Morogoro. Katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira nchini, Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamesaini makubaliano ya utekelezaji mradi wa matumizi ya nishati ya umeme kwa ajili ya kupikia kwenye shule 50 za msingi na sekondari nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Agosti 6, 2025 baada ya makubaliano hayo kusainiwa, Profesa Eliakim Zahabu, Mtendaji Mkuu wa kituo hicho kilipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) alisema shule zitakazohusika katika utekelezaji wa mradi huo utakaohusisha ufungaji wa majiko ya umeme ni za mikoa ya Kigoma, Tabora, Dodoma na Dar es Salaam.
Amesema mikoa hiyo imeingizwa kwenye mradi baada ya utafiti kufanyika na kubaini uwepo wa kasi kubwa ya ukatakaji miti na matumizi ya kuni na mkaa.
“Katika utafiti tuliofanya tumebaini Dodoma ni mkoa unaokuwa kwa kasi na idadi ya watu inaongezeka kila kukicha kwa kuwa ni makao makuu ya nchi, lakini Dar es Salaam kumekuwa na ongezeko la watu na taasisi mfano shule, vyuo na hospitali, hivyo kumekuwa na matumizi makubwa ya nishati ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia,” amesema na kuongeza:
“Hivyo, tuliona ni vyema mradi huu uende kwenye mikoa hii ili kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa ambayo inachochea uharibifu wa misitu. Lakini kwa Tabora na Kigoma kwenye utafiti mikoa hii ilibainika kuwa na uharibifu wa misitu kwa kiasi kikubwa, misitu imekuwa ikiteketea kwa ajili ya matumizi ya nishati ya mkaa na kuni inayotumiwa kwenye miji na majiji mbalimbali nchini.”
Amesema mradi huo licha ya kulenga kutatua changamoto ya uharibifu wa mazingira, pia ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi wa miaka 10 (2024 hadi 2034) uliozinduliwa mwaka jana na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kuhusu uendeshaji wa mradi huo, amesema shule zilizochaguliwa zitakapotekeleza mradi, gharama za umeme zitakazotokana na majiko hayo zitalipwa kupitia mradi.
Mkurugenzi Tathmini na Upimaji wa kituo hicho, Dk Deo Shirima amesema mradi huo umelenga zaidi shule za msingi na sekondari ambazo zimekuwa zikitumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupika chakula cha wanafunzi.
Amesema mradi utasaidia kuokoa misitu ambayo inateketea kila siku kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Kupitia mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, inaelekezwa taasisi zote zinazotoa huduma za chakula kwa watu zaidi ya 100 zikiwamo shule, magereza, hospitali na maeneo mengine kuhakikisha zinatumia nishati safi ya kupikia.
Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy, amesema takribani hekta 500,000 hupotea kila mwaka nchini kutokana na uharibifu wa misitu unaochochewa na matumizi ya nishati ya kuni na mkaa, hivyo matumizi ya nishati ya umeme kwenye shule itaenda kutatua changamoto hiyo.
Amesema matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa pia imekuwa ikisababisha madhara ya kiafya kwa kina mama na watoto, yakiwamo ya kupata magonjwa ya mfumo wa upumuaji.