Mwalimu, Minja kuwavaa Samia, Mpina urais Oktoba

Dar es Salaam. Mbio za kwenda Ikulu ya Tanzania ndani ya vyama vya siasa zimezidi kushika kasi baada ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) nacho kuwapata viongozi wawili watakapeperusha bendera yake.

Salum Mwalimu, katibu mkuu wa chama hicho, ndiye amepewa jukumu la kupeperusha bendera  hiyo huku Devotha Minja akipendekezwa kuwa mgombea mwenza wake.

Kwa uteuzi huo, Chaumma inaungana na vyama vingine kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM), ambavyo vimekwisha kupata wagombea wake.

Mwalimu na Devotha ambao kabla ta kuingia kwenye siasa walikuwa wanahabari, wamepitishwa na mkutano mkuu uliofanyika leo Alhamisi, Agosti 7, 2025 jijini Dar es Salaam.

Wawili hao wakiteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, watakwenda kuchuana na wenzao kwenye majukwaa ya kisiasa, wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa CCM na Luhanga Mpina ACT-Wazalendo.

Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma-bara, Benson Kigaila ameueleza mkutano huo, mchakato wa kumpata mgombea urais, akisema jina la kiongozi huyo lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, yenye jukumu hilo, katika kikao chake kilichofanyika jana.

“Baada ya kufanya utafiti na kufikiri kwa kina ni mtu gani anaweza kutuvusha, Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuja na jina la Salum Mwalimu, anatufaa kutuvusha kwenye mbio za urais wa Tanzania,” amesema Kigaila.

Amesema hadi kumpata, kwanza walifanya utafiti na: “Tuliangalia nani anaweza kutufaa na kutuvusha, tulifanya mazingatio tukimteua mtu anajua matatizo ya Watanzania, akiyaona anaweza kuumizwa nayo na kuyashughulikia.

“Pia tulitafuta mtu asiyekuwa na mawaa, wa kukimbiliwa na makundi yote lakini awe anaelewa ilani ya chama bila mashaka yoyote, tumepanga kwenda kuipumzisha CCM, inayofanana na mchezaji aliyeko uwanjani hadi anafikisha dakika 90 hajafunga, kwa hiyo inafaa aende benchi na kuingiza mchezaji mpya,” amesema Kigaila.

Baada ya jina hilo kuwasilishwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu na kusomwa kwa wasifu wake, waliulizwa kama wanakubaliana nalo na wajumbe wote walikubali kisha wakampitisha kuwa mgombea urais.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Salum alikuwa mgombea mwenza wa urais kupitia Chadema wakati mgombea urais akiwa Tundu Lissu. Amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu-Bara wa Chadema.

Baada ya wajumbe kumpitisha Mwalimu, alipewa nafasi ya kumpendekeza mgombea mwenza, akianza kutoa sifa kedekede juu ya mwanahabari mwenzake huyo kisha akasema: “Kwa heshima na unyeyekevu mkubwa naomba kumtangaza mgombea mwenza wangu katika kampeni za kuomba kura za urais wa Tanzania, kuwa ni Devotha Minja.”

Mwalimu amesema anaamini mgombea mwenza wake huyo anaweza kusimamia maono na matarajio ya Watanzania kwa masilahi mapana ya nchi na wamuone ni mtu ambaye anaweza kubeba haiba ya watu na kulinda thamani ya Watanzania wote.

“Devotha ni mtu ambaye anaijua nchi na Watanzania, ni mtu ambaye anaonekana  mwezao na kimbilio lao, kwenye shida na hata wakimuona wajue wameniona mimi, naamini tuna uwezo wa kusimamia sera na kuondoa magumu yanayowasumbua wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Devotha amesema: “Kwa unyeyekevu mkubwa nasimama kwenye mkutano huu mkuu, kwanza kukupongeza (Mwalimu) kwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama chetu.”

“Binafsi naridhia kuwa msaidizi wako, makamu wako wa urais katika mapambano haya yakuipumzisha CCM, mgombea urais tumeingia wote Chaumma (kutoka Chadema), tumezunguka nchi nzima tumeona matatizo yanayowasumbua wananchi,” amesema.

Devotha amesema wanaingia kwenye mapambano hayo wakiamini huu ni mwaka wao na anaamini wanaenda kupambana na si kushiriki, kuhakikisha wananchi wananufaika na raslimali zao.

Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa wanakwenda kuchukua dola katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tuna uhakika tunakwenda kuchukua Serikali ya nchi hii, ndiyo maana tunasema tunazindua ilani yetu itakayotoa mwelekeo wetu, ahadi pamoja na namna tutakavyozitekeleza,” amesema Rungwe huku akishangiliwa na wajumbe.

Amesema Watanzania wanalia shida nyingi, hawana mtu anayeweza kuwasaidia lakini majibu yote na suluhu ya matatizo hayo yatajibiwa na chama hicho, kwa kuwa kitakwenda kuwatangaza wagombea wenye ushawishi, wanaokubalika na wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.

