Mkurugenzi wa Wizara Apongeza TFS kwa Kuendeleza Shughuli za Uhifadhi na Kutoa Elimu kwa Umma NaneNane 2025

Dodoma. Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ndg. Bernard Marcelline, amepongeza juhudi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa namna unavyoshiriki kikamilifu katika Maonesho ya NaneNane 2025, hususan katika kutoa elimu kwa wananchi na kuonesha shughuli mbalimbali za uhifadhi wa misitu na nyuki zinazotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza leo Agosti 8, 2025, alipotembelea banda la TFS katika Viwanja vya Maonesho ya NaneNane, Nzuguni Dodoma, Marcelline alisema kuwa TFS imeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa namna inavyowasiliana na wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na nyuki.

“Nawapongeza wahifadhi kwa kujitoa kwao kutoa huduma bora kwa wananchi. Banda la TFS limekuwa kivutio kwa wengi kutokana na taarifa, elimu na maonesho yanayowahusu uhifadhi, utalii wa ikolojia, urithi wa malikale na fursa mbalimbali za mazao ya misitu na nyuki,” alisema Marcelline.

Alieleza kuwa amejionea shughuli nyingi muhimu zinazotekelezwa na Wakala, ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu mazao yatokanayo na misitu, upatikanaji wa mbegu bora za miti na miche, pamoja na mafunzo ya ufugaji nyuki kuanzia maandalizi ya manzuki hadi uvunaji na uchakataji wa mazao ya nyuki.

Pia alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuhamasishwa zaidi kutumia fursa zinazotolewa na TFS katika maeneo ya hifadhi ili kuongeza kipato kupitia biashara ya mazao ya misitu na huduma za utalii wa ikolojia.

Aidha, alihimiza wataalamu wa TFS kuendelea kubuni njia mpya za utoaji wa huduma kwa wananchi, kwa kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na inavutia makundi mbalimbali ya jamii kushiriki katika uhifadhi na uwekezaji ndani ya maeneo ya misitu.

“TFS inapaswa kuendelea kuwa wabunifu zaidi, ili kuwavutia wawekezaji na wananchi wengi zaidi kushiriki katika uhifadhi wa misitu, jambo ambalo litasaidia kuongeza vyanzo vya mapato na kulinda urithi wa taifa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisisitiza.

Maonesho ya NaneNane yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuonesha kazi na huduma wanazozitoa. TFS imeendelea kutumia maonesho haya kama fursa ya kufikisha ujumbe kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu na nyuki katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Kumbuka: TFS inashiriki katika maonesho ya NaneNane katika kanda zote nchini. Wananchi wanahimizwa kutembelea mabanda ya TFS ili kupata elimu, kuona bidhaa mbalimbali zinazotokana na misitu, dawa za asili, miche bora ya miti na kujifunza fursa zilizopo kwenye sekta ya misitu na nyuki.