WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga zimepangwa kwa pamoja kuanzia hatua ya awali ya raundi ya kwanza tofauti na misimu mitatu iliyopita zilipokuwa zikitofautiana kwa Simba kuanzia raundi ya pili.
Hatu hiyo imetokana na mabadiliko yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa msimu ujao wa 2025-26 ambao klabu karibu zote shiriki zinaanzia hatua hiyo ya awali isipokuwa vigogo viwili tu vinanyoongoza katika orodha ya klabu bora Afrika.
Droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho inatarajiwa kupangwa Dar es Salaam kesho Jumamosi, ikiwa ni mara ya kwanza inafanyika nje ya makao makuu ya CAF yaliyopo Misri baada ya kupita miaka mingi.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya CAF, msimu huu utashuhudiwa klabu 62 zikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini tofauti na miaka ya nyuma ambapo klabu nne hadi sita zilikuwa zinaanza moja kwa moja hatua ya pili, mwaka huu ni klabu mbili tu za Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ndizo zitaanzia hatua hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba timu 60 zitacheza hatua ya kwanza, ambapo 30 zitaungana na Mamelodi na Ahly katika hatua inayofuata na kuwa timu 32, hii ina maana kuwa sasa kuna uwezekano wa vigogo vya soka Afrika vikatolewa hatua ya kwanza ya michuano hiyo kutoka na droo hiyo itakayofanyika kwa uwazi kutokana na wakubwa wengi kuungana huku.
Hivyo watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga pamoja na watani wao Simba ambao watashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wote watalazimika kuanza kampeni ya CAF kuanzia raundi hii ambayo mechi zake za kwanza zitapigwa kuanzia Septemba 19, 2025.
Msimu uliopita Yanga ilianzia raundi hii pamoja na Azam FC, lakini huko nyuma Simba ilikuwa ikianzia raundi ya pili, ambapo ilikuwa ikicheza mechi moja ya nyumbani na ugenini na kutinga hatua ya makundi, ila sasa ni tofauti, italazimika kucheza na wapinzani wawili tofauti.
Hii ina maana kwamba, baada ya hatua ya kwanza, timu 32 zitacheza hatua ya pili na kubakiza timu 16 ambazo zitaingia hatua ya makundi ambayo kila kundi litakuwa na timu nne.
Uamuzi wa CAF kuileta droo hiyo Tanzania unatokana na mafanikio ya soka Afrika Mashariki na ongezeko kubwa la watazamaji kutoka ukanda huo, hasa kutokana na mchango wa klabu kama Simba na Yanga kwenye mashindano ya kimataifa, lakini pia uwepo wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN 2024 inayoendelea kwa sasa ikishirikisha nchi 19 zikiwamo wenyeji Tanzania, Kenya na Uganda.
Azam Media, ambao ni washirika wa kimkakati wa CAF kwa ukanda wa Afrika Mashariki, wamepewa heshima ya kuandaa droo hiyo baada ya mafanikio ya matukio kama haya kwenye studio za SuperSport na beIN Sports.
Droo hiyo itaonyeshwa mubashara kupitia YouTube ya CAF na vituo vingine vya matangazo.
Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho itaanza rasmi Novemba 21, 2025, huku hatua ya mtoano ikipangwa kuanza Machi 13, 2026.
Wakati Simba na Yanga wakianza mapema, wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika Azam FC na Singida Black Stars nao watapitia mlango huohuo wa hatua ya awali, lakini huku timu sita hazitacheza hatua hii. Hii ni sawa na wawakilishi wa Zanzibar, KMKM (Shirikisho) na Mlandege (Ligi ya Mabingwa).
Zamalek na Al Masry za Misri, Wydad Casablanca (Morocco), USM Alger na CR Belouizidad za Algeria na Stellebosch ya Afrika Kusini ndizo zitakazoanzia raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayoshirikisha jumla ya timu 58, ambapo bingwa wa msimu uliopita alikuwa ni RS Berkane ya Morocco iliyoizidi Simba ujanja kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1. Fainali ya mwisho ikipigwa visiwani Zanzibar.