“Ni matumaini yetu, mambo yote yatakwenda salama na mambo yote tuliyopanga basi yatekelezwe. Ndugu wajumbe kama wawakilishi tunaomba mtuunge mkono,” amesema Rungwe.

Rungwe amewataka wajumbe hao kutulia wakati wanasuka mipango na muda ukifika wataunda Serikali kwa kuzingatia magumu na matatizo yanayowakabili Watanzania, kwa kuweka watu sahihi.

Akimkaribisha kufungua mkutano huo, Mwalimu ametumia nafasi hiyo kutoa taarifa ya shughuli ya chama ikiwemo ziara ya Chaumma For Change (C4C), kuwa imekuwa ya mafanikio katika kuwafikia wananchi.

“Operesheni zilikuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa tulikuwa tunafanya kwa njia ya anga na ardhini na tumefikia mikoa yote katika kuwafikia wananchi na kuwaandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu,” amesema Mwalimu.

Amesema kupitia ziara hizo wamefanikiwa kujenga mtandao mpana wa wanachama na viongozi kutoka mikoa yote Tanzania huku akieleza hata walivyokuwa wanawasilisha hoja kwa wananchi waliwaelewa.

“Mpango wetu ni kutumia rasilimali zikizopo ili ziwanufaishe wananchi katika kuboresha maisha yao, kuna madini, ardhi yenye rutuba itumike kwa tija, kwani umaskini unaowakabili unatokana na kukosa viongozi wenye maono,” amesema.

Mwalimu amesema katika kuandaa wagombea hadi kufikia Agosti 4, 2025 waliochukua fomu za udiwani ni 2,116 katika kata 3,953, kwa upande wa ubunge wana watiania 183 katika majimbo 222 ya Tanzania Bara na Zanzibar watiania 63 katika majimbo 28 kati ya 50.

“Tuna watiania wanaosubiri kuchukua fomu katika uchaguzi mkuu. Kazi hii si ndogo, tumeifanya katika kipindi cha miezi miwili,” amesema Mwalimu.

Katika mkutano huo, wito wa kulinda amani wakati wa uchaguzi umetawala salamu za viongozi mbalimbali wa kisiasa na wadau wa demokrasia waliohudhuria mkutano mkuu huo.

Ramadhan Abdallah, Mwakilishi kutoka chama cha ADC, licha ya kumpongeza Mwenyekiti Rungwe kwa hatua kubwa ya kujenga chama, amesisitiza amani wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

“Hakika nikupongeze Mheshimiwa Rungwe kwa juhudi za ujenzi wa chama hiki. Niwapongeze sana kwa hatua mlizofikia. Lakini niwasisitize twendeni kwenye uchaguzi tukazingatie amani ya nchi yetu,” amesema.

Kosta Kibonde, mwenyekiti wa Chama Makini ambaye pia ni mgombea urais wa chama hicho, amesema: “Nawapongeza kwa maandalizi makubwa, ni mkutano wa kihistoria. Chaumma ninayoijua si Chaumma ninayoiona hapa leo. Hakika kazi mliyoifanya ni ya kizalendo.

“Twendeni tukaombe kura, lakini mkatangulize mbele amani ya nchi yetu.”

Majaliwa Kyala kutoka Chama cha SAU, amesisitiza umuhimu wa kutatua matatizo ndani ya vyama ili kuimarisha taasisi za kisiasa.

“Tusipotatua matatizo yatatuongoza na kusambaratisha taasisi zetu,” amesema na kusisitiza matatizo yanatakiwa kutatuliwa kwa amani ili chama kiendelee kukua.

Salamu zenye kugusa hisia pia zimetolewa na Anna Ngalawa, mwenyekiti wa Shirikisho la Vijana kutoka Chama cha Wenye Ulemavu ambaye ametoa wito kwa vyama vya siasa kuhakikisha vinadumisha amani wakati wa uchaguzi, kwani machafuko huwaumiza zaidi watu wenye ulemavu pindi yanapotokea.

“Machafuko yakitokea ni watu wenye ulemavu ndio hupata taabu. Tunawaomba wanasiasa mkazingatie suala la amani ya nchi yetu.”

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Maduhu William ameweka bayana matarajio ya asasi za haki za binadamu akisisitiza amani, utawala wa sheria na kukomesha ukandamizaji katika jamii.

“Msilete mgombea ambaye hatazungumza suala la amani kwa vitendo. Katumieni muda wa uchaguzi kuuza ilani ya Chaumma, msitukane watu majukwaani,” amesisitiza.

Shughuli hiyo imeshuhudiwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, ambaye ametilia mkazo suala la amani wakati wa uchaguzi, akivisihi vyama vya siasa kuzingatia sheria na Katiba za vyama vyao katika michakato ya ndani.

“Chaumma hii siyo ile. Hongereni sana. Katika ushindani, zingatieni sheria za chama chenu na za nchi, mlinde amani ya nchi yetu,” amesema.