Taifa Stars ina ‘sapraizi’ yenu

ACHANA na matokeo ya mechi ya jana usiku wakati Taifa Stars ikimalizana na Mauritania katika mechi ya pili ya Kundi B la michuano ya CHAN 2024, timu hiyo ya taifa ina sapraizi kwa mashabiki wa soka kupitia fainali hizo, kama itaendelea na moto katika mechi mbili zijazo za kundi hilo.

Stars inayoshiriki fainali za tatu za michuano hiyo ya Ubingwa wa nchi za Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani, ilianza michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 na kuwa mara ya kwanza kwa timu hiyo kupata ushindi katika mechi ya kwanza ya makundi ya CHAN

Katika ushiriki wa fainali zote mbili ikiwamo ile ya mwaka 2009 iliyofanyika Ivory Coast na zile za mwaka 2020, Tanzania ilimaliza ikiwa na pointi nne, lakini ikipoteza mechi zote za kwanza mbele ya wapinzani na kushinda kuvuka kwenda hatua inayofuata.

Hata hivyo, safari hii Stars ilianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso na jana ilikuwa ikisaka pointi nyingine ambazo zinaweza kuwa ni sapraizi kwa timu hiyo kwa fainali hizi kama wenyeji kumaliza na pointi zaidi na zile za fainali mbili zilizopita.

Rekodi zinaonyesha Stars ilianza fainali za kwanza za 2009 kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Senegal kabla ya kuwafunga wenyeji Ivory Coast pia bao 1-0 na kutoka sare ya 1-1 na Zambia na kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne.

Fainali za 2020 zilizofanyika Cameroon, Stars ilianza kwa kichapo cha mabao 2-0 kisha kushinda 1-0 dhidi ya Namibia na kumaliza na sare ya 2-2 dhidi ya Guinea na kumaliza nafasi ya tatu katika Kundi D ikiwa na pointi nne pia kama ilivyokuwa fainali za 2009.

Lakini ushindi dhidi ya Burkina Faso na kama itakomaa katika mechi mbili zilizosalia ikiwamo ya wikiendi hii itakapokabiliana na Madagascar na ile ya mwisho ya Agosti 16 dhidi ya Afrika ya Kati inaweza kuwa sapraizi kwa mashabiki kwa kuishuhudia Stars ikivuna pointi nyingi na kuvuka makundi.

Kocha wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ mapema akizungumzia ushiriki wa Tanzania kama wenyeji alikiri licha ya kuwaheshimu wapinzani wao, lakini lengo kubwa safari hii ni kuiona Stars ikivuka makundi na kwenda robo fainali ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu mwaka 1980 ilicheza fainali za kwanza za Afcon zilizofanyika Nigeria.

“Tuna kila sababu ya kupambana na kuwapa raha Watanzania tukiwa kama wenyeji kuona tunafika mbali na hata ikiwezekana kubakisha kocha nyumbani kama ilivyo slogani ya ‘Linakuja Nyumbani’,” alinukuliwa Morocco, kocha wa kwanza mzawa kuipeleka Tanzania katika fainali hizo za CHAN na Afcon 2015 kwa mipigo.

Bila matokeo ya usiku wa jana, Stars ikishinda mechi mbili za mwisho itakusanya pointi sita, ikichanganywa na zile tatu za awali itaifanya ifikisha tisa ambazo hazijawahi kuzipata hata ukizichanganya pointi zote za fainali mbili za awali za CHAN za 2009 na 2020 ambazo ni nane tu.

Hata hivyo, ni lazima Stars ifanye kitu mbele ya Madagascar iliyolazimishwa suluhu na Mauritania kabla ya kumalizana na Afrika ya Kati ambayo jioni ya jana ilikuwa ikipepetana na Burkina Faso.