Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), watamaliza ubishi na kutoa majibu nani atapeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais wa Tanzania baada ya minong’ono, tetesi na maswali mengi ni nani atasimama.
Pamoja na usiri uliotawala takriban wiki nzima, Mwananchi leo Alhamisi, Agosti 7, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam unapofanyika mkutano huo mkuu, limeelezwa na chanzo cha kuaminika majina mawili ya mgombea urais na mwenza.
Majina yaliyopo kwenye faili na yanatarajiwa kutangazwa mbele ya wajumbe wa mkutano huo, ili kuyathibitisha ni la katibu mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu ambaye inaelezwa atakuwa mgombea urais wa Tanzania.
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma-Bara, Devotha Minja yeye inaelezwa atasimama kama mgombea mwenza. Hata hivyo, Devotha amekwishachukua fomu ya kuwania ubunge Morogoro Mjini.
Salumu na Devotha wataongoza safari ya Chaumma kwenda Ikulu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
“Majina hayo yalipitishwa jana kwenye kikao kilichoketiwa, tukajadili na kukubaliana Salum na Devotha wapeperushe bendera ya chama chetu katika uchaguzi mkuu 2025, tumekubaliana iwe siri tusimueleze yeyote, ila muda ukifika tutangaze” amedokeza mmoja wa wajumbe wa kamati kuu.
Chanzo hicho kimedai mwanzo matarajio na walivyojipanga nafasi hiyo alitakiwa agombee, mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe lakini kulingana na upepo ulivyo wameona bora wabadili gia angani, Salum na Devotha wapeperushe bendera ya chama hicho kwenye nafasi hizo.
Mmoja wa watu wa karibu na Mbowe aliyezungumza na Mwananchi amesema: “Mwenyekiti hawezi kwenda Chaumma, ingawa watu wake wa karibu wengine wamekwenda Chaumma na wengine wapo Chadema. Yaani Freeman ana watu kwenye vyama vyote kwa hiyo kuhusishwa kwake ni kawaida lakini hakuna lolote.”
Hata hivyo, jitihada za mara kadhaa za Mwananchi kumpata Mbowe zimekwama kwani simu yake ya mkononi haikupokelewa.
Chanzo kingine kutoka Chaumma kimesema katika mkutano huo unaoendelea Mlimani City, Mbowe anaweza kutokea: “Lolote leo linaweza kutokea, Freeman akaja hapa ukumbini kwa hiyo subirini mtaona.”
Kabla ya kuzungumza na chanzo hicho, awali Mwananchi lilizungumza na Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma, John Mrema kutaka kujua ni nani? atawania nafasi hiyo katika majibu yake amesema: “Leo ni siku ya Saprize ‘package’ bado muda mchache tu utajua njoo pale Mlimani City.”
Katika mkutano huo, kabla ya kutangazwa majina hayo, wajumbe hao wataanza kuzindua ilani yao inayoeleza dira, malengo na mikakati yao katika kutatua changamoto mbalimbali za kitaifa. Ahadi kwa wananchi kuhusu mambo ambayo chama hicho kitayatekeleza endapo kitapata ridhaa ya kuunda Serikali.
Chama hicho kilichokuwa cha kawaida miaka 13 iliyopita kabla ya kuanza kuzungumzwa zaidi kuanzia mapema mwaka huu, baada ya waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujiunga nacho, uamuzi utakaofanywa kwa kuwatangaza wagombea hao unaenda kuchochea mbio za urais.
Tayari mkutano huo umeanza kwa viongozi wakuu wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa wameingia ukumbini.
Mkutano huo unafanyika baada ya kutanguliwa na vikao vya Sekretarieti na Halmashauri Kuu vilivyokuwa na jukumu la kuandaa ajenda za mkutano huo mkuu. Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni watiania wa udiwani, ubunge na uwakilishi.
Baadhi ya makada na wajumbe wa mkutano huo, akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Ngorongoro, Zakaria Bayo amesema matarajio yao kupitia mkutano huo watapata mgombea bora mwenye ushawishi na uwezo wa kuongoza dola wakichukua katika uchaguzi unaokuja.
“Ni matumaini yetu mkutano utakuwa wa heri lakini jambo kubwa tunahitaji, kupitia mkutano huu tupate mgombea mwenye sifa na uwezo wa kuongoza dola, iwapo tutashinda Uchaguzi Mkuu 2025,” amesema.
Mjumbe mwingine, Hamad Juma kutoka Pemba amesema wanatarajia mkutano utakuwa mzuri na utaisha salama kwa kuwapatia wagombea watakaowafikisha wanakohitaji.
Alipoulizwa kuhusu Salum, Devotha kugombea urais amesema: “Hao wanafaa hakuna mashaka na uwezo wao, Salum ana kitu ambacho kinaweza kuwa zaidi kwa kuwatumikia Watanzania,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi