Mpina, Othman turufu ya ushindi ACT Wazalendo

Dar es Salaam. Mipango ya Chama cha ACT Wazalendo kuisaka dola imekamilika, baada ya chama hicho kuhitimisha mchakato wa kuwapata wagombea wa urais wa Tanzania na Zanzibar.

Mbunge wa zamani wa Kisesa, Luhaga Mpina ndiye aliyetangazwa kuwa mgombea wa urais wa Tanzania huku Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman naye akapitishwa kugombea nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar.

Kupatikana kwa wagombea hao, kumeenda sambamba na kupitishwa kwa Ilani ya uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025-2030, ikibeba mambo mambo mengi, yakiwemo saba muhimu watakayoyanadi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Kukamilika kwa hatua hiyo, kumechangiwa na ramani aliyoichora Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, aliyekuwa amechukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri awali lakini akalazimika kujiweka kando kutoa nafasi kwa chama kumpata mwanachama mwingine, ambaye kinaona ni turufu ya ushindi.

Hatua hiyo, inakiweka tayari chama hicho kukabiliana na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho tayari kimempitisha Rais Samia Suluhu Hassan kugombea urais wa Tanzania na Dk Hussein Ali Mwinyi kwa upande wa Zanzibar.

Kutokana na hatua hiyo, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ameitaka CCM ijiandae kukabiliana nao, akidokeza kuwa anapokea maombi ya wanasiasa wengi kutoka vyama mbalimbali, kikiwemo chama tawala, wanaotaka kujiunga na chama hicho.

Hayo yameshuhudiwa jijini Dar es Salaam jana usiku katika Mkutano Mkuu Maalumu wa ACT Wazalendo, uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City.

Akitoa salamu za chama hicho katika mkutano huo, Shaibu amesema chama hicho kimekamilisha mchakato wa kuwapata watiania wa udiwani, uwakilishi na ubunge kwa Tanzania Bara na Zanzibar,  hivyo akaitaka CCM ijiandae na kuwa milango ipo wazi ili kuunganisha nguvu ya kuiondoa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Jumatano, Oktoba 29, 2025.

“Njooni tuunganishe nguvu ya kuiondoa CCM madarakani,” amesisitiza Ado.

Mtendaji mkuu huyo wa chama hicho, amewaambia wajumbe wa mkutano huo ACT Wazalendo ina watiania wa udiwani katika kata zote za Tanzania Bara na Zanzibar akisema ndio silaha za kuiondoa CCM madarakani.

“Pia tumeshakamilisha mchakato wa kuwapa watiania ubunge na uwakilishi wa Zanzibar, vivyo hiyo katika majimbo ya Tanzania bara CCM ijiandae,” amesema Ado.

Tukio hilo, liliambatana na uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho mwaka 2025/30. Mwenyekiti wa kamati ya ilani, Emmanuel Mvula amesema endapo ACT Wazalendo ikifanikiwa kushika madaraka itahakikisha inazalisha uchumi wa watu utakaozalisha ajira milioni 12 kupitia viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, biashara, sanaa na huduma za teknolojia.

Mengine ni kujenga taifa lenye haki na demokrasia ili kuondoa rushwa na kujenga Serikali yenye uwazi na uwajibikaji, kulinda na kusimamia ardhi, mazingira na rasilimali kwa maslahi ya wananchi wote.

Kabla ya kuwasilisha muhtasari huo, Mvula amewahakikishia wajumbe wa mkutano huo ilani hiyo ya uchaguzi imebeba maono ya kujenga Tanzania mpya itakayokuwa na maslahi ya wote na manufaa kwa wote.

“Tumejipanga kuhakikisha uchumi unakuwa kwa watu na si takwimu, huduma za jamii zinatekelezwa kwa haki na miundombinu inajengwa kwa maendeleo ya watu si kwa sifa za kisiasa,” ameeleza Mvula.

Amesema endapo ACT Wazalendo ikifanikiwa kushika madaraka itahakikisha inazalisha uchumi wa watu utakaozalisha ajira milioni 12 kupitia viwanda,kilimo,  uvuvi, mifugo, biashara, sanaa na huduma za teknolojia.

