Kocha Simba apata chimbo Ghana

ALIYEKUWA kocha wa Simba Queens, Yussif Basigi ametambulishwa kwenye kikosi cha Police Ladies ya Ghana kuiongoza timu hiyo kwenye michuano ya WAFU kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake.

Kocha huyo raia wa Ghana alihudumu Simba msimu mmoja akitokea Hasaacas Ladies ya nchini kwao, lakini hakufanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi ya Wanawake akiushuhudia ukienda kwa JKT Queens.

Akizungumza na Mwanaspoti, Basigi alisema anahudumu kama kaimu kocha mkuu baada ya kocha wa timu hiyo kukosa leseni inayohitajika na CAF kwenye mashindano ya kimataifa.

“Ni mkataba wa muda tu kuwasaidia kwenye mashindano ya kimataifa na nitashirikiana na kocha mwenzangu Abu Kassim ambaye ana leseni B. Ila kwa sasa nakaimu tu, labda kwa baadaye kama watataka niongoze rasmi,” alisema Basigi.

Kassim ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu hiyo akiiongoza kubeba taji la kwanza la ligi ya Ghana, atahudumu kama kocha msaidizi.

Basigi ni mzoefu kwenye mashindano hayo kwani mwaka 2021 akiwa na Hasaacas aliipeleka fainali ya kwanza ya CAF.

Ukanda wa WAFU, mashindano hayo yatashirikisha timu za Bayelsa Queens kutoka Nigeria, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, AS GNN (Niger), USFA (Burkina Faso), ASKO (Togo), Police Ladies (Ghana) na Sam Nelly (Benin).