Tarime. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya mkoani Mara limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wali-oandamana wakidai watu wawili wamepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Wanaodaiwa kupotea ni Sinda Mseti, mgombea udiwani Kata ya Sirari, wilayani Tarime aliyeongoza kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika Agosti 4, 2025 pamoja na rafiki yake aliyefahamika kwa jina moja la Kitale.
Katika kura hizo, Sinda aliongoza kwa kupata kura 263, huku diwani aliyemaliza muda wake, Amos Sagara akishika nafasi ya pili kwa kura 64 na Boni Nyablanketi alipata kura 13.
Maandamano hayo yamefanyika mjini Sirari leo Alhamisi Agosti 7, 2025, huku waandamanaji hao wakidaiwa kuchoma matairi na kuharibu miun-dombinu ya barabara wakitaka Sinda arejeshwe wakidai ni diwani wao mtarajiwa.
Inaelezwa maandamano hayo yalisimamisha baadhi ya shughuli kutokana na vurugu zilizofanyika na kusababisha kufungwa barabara za kuingia na kutoka mjini Sirari kwa takribani saa tatu.
Kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Mark Njera ali-potafutwa na Mwananchi kuzungumzia tukio hilo simu yake ya mkononi iliita pasipo kupokewa na hata ujumbe aliotumiwa haukujibiwa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele aliyefika mjini Sirari amewataka wananchi kuwa watulivu kwa kuwa, tayari Serikali imeamza kushughulikia suala hilo.
“Kama walivyosema huyu mtu alishinda kura za maoni kwa hiyo upo uwezekano akapeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi, kwa hiyo tayari uchunguzi umeanza,” amesema.
Kuhusu madhara yaliyotokea kutokana na maanda-mano hayo, Gowele amesema hakuna madhara kwa binadamu zaidi ya kuchomwa matairi.
Amesema ameongea na wananchi na wamemuelewa hivyo wameacha maandamano.
Kwa upande wake, Mwita Mseti, ambaye ni mdogo wake Sinda, amesema tukio la ndugu yao kupotea lilitokea jana Agosti 6, 2025 saa 10:00 jioni akiwa njiani kuelekea mjini Tarime akitokea Sirari.
“Niliongozana naye, yeye akiwa mbele anaendesha gari lake akiwa na rafiki yake, mimi nikawa nyuma. Tulipofika kwenye ‘barrier’ (kizuizi) pale Nkende tulikutana na askari polisi tukasimama,” amesema.
Mwita amesema waliposimama askari mmoja am-baye anadai ana cheo kikubwa alimfuata kaka yake kwenye gari na kuzungumza naye, maongezi am-bayo hakujua yalihusu kitu gani.
Anadai kaka yake na askari huyo wanafahamiana na kuna nyakati hukutana kwa mazungumzo.
Amedai baada ya maongezi hayo askari huyo alipanda gari la kaka yake kisha likaondoka na kwamba, yeye alishindwa kuwafikia kwani wali-potezana mita chache baadaye.
“Sikuwa na wasiwasi nikaendelea na shughuli zangu, lakini baada ya saa moja ikabidi nimpigie simu cha ajabu simu zikawa hazipatikani. Hapo ndipo nikapa-ta hofu, ikabidi tuanze kufuatilia,” amesema.
Amesema walikwenda ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda ya Tarime/Rorya kabla ya kwenda ofisi ya kamanda ambako walikesha hadi asubuhi wakisubiri majibu ya walipo ndugu zao.
“Asubuhi tulirudi Sirari kwa sababu niliitwa Kituo cha Polisi Sirari kwa ajili ya kutoa maelezo, ilipofika saa mbili asubuhi wananchi walianza kuandamana wakitaka kujua alipo diwani wao mtarajiwa,” ames-ema.
Mwita amesema baada ya maandamano yaliyodumu kwa saa kadhaa, mkuu wa Wilaya ya Tarime alifika eneo hilo na kuwataka wananchi kuacha kuanda-mana watulie, kwani suala hilo linafanyiwa kazi na Serikali, akiahidi ndugu zao watapatikana.
Amedai wakati ndugu yao akitoweka alikuwa na zaidi ya Sh15 milioni alizozipata baada ya kuuza mahindi.
Amesema mbali na siasa, kaka yake ni mfanyabiasha-ra katika eneo hilo la mpaka wa Tanzania na Kenya.
Tukio hilo limetokea ikiwa siku 10 zimepita tangu kuripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha aliyekuwa mgombea udiwani Kata ya Ganyange, wilayani Tarime, Siza Mwita.
Mwita pamoja na rafiki yake Anthony Gabriel wali-potea wakiwa kwenye safari zao za kibiashara baada ya gari lao kukutwa likiwa limetelekezwa mjini Nze-ga, mkoani Tabora.
Katika kura za maoni ndani ya CCM, Mwita alishika namba tatu kwa kupata kura 120, akizidiwa kwa ku-ra 22 na mshindi wa kwanza katika kinyang’anyiro hicho.