Mkwasa ataka mabao zaidi CHAN

KOCHA wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Boniface Mkwasa amesema benchi la ufundi la timu ya taifa lina kazi kubwa ya kufanya kwa kuhakikisha washambuliaji wanatumia nafasi wanazotengeneza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika mechi zao za fainali za CHAN 2024.

Mkwasa amefunguka hayo baada ya Stars kuandika rekodi ya kuongoza kundi ikishinda mechi mbili mfululizo kwenye michuano ya CHAN baada ya juzi kuikanda bao 1-0 Mauritania.

Stars ilianza michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza ikiandaliwa na nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kwa kuifunga Burkina Faso mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi wa fainali hizo za nane.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkwasa alisema furaha ni kubwa sana kwa rekodi iliyoandikwa lakini benchi la ufundi likiongozwa na Hemed Morocco linatakiwa kufanyia kazi dosari zilizopo eneo la ushambuliaji ili kuweza kufikia malengo.

“Ni jitihada kubwa za wachezaji kufikia rekodi iliyoandikwa hadi sasa, lakini tuna maeneo tunakwama kama kurudisha sana mipira nyuma, pia kushindwa kutumia nafasi zinazotengenezwa hili ni tatizo kubwa,” alisema nyota huyo wa zamani wa kimataifa aliyeshiriki Afcon 1980 aliyeongeza;

“Ili uweze kuwa bora ni kupata matokeo na pia kufunga mabao mengi kulingana na nafasi zinazotengenezwa. Tuna washambuliaji wazuri waelekezwe ili waweze kutumia nafasi kwani kuonekana mnamiliki mpira kwa kucheza eneo lenu sio salama.”

Mkwasa alilipongeza benchi la ufundi kwa kuongoza kikosi kufanya kitu kikubwa ambacho kitaendelea kubaki kwenye kumbukumbu huku akisisitiza kuwa nafasi bado ipo kufikia malengo muhimu zaidi ni kutumika kwa nafasi.

Alisema juhudi za wachezaji na mashabiki ambao wanajitokeza kuwapa nguvu ni sehemu ya mafanikio kutokana na kukosoa wachezaji ambao pia wanajirekebisha na kufanya vitu vikubwa ambavyo vimeleta tija na ushindi.