TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ishindwe yenyewe kuvuna mamilioni ya pesa kutoka kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anayetoa vibunda kila inaposhinda mechi.
Stars ilianza kuvuta mkwanja mrefu wa Sh. 60 milioni mechi ya ufunguzi dhidi ya Burkina Faso, Sh. 20 milioni ilitoka kwa Rais Samia, Sh. 20 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Sh. 20 kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi.
Wachezaji wa Stars na benchi la ufundi linaloongozwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ akisaidiana na Juma Mgunda wanaendelea kuneemeka baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania, mechi iliyopigwa jana Agosti 6, Uwanja wa Benjamin Mkapa, walipewa Sh. 10 milioni kutoka kwa Rais Samia, Sh.20 milioni kutoka kwa Chalamila na Sh.25 Milioni ahadi aliyoitoa Azim Dewji.
Aliyekabidhi zawadi ya pesa kutoka kwa Rais Samia ni Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, aliyesema: “Pesa za mama ni nzito, tutaangalia namna nyingine ya kuwapa motisha ili muendelee kushinda, mlichokifanya Watanzania wana furaha.”
Kwa upande wa Chalamila alisema: “Tunachokifanya ni kumuunga mkono mheshimiwa Rais kwa kila anachokifanya, kuhakikisha tunakuwa na heshima kubwa Dar es Salaam na Afrika Mashariki kwa ujumla wake.”
Wakati pesa hizo zinakabidhiwa alikuwepo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyesema: “Tumejaaliwa kizazi cha wachezaji wenye uwezo mkubwa, mmepata mnachostahili pia mjue hakuna mechi rahisi mwendelee kupambana.”