“Serikali ya ACT Wazalendo itawezesha kwa kiwango kikubwa maeneo ya uwekezaji na kuwezesha wananchi kiuchumi,” amesema Mvula.

Kuhusu kuboresha huduma za jamii kwa wote, Mvula amesema ilani ya ACT Wazalendo itakuwa na mkakati maalumu wa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji na nishati na hifadhi ya jamii na watawekeza bima ya afya kwa wote.

“Tutatoa huduma za kutosha kwa watumishi wa elimu na kada ya afya.

Amesema ACT Wazalendo imedhamilia kuboresha miundombinu ili kuchochea maendeleo ya uchumi na kijamii kwa kujenga reli ya kisasa ya SGR Kanda ya Kusini sambamba na kujenga barabara za kimkakati.

“Tutapambana na vitendo na ukandamizaji na uonevu dhidi ya vyombo vya dola, polisi itakuwa huduma kwa jamii si badala ya kutumia nguvu dhidi ya wananchi Tutajenga mifumo bora ya haki jinai na ndani ya miezi sita ya kwanza tutafufua mchakato wa Katiba Mpya ya wananchi,” amesema Mvula.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman amesema mkutano huo umetengeza ramani ya kuwapatia Watanzania watu watakaozisemea changamoto zinazowakabili.

“Mkutano mkuu unakwenda kuwapaza sauti za Watanzania ambazo zimezimwa na kuzuia kwa muda mrefu. Mkutano huu unakwenda kutengeneza ramani na miundombinu ya kuwapatia Watanzania watu watakaosemea changamoto zao pale ambapo wamekwama,” amesema.

“Njia ya sauti zao kusikika ni kuweka viongozi wanaowataka na kuwa na uwezo wa kuwawajibisha. Mkuu mkuu huu unakwenda kuwatoa Watanzania huko waliko, naomba tusiwaaungushe wananchi,” amesema Othman.

Ameelezachama hicho kinakwenda kwenye mapambano ambayo silaha ya mwanzo ya mwanajeshi yeyote si bunduki wala mzinga bali nidhamu.

“Niwaombe wajumbe mkutano mkuu kusimamia maslahi ya Watanzania kwa nidhamu ili tufanikiwa. Tumeamua kuwatumikia Watanzania lakini tubaki kwenye nidhamu,” amesema Othman.

Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe amesema kiongozi wa sasa, Dorothy Semu amechora ramani ya mapambano katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Amesema Semu amekisaidia chama na Taifa na miezi mitatu ijayo itakwenda kuzibadili siasa za Tanzania.

“Tunakwenda kwenye miezi mitatu migumu sana, lakini ni miezi mitatu ya kurejesha heshima ya kura na Kiongozi wetu wa chama ametuchorea tunakushukuru sana na Mungu akubariki,” amesema.

“Utakumbukwa kama kiongozi ambaye uliyeweka pembeni matakwa yako, kwa ajili ya matakwa ya Taifa. Mmewaona watiania wa urais Tanzania (Mpina na Aaron Kalikawe) hii ni vita ya kizazi kitakwenda kumaliza kazi niliyoishinda,” amesema Zitto.

Mkutano huo ni wa kwanza kwa Mpina kuhudhuria tangu alipojiunga na chama hicho, juzi akitokea CCM alikokuwa tangu Umoja wa Vijana (UVCCM).

Hatua yake ya kuwasili ukumbini hapo na kuitwa mbele ya wajumbe wa mkutano huo, iliibua shangwe, akishangiliwa kwa karibu wahudhuriaji wote kusimama.

Mpina aliingia ukumbini hapo kimyakimya. Ni wajumbe wachache ndiyo walimuona kupitia luninga iliyopo mbele wakati Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa akizungumza.

Ghafla utulivu ukakosekana, baada ya wanahabari kwenda alikoketi Mpina kwa ajili ya kupata picha, jambo lililomlazimu Katibu Mkuu, Ado Shaibu kuiwahisha ratiba ya utambulisho wa watiania wa urais tofauti na ilivyopangwa hapo awali.

“Kwa vile msajili msaidizi wa vyama vya siasa (Sisty Nyahoza) amekugusia suala la wagombea ngoja niwatambulishe ingawa ratiba yao ilikuwa baadaye. Nawaomba niwaite kabla ya Kiongozi wa chama hajafika kutoa hotuba yake,” amesema Ado.

