Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwapatia fursa ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kilometa 20 makandarasi wanawake mkoani Songwe mradi huo unaweza kusema umekuwa kama jicho la kutazama utendaji wao katika kupata fursa nyingi zaidi.
Hatua hiyo inafuatia baada ya mipango ya Serikali ya muda mrefu ya kuwainua makandarasi wanawake katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya nchi pamoja na kushindana na kampuni nyingie pale fursa zinapotangazwa kupitia zabuni.
Hata hivyo, mara kwa mara Serikali imekuwa ikisema ipo tayari kushirikiana na Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA) pamoja na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) ili kuhakikisha kundi hilo linapata nafasi wanayostahili, hususan kwenye miradi mikubwa inayoweza kuchangia kujenga uwezo wao kiuchumi.

Akizungumza Mhandisi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Aloyce Matei leo Alhamisi Agosti 7, 2025 kwenye Sherehe ya kuadhimisha miaka mitano ya TWCA, amesema mradi huo utakuwa ni pazia la fursa zaidi kwa wanawake katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa huku akiwataka kutenda kwa wakati, ubora na ufanisi.
Matei ambaye amemuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mhandisi Aisha Amour, amesema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikitumia makandarasi wageni hasa Wachina huku wizara hiyo ikajitafakari hali hiyo hadi lini!
Akitaja changamoto zilizosababisha wazawa kushindwa kushindana na wageni amesema vigezo, masharti na vipengele vingi, mitaji ya kifedha ilikuwa ikiwashinda wazawa.
“Tukaona tuweke mipango ya kwenda na makandarasi wazawa kwa kuwajengea uwezo ili ifikie mahali tuanze kuwatumia na katika hilo ikaja hoja ya kuwafikiriia makandarasi wazawa wanawake kuwapa upendeleo.
“Tuwajengee uwezo kisha tuwashindanishe wao wanawake wenyewe ili waweze kushindana na kampuni nyingine za wanaume na zile za kigeni. Sasa wakapewa mradi wa kuanzia wa kilometa 20 huko mkoani Songwe. Waliopata wawe kama mfano kwa wengine sasa wakifanya vibaya wataharibia wenzao,” amebainisha.
Akieleza zaidi amesema anaamini wanawake wanaweza kutekeleza mradi huo ambao utakuwa mwanzo wa kupata miradi mingi zaidi huku akitaka kufanya kwa ufanisi.
“Mkafanye kwa ubora na uaminifu mkubwa ili kufungua fursa kwa wanawake wengi zaidi, mkishindwa itakuwa pigo kuwa katika ajenda hii ya kukuza makandarasi wanawake” amesisitiza.
Hata hivyo, hayo yanajiri wakati Serikali ikibadilisha sheria ya manunuzi ambapo kwa sasa makandarasi wazawa wanaweza kufanya miradi ya Sh50 bilioni kutoka Sh10 bilioni iliyokuwa awali.
Akiielezea Mwananchi mradi huo wa mkoani Songwe, Katibu wa TWCA, Debora Sengati amesema kampuni za wanawake zimeungana zimekuwa 12 ambazo zitatekeleza mradi huo wa kilometa 20.
“Mradi huo wa lami inathamani Sh55 bilioni tumesaini ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu uhuru wanawake kufanya mradi wa lami. Tutapelekwa saiti kuoneshwa hizo kilometa 20 tumegawana kilometa 5 kwa kila kampuni.
“Tunatambua tumetolewa kama mfano ili kuona wanawake wanaweza. Tunaimani tutatekeleza vizuri ili kufungua milango mingine zaidi,” amesema Katibu huyo.
Hata hivyo, mhandisi Matei akisema hotuba ya Katibu Mkuu Ujenzi amesema, Serikali inachotaka ni kuwawezesha na kuwaamini wanawake wazawa wakue ili washindane na yeyote yule pale itakapotokea fursa ya kazi.
Akielezea fursa hiyo, Mkandarasi Flora Makota amesema watatekeleza kwa ufanisi huku akiwaasa waliopata tenda hiyo wasimamie vizuri kikamilifu na kwa wakati ili kuwa pazia kwa wengine.
Naye, Mkandarasi Kuluthum Sagamiko amesema wanawake wanauthubutu na uoga wa kuharibu hivyo watafanya kazi kwa uaminifu. Anaamini fursa hizo walizopewa watafanya kwa uaminifu.
“Changamoto ilikuwa mitaji na tulikuwa hatuna ulinzi, sasa benki zinatuamini, tunaenda vizuri, na miradi itaenda kukamilika kwa asilimia 100,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TWCA, Profesa John Bura amewaonya TWCA kuwa waangalifu kutekeleza kazi wanazozipata aidha, amewashauri kufanya kazi kwa pamoja.
Hata hivyo, katika sherehe hiyo ya miaka mitano ya TWCA iliofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mbali na mengine umefanyika uchaguzi wa uongozi mpya utakaohudumu kwa muda wa mika mingine mitano.
Katika uchaguzi huo rais wa sasa, Judith Odunga anayejivunia kuaminiwa kwa makandarasi wanawake akitolea mfano Mkoa wa Tabora kuwa na miradi ya wanawake ikiwemo barabara madaraja amechaguliwa tena kuendeleza miaka mingine mitano.
Aidha, wamechaguliwa wenyeviti na makatibu wa kanda mbalimbali kaskazini, Mashariki na Pwani, Kati, Kusini, amechaguliwa Katibu Mtendaji Katibu Mkuu.