Dodoma. Waliokuwa wabunge wa Mkoa wa Dodoma, wamemtaja marehemu Job Ndugai kuwa ilikuwa alama yao na chuo cha kuwafunda wengine.
Ndugai ambaye amedumu katika Jimbo la Kongwa kwa vipindi vitano mfululizo, amefariki dunia jana Jumatano Agosti 6, 2025 Jijini Dodoma.
Ndugai ndiye alikuwa mbunge kwa muda mrefu zaidi kati ya wabunge waliomaliza muda wao hivi karibuni na aliingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka 2000, hivyo kulitumikia Jimbo la Kongwa kwa miaka 25.
Spika huyo wa zamani amefariki dunia zikiwa zimepita siku mbili tangu aliposhiriki uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kushinda.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 7, 2025 namna alivyopokea msiba wa aliyekuwa mbunge wa Kongwa na Spika mstaafu, Job Ndugai, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene amesema;
“Wengi hawajui, lakini nitamkumbuka Ndugai kwa namna alivyoongoza mageuzi makubwa ya kanuni za Bunge mwaka 2007 ambazo zinatumika hadi leo.”
Simbachawene ambaye pia ameutumikia ubunge kwa miaka 20, amesema kilicholala siyo mwili wa mwanasiasa huyo, bali ni jabali la maendeleo kwa Mkoa wa Dodoma.
Amesema katika Bunge lililoongozwa na marehemu Samuel Sita, Ndugai alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyopewa nafasi ya kutembelea mabunge mbalimbali duniani kwa lengo la kujifunza jinsi ya uendeshaji wa shughuli zao na baada ya kurejea, akaongoza jopo la utungaji wa kanuni.
Amesema kwa sasa anajiona mpweke kwa sababu atakosa mawazo na mchango wa mkongwe huyo ambaye alikuwa pia mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Dodoma.
“Nafasi hiyo (mwenyekiti) huwa tunapeana kwa kuangalia seniority (uzowefu), sasa yeye alianza ubunge mwaka 2000 wakati mimi nilianza 2005, hivyo sikuwa Makamu Mwenyekiti, bali nilitumika kama hayupo, lakini kwa kweli tumepoteza jembe na mtu makini sana tena mwenye misimamo yake,” amesema Simbachawene.
Simbachawene ambaye ameshinda kura za maoni katika Jimbo la Kibakwe, amesema enzi za uhai wake, Ndugai aliamini na kusimamia haki na hakuwa tayari kuona inapotezwa na mtu.
Hata hivyo, ameshukuru na kupongeza namna watu wa Dodoma walivyoshikamana tangu walipopokea taarifa za msiba huo na imemtia moyo kuwa baada ya ratiba ya mazishi kutolewa na Serikali, wataungana vema kumsindikiza katika nyumba yake ya milele.
Akimzungumzia marehemu Ndugai, aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma ambaye ameshinda kura za maoni Jimbo la Kondoa Mjini, Mariam Ditopile amesema; “Tumempoteza kiongozi ambaye aliipenda nchi yake kwa dhati na aliipenda sana Dodoma.”
Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Dodoma ambaye ameshinda Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde ameeleza namna Ndugai alivyokuwa na matamanio ya maendeleo kwa Mkoa wa Dodoma.
“Kama mwenyekiti wetu wa wabunge wa Mkoa wa Dodoma, alitamani kuona maendeleo ya Dodoma yanakua kwa kasi hasa mkazo wake mkubwa siku zote ulikuwa ni kwenye kuwajengea mfumo mzuri watoto wa Dodoma kupata elimu bora,” amesema Mavunde.
Amesema wabunge wataendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa elimu kwa jamii ya WanaDodoma kama njia nzuri ya kumuenzi marehemu Ndugai.
Naye aliyekuwa mbunge wa Mvumi, Livingston Lusinde amesema Ndugai alikuwa mwalimu wake kwenye siasa na ataendelea kumkumbuka kwa misimamo yake katika kuamua mambo hasa kunapotokea mkwamo.
Lusinde (Kibajaji) anamkumbuka Mzee Ndugai alivyokuwa akimtia moyo tangu 2025, amesema alipokuwa Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Kongwa, alikuwa akimtabiria mema na kamwe hakumkatia tamaa.