KIKAO kizito kinachotarajia kufanyika ndani ya wiki hii kati ya uongozi wa JKU Zanzibar na JKT Tanzania, kitahusu kinachoendelea kwa kipa Yakoub Suleiman kuhusishwa kutakiwa na Klabu ya Simba iliyopo jijini Ismailia, Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Mwanaspoti lina taarifa kutoka chanzo cha ndani kilichodai kwamba wachezaji askari wanapotoka Zanzibar kuja kucheza Bara kuna utaratibu unaowekwa kwa maslahi mapana ya waajiri wake na mhusika.
“Yakoub wakati anajiunga na JKT Tanzania ilikuwa ni bure kwa makubaliano ya kiofisi. Baada ya kuonyesha kiwango chake msimu uliopita Yanga na Simba zilitamani huduma yake.
“Utaratibu upo hivi JKT Tanzania hairuhusiwi kumuuza Yakoub bila makubaliano na JKU ambayo itatoa uamuzi wake, kwa sababu mchezaji anapotakiwa kurejea kufanya majukumu yake ya kiaskari anatakiwa kuwa tayari wakati wowote,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kikao hicho kitatoa mwelekeo wa kipi kitaamuliwa kuhusiana na kinachoendelea kwa sasa. Endapo hitimisho itakuwa aende Simba, basi JKU na JKT Tanzania pesa atakayouzwa mchezaji itagawanywa kati kwa kati pia itazingatiwa maslahi mapana ya mchezaji.”
Chanzo hicho kilisema Simba ilitajiwa Sh200 milioni ili inunue mkataba wa miaka miwili ya Yakoub na si miwili na nusu kama inavyoelezwa, lakini klabu hiyo iliomba kupunguziwa dau na mazungumzo yanaendelea kufanyika.
“Simba iliwaambia viongozi wa JKT Tanzania endapo kama wakiwapunguzia itawapa na kipa Ally Salim kwa mkopo ili awe mbadala wa Yakoub ambaye wanaona atakuwa chachu ya kuibua ushindani dhidi ya kipa wa kigeni Moussa Camara, kinara wa clean sheet 19 msimu uliopita,” kilisema chanzo hicho na kusisitiza kuwa:
“Ingawa kwa sasa itakuwa ngumu kwa Salim kujiunga na JKT Tanzania kwa sababu tayari kasajiliwa kipa ambaye msimu uliopita alikuwa na Kagera Sugar, Ramadhani Chalamanda anayetazamwa kama mbadala wa Yakoub.”