MKUTANO MKUU CHAUMMA: Wito amani Uchaguzi Mkuu watawala

Dar es Salaam. Wito wa kulinda amani wakati wa uchaguzi umetawala salamu za viongozi mbalimbali wa kisiasa na wadau wa demokrasia waliohudhuria mkutano mkuu wa Taifa wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) unaoendelea leo, Alhamisi Agosti 7, kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Wadau wametoa kauli hizo katika mkutano mkuu ambao chama hicho kinatarajiwa kutangaza wagombea wake wa nafasi ya urais kwa Tanzania  bara na Zanzibar.

Ramadhan Abdallah, Mwakilishi kutoka chama cha ADC, licha ya kumpongeza Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe kwa hatua kubwa ya kujenga chama, amesisitiza amani wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.

“Hakika nikupongeze Mheshimiwa Rungwe kwa juhudi za ujenzi wa chama hiki. Niwapongeze sana kwa hatua mlizofikia. Lakini niwasisitize twendeni kwenye uchaguzi tukazingatie amani ya nchi yetu,” amesema.

Akizungumza kwa msisitizo zaidi kuhusu hadhi ya mkutano huo, Kosta Kibonde, Mwenyekiti wa Chama Makini ambaye pia ni mgombea urais wa chama hicho, amesema; “Nawapongeza kwa maandalizi makubwa, ni mkutano wa kihistoria. Chaumma ninayoijua si Chaumma ninayoiona hapa leo. Hakika kazi mliyoifanya ni ya kizalendo.

“Twendeni tukaombe kura, lakini mkatangulize mbele amani ya nchi yetu.”

Majaliwa Kyala kutoka Chama cha SAU, amesisitiza umuhimu wa kutatua matatizo ndani ya vyama ili kuimarisha taasisi za kisiasa.

“Tusipotatua matatizo yatatuongoza na kusambaratisha taasisi zetu,” amesema na kusisitiza matatizo yanatakiwa kutatuliwa kwa amani ili chama kiendelee kukua.

Naye Embros Mchome, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, amewakumbusha washiriki wa uchaguzi wajibu waliobeba katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa Taifa.

“Nendeni mkaangalize masilahi ya umma, mkawakomboe Watanzania na nitawaunga mkono katika kampeni zenu,” amesisitiza.

Salamu zenye kugusa hisia pia zimetolewa na Anna Ngalawa, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vijana kutoka Chama cha Wenye Ulemavu ambapo ametoa wito kwa vyama vya siasa kuhakikisha vinadumisha amani wakati wa uchaguzi, kwani machafuko huwaumiza zaidi watu wenye ulemavu pindi yanapotokea.

“Machafuko yakitokea ni watu wenye ulemavu ndio hupata taabu. Tunawaomba wanasiasa mkazingatie suala la amani ya nchi yetu.”

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Maduhu William ameweka bayana matarajio ya asasi za haki za binadamu akisisitiza amani, utawala wa sheria na kukomesha ukandamizaji katika jamii.

“Msilete mgombea ambaye hatazungumza suala la amani kwa vitendo. Katumieni muda wa uchaguzi kuuza ilani ya Chaumma, msitukane watu majukwaani,” amesisitiza.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, ametilia mkazo suala la amani wakati wa uchaguzi, akisisitiza vyama vya siasa kuzingatia sheria na katiba za vyama vyao katika michakato ya ndani ya vyama.

“Chaumma hii siyo ile. Hongereni sana. Katika ushindani, zingatieni sheria za chama chenu na za nchi, mlinde amani ya nchi yetu,” amesema.

Leo, Chaumma kinahitimisha vikao vyake na kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali zinazowaniwa, ikiwa ni siku chache kuelekea ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Endelea kufuatilia Mwananchi