TPDC YASISITIZA UMUHIMU WA KULINDA MIUNDOMBINU YA BOMBA LA GESI

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekutana na kuwapa elimu wafanyabiashara wadogowadogo wanaofanya shughuli zao ndani ya mkuza wa bomba la gesi asilia katika eneo la Kinyerezi Mwisho, Mtaa wa Kanga na Kibaga ili kuweza kuondoka eneo hilo ambalo sio rasmi na salama kwa shughuli zozote za kibinadamu ikiwemo kufanya biashara.

Akizungumza leo Agosti 7, 2025 Jijini Dar es Salaam, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka TPDC, Bw. Oscar Mwakasege, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao juu ya athari zinazoweza kujitokeza endapo wataendelea kufanya shughuli za kibiashara katika mkuza wa bomba la gesi.

“Kufanya biashara ndani ya mkuza wa bomba la gesi siyo salama, kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu binafsi na pia kuathiri uchumi wa taifa endapo ajali ya bomba itatokea,” amesema Mwakasege.

Amesema kuwa bomba hilo la gesi linalotoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni miundombinu muhimu kwa ustawi wa taifa, ikiwemo kuimarisha sekta ya viwanda, kuongeza wawekezaji, na kutoa umeme wa uhakika.

Kwa upande wa wafanyabiashara hao wametoa shukrani kwa TPDC na Serikali ya Mtaa kwa kuwapa elimu kabla ya zoezi la kuwaondoa kuanza rasmi, hivyo wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa ujazaji wa kifusi kwenye bwawa la Kanga, ili waweze kuhamia katika eneo hilo ambalo limetengwa rasmi kwa ajili yao.

Nae Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kanga, Shamte Mkali amesema kuwa eneo la bwawa la Kanga liliombwa mahsusi na wafanyabiashara hao kwa ajili ya kuendeleza biashara zao, na Serikali iko katika hatua ya awali ya maandalizi kwa kuanza na ujazaji wa kifusi.

“Tunaishukuru TPDC kwa ushirikiano. Tayari tumeshawasilisha maombi rasmi kwa TPDC kusaidia kifusi ili kufukia bwawa hilo. Tunataka kuwaondoa wafanyabiashara katika eneo la sasa ambalo ni hatarishi na kuwapeleka mahali salama,” alisema mwenyekiti huyo.