Baada ya hapo, Ado alianza kumuita Othman kwenda mbele ya jukwaa kuu kuwapungia mkono wajumbe wa mkutano mkuu maalumu.

Alipoitwa ukumbi ulilipuka kwa shangwe na vigeregere kwa mtiania huyo, kisha akafuata mtiania Aaron Kalikawe anayewania naye akashangiliwa. Lakini funga kazi ilikuwa kwa Mpina alipoitwa karibu wajumbe wote walisimama na kumshangilia.

“Sasa hapa naweza kumwita Kiongozi wa chama (Semu) aje kuhutubia maana utulivu kupatikana,” amesema Ado baada ya kuwatambulisha watiania urais hao.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amewapongeza ACT Wazalendo kwa kuendelea kutambua asasi za kiraia kwenye suala la demoksraia na utawala bora.

“ACT Wazalendo walitupa nafasi ya kuwasilisha maoni yetu, tunaamini Ilani itakayozinduliwa leo itabeba yale maono tulioyawasilisha tulipoitwa, ikiwemo Katiba Mpya,” amesema Ole Ngurumwa.

Ole Ngurumwa amesema vyama vya kisiasa ndio mlango pekee wa kutimiza ndoto za Watanzania ili kushiriki nafasi za uongozi kwa ngazi mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Ole Ngurumwa amesema kuelekea uchaguzi kila chama kina mpango mkakati ikiwamo kuja kaulimbiu ‘ Oktoba tunatiki’ kingine Oktoba Linda Kura’ na wengine No reforms, no election’.

“Kikubwa tusibezana kila mtu anayeamini njia yake basi aachwe aamini katika njia yake kwa sababu kila chama nia yake ni kuchukua dola. Chama kinachotaka kuchukua dola vihakikishe vinakuwa pamoja hasa katika ushirikiano,” amesema Ole Ngurumwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (Wildaf), Anna Kulaya amesema, “Tunashukuru kuwa sehemu ya kushiriki mkutano mkuu maalumu tunawapongeza ACT Wazalendo kwa maandalizi mazuri.

“Mmetwambia kuwa watiania wa udiwani hadi ubunge wameshapatikana tunatarajia mtazingatia jinsia katika mchakato wa uteuzi wa watiania hawa,” amesema Kulaya.

Msajili Msadizi wa Vyama vya Siasa, Sity Nyahoza amesema ofisi hiyo inawapongeza ACT Wazalendo, kwa kufanya mkutano mkuu huo ambapo wamekamilisha takwa ambalo ni la kidemokrasia.

Nyahoza aliyemwakilisha Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema jukumu la ofisi yake ni kufuatilia jukumu la kuangalia vyama vya siasa kuhakikisha vinafuata sheria za vyama vya siasa.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi kuna vyama vya siasa, hivyo tunavipongeza na kiviasa vizingatia sheria na kufuata utaratibu uliokwekwa ili kudumisha amani,” amesema Nyahoza.

Kada wa ACT Wazalendo, Muhidin Mkwera amesema Mpina na Othman ni wagombea sahihi na turufu inayoweza kuwavusha katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

“Wataweza kuongeza kura za wabunge hata kushinda urais na kukifanya chama kuvuma zaidi na kujulikana na tofauti na hivi sasa,” amesema.

Kada mwingine, Dk Mohamed Ali Suleiman amesema amesema Mpina ni mtu muhimu na amejipambanua tangu akiwa CCM, na sasa ameamua kuingia ACT Wazalendo.

“Othman na Mpina, hawa watatuvusha salama kutokana na maono yao, kwa ushirikiano wa viongozi wa chama ambao baadhi yao wameshawahi kuwa viongozi wa Serikali kwa nyakati tofauti,” amesema Dk Suleiman.

Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Khadija Anuary Mohamed amesema Othman ndiye mgombea sahihi ACT Wazalendo ili kuendeleza mapambano yaliyoachwa na mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wa Zanzibar.

“Hadi kufikia uamuzi wa kumkabidhi Othman kijiti hiki chama kilitafakari kwa kina hatimaye kumwamini mwenyekiti huyu ili kuendeleza pale alipoishia Maalim Seif,” amesema.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar, Othman amesema uongozi wake utajikita kuifanya Zanzibar yenye haki, usawa na maendeleo kwa wote.

Amesema Zanzibar chini yake itaweka mbele misingi ya uwazi, uwajibikaji na maadili ya uongozi bora, uchumi jumuishi, utalii, viwanda vidogo, uvuvi na biashara ndogondogo.

Ameeleza Serikali yake itaanzisha programu mahsusi ya kuajiri na kuwawezesha vijana na wanawake ili waajirike katika soko la ajira lililopo Zanzibar na kwingineko.

Ameahidi kuanzisha mfuko wa uwezeshaji wa wajasiriamali wa Zanzibar, atafufua viwanda vya ndani ili kuongeza ajira na kipato na kuhamasisha elimu ya ufundi na ujasiriamali.

Jambo lingine aliloahidi ni kupambana na rushwa na ubadhirifu kwa kutangaza vita dhidi ya matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

“Nitaanzisha taasisi imara za uangalizi wa matumizi ya fedha za Serikali, kuongeza ushiriki wa wananchi katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, haki, umoja na maridhianao,” amesema.

Ameahidi kuweka mbele mshikamano wa kitaifa kwa maendeleo endelevu ili kila Mzanzibari popote alipo duniani atumie ujuzi alionao kuijenga Zanzibar mpya.

Othman alizaliwa mwaka 1963 na ana shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuucha London nchini Uingereza. Amewahi kuwa mtumishi wa umma katika nafasi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais anayeshughulikia sheria na baadaye akateuliwa kuwa Katibu Mkuu na Naibu Mwanasheria Mkuu katika Ofisi ya Waziri Kiongozi wa Zanzibar mwaka 1996.

Aliendelea kulamba teuzi nyingine akiwa Katibu Mkuu, Wizara ya Utawala Bora huku akiendelea kuhudumu kama Naibu Mwanasheria Mkuu hadi mwaka 2000.

Ndiye kiongozi aliyesimamia kuanzishwa kwa Ofisi ya Mashtaka visiwani Zanzibar mwaka 2002 na aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Ofisi ya Mashtaka visiwani humo kwa miaka tisa.

Luhaga Mpina (50) aliyekuwa Mbunge wa Kisesa mkoa wa Simiyu alizaliwa 1975 na kupata elimu ya msingi Shule ya Mwandu Itinje, Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu kuanzia 1983 hadi 1989.

Baada ya kuhitimu shule ya msingi, Mpina alijiunga na masomo ya Sekondari Shule ya Meatu 1991 hadi 1994 na hatimaye 1995 hadi 1997 akasoma kidato cha tano na sita.

Mwaka 2000 hadi 2003 Mpina alijiunga na Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro, akisomea shahada ya kwanza katika fani ya uhasibu na usimamizi wa fedha.

Hakuishia hapo, 2009 hadi 2010 alipata shahada ya uzamili ya masuala ya sayansi katika usimamizi wa fedha katika Chuo Kikuu cha Strathclyde University nchini Marekani.

Katika utendaji wake wa kazi, Mpina 1997 hadi 1998 alikuwa mkaguzi mkuu wa kampuni ya S & C Ginning Ltd, Meatu na ofisi ya kanda Maswa.

Mpina akiwa Wilaya ya Meatu akiripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wilaya 1999 hadi 2000 alihudumu kama Ofisa Mtendaji wa kata, 2000 hadi 2003 akawa Kaimu Ofisa Biashara, 2004 hadi 2005 mhasibu daraja ii na mwaka huohuo akawa kaimu ofisa usambazaji.

Ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mpina ameshika nafasi mbalimbali ikiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana UVCCM wilaya ya Meatu 2003 hadi 2008, wakati huohuo alikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM.

Pia Mpina akiwa Meatu aliwahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa UVCCM tangu 2003 hadi 2008 vilevile mjumbe wa kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM wilaya.

Majukumu mengine, Mpina ni Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Simiyu kuanzia 2005 hadi sasa.

Kwa upande wa taasisi za elimu, Mpina aliwahi kuwa Kamishna wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuanzia 2009 hadi 2015.