BAADA ya Simba Queens kumrejesha mshambuliaji Mkenya Jentrix Shikangwa inaelezwa viongozi huenda wakavunja mkataba wa Magnifique Umutesiwase raia wa Rwanda.
Hadi sasa Simba imesajili wachezaji sita wa kigeni ambao ni Zainah Nadende (Uganda), Ruth Aturo (Uganda), Zawadi Usanase (Rwanda), Cynthia Musungu (Kenya), Fasila Adhiambo (Kenya) na Magnifique Umutesiwase.
Na wale waliokuwepo msimu uliopita ni Winifrida Cedar, Shikangwa, Vivian Corazone, Elizabeth Wambui na Ruth Ingosi ikiwa na jumla ya nyota 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa viongozi wa timu hiyo (jina tunalo) alisema wataongeza wachezaji wawili wa kigeni eneo la beki wa kati, hivyo wanaangalia uwezekano wa kumtoa mshambuliaji mmoja ili kuziba nafasi ya mabeki hao. “Katika eneo la ushambuliaji lina wachezaji wengi, watatu wa kigeni wapo, pia wazawa wengi kwenye eneo hilo, na bado tunauhitaji wa mabeki wa kati wawili,” alisema kiongozi huyo.
“Sasa kama itashindikana kuvunja mkataba, tutaangalia namna ya kumtoa kwa system hadi dirisha dogo. Tutaangalia uwezekano wa nani atolewe kisha tumuingize.” Msimu uliopita Simba Queens ilipoteza taji la Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kwa kuzidiwa ujanja na JKT Queens na kuzifanya timu hizo kulingana zikitwaa mataji mara nne kila moja tangu michuano hiyo ianze 2016