama hicho cha upinzani na ndiye aliyepitishwa na mkutano mkuu kuwa mgombea wa urais, atakayeshindana na wagombea wa vyama vingine, akiwemo wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.
Ukiacha Mpina, suala la kuenguliwa kwa wagombea na kuvihama vyama vyao limeshuhudiwa hata katika mchakato wa ndani wa CCM kumpitisha mgombea urais mwaka 2015.
Katika mchakato huo, Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Lowassa alikihama chama chake na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kisha kupewa ridhaa ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuungwa mkono na vyama shirika vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (CUF, NLD, NCCR-Mageuzi na Chadema wenyewe).
Kama hiyo haitoshi, katika uchaguzi wa mwaka 2020, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, hayati Bernard Membe alijiunga na ACT-Wazalendo na kuwania urais, na baadaye chama hicho kilitangaza kumuunga mkono mgombea wa Chadema, Tundu Lissu.