Mayele anukia Mtibwa Sugar | Mwanaspoti

MABINGWA wa zamani w Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar wanakaribia kuipata saini ya mshambuliaji wa TMA ya Arusha, Kassim Shaibu ‘Mayele’, baada ya nyota huyo kufanya mazungumzo na timu hiyo, ambayo hadi sasa yanaendelea vizuri ili kukitumikia kikosi hicho msimu ujao.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Shaibu amekubaliana maslahi binafsi ya kujiunga na Mtibwa Sugar kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho, licha ya mabosi wa TMA kumwekea mkataba mpya ili kuipigania pia timu hiyo ya Ligi ya Championship.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shaibu aliyefunga mabao sita msimu wa 2024-2025 katika Ligi ya Championship akiwa na TMA, alisema hadi sasa kuna baadhi ya timu ambazo zimeonyesha nia ya kumuhitaji, ingawa hakuna kilichofikiwa.

“Nafikiri tusubiri baada ya muda sio mrefu tunaweza kukamilisha mazungumzo na moja ya timu, siwezi kutaja ni ya Ligi Kuu Bara au ya Championship, kwa sababu ninachozingatia ni maslahi yangu tu binafsi na wala sio vinginevyo,” alisema Shaibu.

Nyota huyo amejiunga na TMA msimu wa 2024-2025, akitokea KenGold aliyoipandisha Ligi Kuu Bara kisha kushuka msimu huu wa 2024-2025, ambapo aliifungia mabao tisa ya Ligi ya Championship, huku akiwahi kuwatumikia pia maafande wa Green Warriors.

Pia, ameichezea Mbeya Kwanza huku chimbuko la jina hilo alipewa akiichezea Lumo Combine ya Buza jijini Dar es Salaam, wakati wa ‘Ndondo Cup’ kutokana na upambanaji wake akifananishwa na nyota wa zamani wa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele aliyepo Pyramids ya Misri.

Mtibwa iliyoshuka daraja 2023-2024, imerejea tena Ligi Kuu ikiwa ndio mabingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza kinara kwa pointi zake 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea pia kufuatia kushuka daraja msimu wa 2022-2023.

Mtibwa Sugar ndio timu pekee nje ya Simba na Yanga kuweza kutetea taji la Ligi ya Bara ikifanya hivyo ilivyotwaa mataji misimu miwili mfululizo 1999 na 2000.