Mwana FA, AY washinda rufaa shauri la mabilioni ya Tigo

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufaa imetengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha ya awali iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya Ilala katika kesi ya madai ya hakimiliki iliyofunguliwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Flavour), Hamisi Mwinyijuma (Mwana FA) na Ambwene Yesaya (AY).

Mahakama ya Rufaa imetengua hukumu hiyo baada ya kukubaliana na rufaa waliyokata warufani wakipinga ya awali ya Mahakama Kuu kuhusu malipo ya fidia ya Sh2.1 bilioni walizolipwa na kampuni ya huduma za simu za mkononi Mic (T) Limited maarufu Tigo (sasa Honora).

Katika hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyotolewa leo Alhamisi Agosti 7, 2025 na jopo la majaji watatu imeiamuru Mahakama Kuu kuisikiliza tena kuhusu sababu nyingine za rufaa iliyokatwa na Tigo ambazo hazikusikilizwa awali.

Majaji hao Gerald Ndika (kiongozi wa jopo), Panterine Kente na Latifa Mansour wamefikia uamuzi huo kwa kuzingatia sababu moja ya rufaa kati ya nne walizowasilisha warufani (Mwana FA na AY) kuhusu mamlaka ya Mahakama ya Wilaya kusikiliza kesi za hakimiliki, ambayo imetosha kutengua hukumu ya Mahakama Kuu.

Mahakama Kuu ilibatilisha hukumu ya Mahakama ya Wilaya Ilala iliyowapa ushindi wasanii hao, ikidai haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa imekubaliana na sababu ya wasanii hao kuwa, Mahakama ya Wilaya ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Imesema msimamo sahihi wa kisheria ni kwamba, Sheria ya Hakimiliki, ikiwa ni sheria mahususi iliyoandikwa ilitoa kwa uwazi mamlaka ya awali na ya kipekee kwa mahakama za wilaya kushughulikia mashauri ya uvunjaji wa hakimiliki nchini Tanzania.

“Kwa kuwa kuna sheria mahususi iliyoandikwa ambayo imetoa mamlaka kwa mahakama za wilaya kushughulikia mashauri ya uvunjaji wa hakimiliki kama mahakama ya awali, basi sheria ya mamlaka ya jumla haiwezi kutumika,” limeeleza jopo hilo na kuongeza:

“Kwa msingi wa maelezo yote hapo juu, tunaikubali rufaa hii, tunabatilisha uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu katika rufaa ya madai namba 112 ya mwaka 2019. Pia tunaamuru kuwa Mahakama Kuu ishughulikie sababu nyingine zote za rufaa zilizowasilishwa na mjibu rufaa.”

Mbali na hayo, imemuamuru mjibu rufaa, kampuni ya Honora Tanzania Public Limited Company (MIC, maarufu kama Tigo wakati huo) kuwalipa wasanii hao gharama za rufaa hiyo.

Mwaka 2012, Mwana FA na AY walifungua kesi ya madai katika mahakama ya wilaya dhidi ya kampuni ya Tigo (Honora) kwa kutumia nyimbo zao za Usije Mjini na Dakika Moja kibiashara kwenye miito ya simu pasipo ridhaa yao.

Katika kesi hiyo namba 17 ya mwaka 2012, wasanii hao waliiomba mahakama itamke kuwa mdaiwa alivunja haki zao kwa kutumia kibiashara kazi zao za kimuziki walizotunga kwa pamoja bila ridhaa yao wala makubaliano kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Pia waliomba zuio dhidi ya mdaiwa, wakala au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba yake kutokuendelea na uvunjaji huo wa haki zao, kwani walishazisajili katika Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki Tanzania (Cosota), Septemba 24, 2010 isipokuwa tu kwa kibali kutoka kwao.

Vilevile waliiomba malipo ya fidia ya jumla ya Sh4.37 bilioni, Sh50 milioni zikiwa ni fidia ya hasara ya jumla na Sh4.32 bilioni zikiwa ni hasara maalumu pamoja na riba ya asilimia 20.

Tigo katika utetezi wake ilidai ilipelekewa nyimbo hizo na kampuni ya Cellulant Tanzania Limited, waliyoingia nayo mkataba wa kisheria kwa huduma hiyo na kwamba, ndiyo inapaswa kuwalipa wasanii husika.

April 11, 2016, Mahakama ya Wilaya Ilala iliiamuru Tigo kuwalipa wasanii hao fidia ya Sh2.16 bilioni baada ya kukubaliana na hoja zao katika kesi hiyo ya madai.

Mahakama katika hukumu iliyotolewa na hakimu Hassan ilikubaliana na madai na hoja za wasanii hao kuwa mdaiwa alitumia kazi zao bila ridhaa yao na kwamba alijipatia mapato, huku wasanii hao wakipata hasara kwa kutokufanya biashara kwa kazi zao hizo.

Hata hivyo, baada ya kufanya tathmini ya fidia, Hakimu Hassan aliamuru wasanii hao walipwe fidia ya hasara ya jumla ya Sh25 milioni, na hasara halisi ya Sh2.16 bilioni.

Kampuni hiyo haikuridhika na hukumu ikakata rufaa Mahakama Kuu, pia iliomba kuzuia utekelezaji wa hukumu ili kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa rufaa yao, lakini hilo halikufanikiwa.

Hivyo, wasanii hao waliendelea na hatua za utekelezaji wa hukumu  wakapata amri ya mahakama ya kukamata akaunti za kampuni hiyo ambayo iliwalipa fidia, huku ikiendelea na mchakato wa rufaa.

Tigo katika rufaa iliwasilisha sababu 11 za kupinga hukumu na amri ya Mahakama ya Wilaya Ilala, lakini Jaji Joaquine De-Mello alitengua hukumu hiyo kwa kutumia sababu moja pekee, kwamba mahakama hiyo haikuwa na mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.

Mahakama Kuu katika hukumu ya rufaa hiyo ya Tigo, ilibatilisha na kutengua hukumu ya Mahakama ya Wilaya Ilala iliyoiamuru kampuni hiyo kuwalipa fidia wasanii hao.

Jaji De-Mello alikubaliana na hoja za Tigo iliyowakilishwa na Wakili Rosan Mbwambo kuwa kiwango cha fidia walichodai wasanii hao kwenye hati ya madai yao, zaidi ya Sh4.3 bilioni ni kikubwa kuliko uwezo wa kisheria wa mahakama hiyo.

Kutokana na hukumu hiyo ndipo wasanii hao kupitia wakili wao Albert Msando wakakata rufaa Mahakama ya Rufaa, huku wakiwasilisha sababu nne.

Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo, waombaji rufaa waliwakilishwa na mawakili Elisa Mndeme na Salmin Suleiman Mwiry, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na wakili John Ismail.

Kwa hukumu ya Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu inapaswa kusikiliza sababu nyingine 10 ambazo kampuni hiyo iliziwasilisha na ambazo haikuziamua.