Nalirudia tena hili maana linauma na kusikitisha sana. Hivi karibuni wabunge walio wawakilishi wa wananchi, akiwamo mstaafu, wamemaliza kipindi chao cha kupokea mshahara wa Sh14 milioni kwa mwezi kwa miaka mitano, kwenye nchi hii inayodai kuwa ni masikini, japo wa kujitakia!
Kwa kazi ngumu yao ya kuunga mkono hoja na kupiga makofi kushangilia hoja, badala ya kupiga makofi wale ‘vibaka’ ambao CAG anatuambia kila mwaka kuwa, hela za tozo tunazolipa zinaishia kwenye mifuko yao na sio kwenye mifuko inayohusika, lakini bado wanatesa kwenye ajira bila kuchuliwa hatua yoyote!
Ndio, ‘wastaafu’ hawa baada ya kazi ngumu ya miaka mitano wamelipwa kiinua mgongo kweli cha Sh400 milioni wakati mstaafu wa kweli aliyefanya kazi ya kweli ya kuijenga nchi hii kwa miaka 40 ameishia kulipwa ‘kipindisha mgongo’ cha Sh30 milioni tu na hakuna mtu yeyote aliyeupiga mwingi kwake!
Yaani ‘ajira’ ya miaka mitano tu, mtu analipwa kiinua mgongo cha Sh400 milioni huku yule wa ajira ya miaka 40 anapewa ‘kipindisha mgongo’ cha Sh30 milioni tu.
Anayesema ‘binadamu wote ni sawa’ tafadhali awasiliane na bakora yangu watete kidogo!
Kibubu ambacho kimetunza akiba ya mstaafu kwa miaka 40 na kukifanyia biashara ya akiba hiyo bila hata kumuambia mstaafu mwenye hela zake, kimeishia kumpa pensheni aliyokatwa kwenye kijimshahara chake. Watu wanaposema wametoka mbali na nchi hii muelewe.
Kibubu cha akiba yao wastaafu, kimefanya mambo mengi mema lakini hakijamkumbuka mstaafu mwenye hela zake hata jambo moja dogo tu. Ndio, wanaitumia kwa mambo mengi ikiwamo kujenga maghorofa na madaraja lakini sio kumjenga mstaafu azeeke vyema kama vile sio yeye aliyeijenga nchi hii kwa jasho na damu yake!
Kibubu kimeshindwa kufanya ubunifu wa kutumia hela ya ghorofa moja walilojenga kutengeneza benki ndogo ya wastaafu ili mstaafu aweze kupata mikopo midogo midogo ya kuwasaidia badala ya kuwaacha wabamizwe na hizi benki zenu za dotcom ambazo mikopo ya wastaafu na ile ya wafanyabiashara zote riba na tozo ni moja!
Kibubu kimefanya jambo moja kwa mstaafu anayekuwa mkazi wa kudumu Kinondoni. Kimesema kuwa kitatoa Sh5 milioni kwa wategemezi wa mstaafu pale anapokuwa tayari ‘ameihahakikiwa’ kuwa kweli ni mkazi wa kudumu wa Kinondoni!
Ni jambo jema, lakini ni bahati mbaya sana mstaafu anapata Sh5 milioni zinazomhusu akiwa tayari marehemu sio akiwa hai ili amalizie
maisha yake kwa amani kwenye nchi hii ambayo sasa inajifanya kuwa hata haikumbuki kwamba yeye ndiye aliyeijenga!
Linaweza likawa jambo jema kwa kibubu na siri-kali kuwapa wategemezi wa mstaafu aliyefariki Sh5 milioni huku kikishindwa kumuongezea pensheni yake ya Sh150,000 kwa miaka 21 wakati unafanyia biashara hela zake!
Ni jambo linalopaswa kuwafikirisha sana wahusika.
Inakuwa ni yale yale ya jamii ya kudai kuwa pengo la marehemu halitazibika wakai kabla hata hajazikwa, tayari ofisi aliyokuwa akifanya kazi kabla ya msiba wake tayari mtu ameishachaguliwa kukalia meza alivyokuwa akiikalia yeye ambaye pengo lake halitazibika!
Kibubu na siri-kali vikae chini na kuweka utaratibu wa kumpa mstaafu Sh5 milioni zake akiwa hai na sio akiwa tayari yupo Kinondoni.
0754 340606 / 0784 340606