Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa amewahakikishia wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kwamba wanakwenda kuchukua dola katika Uchaguzi Mkuu utakaofayia Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Rungwe amesema hayo leo Alhamisi, Agosti 7, 2025 wakati anafungua mkutano mkuu huo unaoendelea katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, watapitisha majina ya wagombea urais wa Tanzania na Zanzibar.
“Tunauhakika tunakwenda kuchukua Serikali ya nchi hii, ndiyo maana tunasema tunazindua ilani yetu itakayotoa mwelekeo wetu, ahadi pamoja na namna tutakavyotekeleza,” amesema Rungwe huku akishangiliwa na wajumbe.
Amesema Watanzania wanalia shida nyingi hawana mtu anayeweza kuwasaidia lakini majibu yote na suluhu ya matatizo hayo yatajibiwa na chama hicho kwakuwa kitakwenda kuwatangaza wagombea wenye ushawishi, wanaokubalika na wenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
“Ni matumaini yetu, mambo yote yatakwenda salama na mambo yote tuliyopanga basi yatekelezwe. Ndugu wajumbe kama wawakilishi tunaomba mtuunge mkono,” amesema Rungwe.
Rungwe amewataka wajumbe hao kutulia wakati wanasuka mipango na muda ukifika wataunda Serikali kwa kuzingatia magumu na matatizo yanayowakabili Watanzania kwa kuweka watu sahihi.
Awali, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu akitoa taarifa ya shughuli ya chama ikiwemo ziara ya Chaumma For Change (C4C) amesema imekuwa ya mafanikio makubwa katika kuwafikia wananchi.
“Operesheni zilikuwa na mafanikio makubwa kwakuwa tulikuwa tunafanya kwa njia ya anga na ardhini na tumefikia mikoa yote katika kuwafikia wananchi na kuwaandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu,” amesema Mwalimu.
Amesema kupitia ziara hizo wamefanikiwa kujenga mtandao mpana wa wanachama na viongozi kutoka mikoa yote Tanzania huku akieleza hata walivyokuwa wanawasilisha hoja kwa wananchi waliwaelewa.
“Mpango wetu ni kutumia rasilimali zikizopo ili ziwanufaishe wananchi katika kuboresha maisha yao, kuna madini, ardhi yenye rutuba itumike kwa tija, kwani umaskini unaowakabili unatokana na kukosa viongozi wasiokuwa na maono,” amesema.
Mwalimu amesema katika kuandaa wagombea hadi kufikia Agosti 4, 2025 waliochukua fomu za udiwani ni 2116 kati ya Kata 3953, kwa upande wa ubunge wana watiania 183 katika majimbo 222 ya Tanzania Bara na Zanzibar wana watiania 63 katika majimbo 28 kati ya 50.
“Tuna watiania wanaosubiri kuchukua fomu katika uchaguzi mkuu. Kazi hii si ndogo, tumeifanya katika kipindi cha miezi miwili,” amesema Mwalimu.
Kuhusu ilani ya uchaguzi, Mwalimu amesema ilani hiyo imejikita katika kutoa majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuiita kuwa ni “dawa ya magonjwa ya taifa” tangu uhuru.
“Ilani yetu imesheheni majibu ya changamoto mbalimbali za wananchi. Itakuwa ukombozi wa kweli kwa kizazi cha sasa na kijacho. Tunalenga kukuza uchumi jumuishi kwa lengo la kupunguza umaskini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuboresha maisha na ustawi wa jamii ya Watanzania,” amesema Mwalimu.
Baadhi ya nguzo kuu za Ilani hiyo ni pamoja na kuondoa umaskini wa kipato, kujenga uongozi unaozingatia maadili, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria, kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi na kuvutia wawekezaji kwa mazingira rafiki.
Aidha, Mwalimu amegusia umuhimu wa kuhuisha na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Endelea kufuatilia Mwananchi